img

Miaka 20 nchini Afghanistan: Je Marekani ilifanikiwa ?

July 24, 2021

Dakika 12 zilizopita

Vita vya miaka 20 Afghanistan vimesababisha machungu ya aina yake kwa Marekani

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Vita vya miaka 20 Afghanistan vimesababisha machungu ya aina yake kwa Marekani

Uamuzi wa Biden wa kuondoa wanajeshi wa Marekani kutoka Afghanistan kufikia Septemba 11, 2021 umechukuliwa na mtazamo tofauti kote duniani.

Kuna wale wanachoshikilia kwamba ndio uamuzi stahiki na kudai imekuwa safari ndefu ambayo haikufanikiwa kufikia malengo yake ingawa pia kuna wakosoaji wake ambao wanachukulia kuwa hakukutolewa muda wa kutosha kwa Afghanistan kujitayarisha ipasavyo katika utekelezaji wa jukumu la kujilinda yenyewe kikamilifu.

Wakati huo Biden akiwa makamu rais, alikuwa anaunga mkono usaidizi wa kijeshi na kibinadamu kujenga tena Afghanistan baada ya Marekani kuondoa utawala wa serikali ya wanamgambo wa Taliban kwasababu ya kumuunga mkono kiongozi wa kundi la al- Qaeda Osama bin Laden, mratibu wa shambulizi la kigaidi lililotokea Septemba 11, 2001 nchini Marekani.

Kipindi hicho, Joe Biden alitembelea Afghanstani katika ziara rasmi kukutana na rais wakati huo Hamid Karzai kujadiliana hali nchini humo, lakini walitofautiana na kulingana na waliokuwa karibu, hafla ya chakula cha jioni ilikasitishwa ghafla bila kutarajiwa.

Bwana Biden alimaliza ziara yake akihisi kuwa vita vya Afghanistan ni kama mtego kwa Washington na huenda Marekani ikakosa kuvishinda.

Na aliporejea Marekani moja kwa moja alitoa onyo kali kwa aliyekuwa rais wakati huo Barack Obama kwamba ”sasa sio wakati wa kuongeza wanajeshi wetu Afghanistan”.

Kipindi hiki ambapo Joe Biden ndio rais, ameamua kuondoa wanajeshi wake licha ya pingamizi kutoka kwa baadhi ya wataalam wa jeshi, wabunge wa Democratic na Republican na mafisa wa mashirika ya kutoa msaada.

Mtangulizi wa Biden, Donald Trump alifikia makubaliano na Taliban kwamba wanajeshi wote wa Marekani wataondoka nchini Afghanistan kufikia Mei mwaka huu na vyanzo vinasema kuwa Biden alikuwa na wasiwasi kwamba kukiukwa kwa makubaliano hayo huenda kungesababisha tena mashambulizi zaidi dhidi ya wanajeshi wa Marekani na kuwa sababu ya kuendeleza vita hivyo.

‘Raia wa Afghanistan waamue hatma yao’

Akitetea uamuzi wake, Rais Biden amekiri kuwa huenda kukazuka tena vita vipya vya wenyewe kwa wenyewe huko Afghanistan lakini akarejelea kwamba nchi yake imejitolea kuondoa wanajeshi wake nchini humo huku Marekani ikiendeleza kuunga mkono usaidizi wa kidiplomasia na kibinadamu na kusisitiza kuwa hatma yao ipo mikononi mwao.

Tukio la ulipuaji wa ubalozi wa Marekani jijini Nairobi

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Tukio la ulipuaji wa ubalozi wa Marekani jijini Nairobi

”Raia wa Afghanistan, ni lazima waamue hatma yao badala ya kuweka kizazi kingine cha Marekani hatarini kwa vita ambavyo haiwezi kushinda”.

Biden alisema kuwa jeshi la Afghan lina uwezo wa kukabiliana na kundi la Taliban.

Vita hivyo vya muda mrefu ambavyo vimekuwa vikiendelea kwa kipindi cha miaka 20, Biden alisema kuwa Marekani ilifikia lengo lake: ikiwa ni kukabiliana na kundi la wanamgambo wa Al-Qaeda na kuzuia mashambulizi zaidi dhidi ya Marekani kama lililotokea Septemba 11, 2011.

Mratibu wa shambulizi hilo, Osama bin Laden aliuliwa na timu ya wanajeshi wa Marekani mwaka 2011.

“Tulifikia malengo hayo, na hiyo ndio sababu tulienda huko. Hatukwenda Afghanistan kujenga taifa. Na ni haki na wajibu wa raia wa Afghan peke yao kuamua hatma yao na namna wanavyotaka kuendesha nchi yao,” Biden alisema.

Bwana Biden pia alitoa wito kwa nchi za eneo hilo kusaidia kuleta utulivu wa kisiasa kati ya pande zinazozozana. Alisema kuwa serikali ya Afghan inastahili kutafuta makubaliano na kundi la Taliban ili kuwezesha kuishi kwa amani kwa pamoja.

wanawake waomboleza nje ya hopsitali nchini Afghanistan kufuatia shambulio la bomu

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

wanawake waomboleza nje ya hopsitali nchini Afghanistan kufuatia shambulio la bomu

Hata hivyo, kile ambacho kimekuwa kikilaumiwa ni uongozi mbaya wa Afghanistan ambao ulilemaza uthabiti na kuruhusu Taliban kupenyeza tena.

Pia utawala wa Biden ulijaribu kutathmini tishio la ugaidi nchini Afghanistan hii leo, na kuhitimisha kwamba athari zake ni ndogo ikilinganishwa na maeneo mengine ya Afrika na Mashariki ya Kati.

Mfano, nchini Somalia, kundi la Al-Shabab linaendelea kujitanua na kuongeza nguvu yake pamoja na ushirikiano na kundi la al-Qaeda.

Makundi kadhaa yenye kuhusishwa na Al-Qaeda na ISIS pia yanaendesha shughuli zao eneo la Mali na mengineo ya jangwa la Sahel na Afrika Kaskazini. Hivyobasi, hata kama Taliban haitakuwa tayari kukatiza uhusiano wake na kundi la Al-Qaeda tishio hilo sio tofauti ikilinganishwa na maeneo mengine dhidi ya Marekani na washirika wake.

Wakosoaji wa Biden

Baadhi ya wakosoaji wa Joe Biden wanasema kuwa kuondoka kwa wanajeshi Afghanistan kulingana na uhalisia wa hali ilivyo kunaweza kusababisha kuimarika kwa mazingira ya kundi la Taliban na huenda hatua hiyo likapelekea kusutwa kwa utawala wa Biden siku zijazo.

“Kwa namna mbalimbali, gharama ya kuendelea kuwepo inaonekana kuwa ya muda mfupi itakayolemea upande wa Marekani lakini gharama ya jeshi hilo kuondoka itagharimu raia wenyewe wa Afghanistan tena kwa kipindi kirefu,” aliandika Madiha Afzal wa Taasisi ya Brookings katika gazeti la Washington Post mapema mwezi huu.

Jingine ambalo halikuzungumziwa na Rais Biden ni jukumu la kimaadili kwa Marekani dhidi ya mamilioni ya raia wa Afghan ambao kwa usadizi wa Marekani wameanza maisha mapya kwa uhuru na kujenga jamii ya kisasa zaidi.

Hata hivyo, ingawa rais hakulizungumzia, lilijitokeza ni sifa ya Marekani ambayo huenda ikajitokeza kama yenye kuacha kuunga mkono washirika wake katikati ya kipindi ambacho wanawahitaji sana.

Na hii sio mara ya kwanza

Mara ya kwanza ni mwaka 1973 katika vita vya Vietnam, Beirut mwaka 1983 baada ya kambi za jeshi la majini la Marekani kuvamiwa kwa mabomu, Somalia mwaka 1995 huku Iraq ikinyolewa kwa wembe ule ule mwaka 2011 na sasa hivi ikiwa Afghanistan.

Ni wazi kwamba kutokana na matukio ya awali, kundi la Taliban linaweza kutumia tajriba za miaka ya nyuma na kupata shauku ya kupenyeza zaidi katika miji ya Afghanistan.

Uamuzi wa Biden wa kuondoa majeshi yake Afghanistan huenda kukaakisi kwamba Marekani haina subra katika utekelezaji wa mkakati wake licha ya kuwa kuna wale wanaoona kwamba Afghanistan ilipewa fursa na ikashindwa kuitumia vizuri.

“Raia wa Afghan tumewapa ulinzi kupitia maelfu ya wanaume na wanawake waliopoteza maisha yao, mamia ya mabilioni ya raia wetu, na takriban miaka 20 baadye, serikali ya Afghan ingekuwa imejipanga na kuhakikisha majadiliano na wanamgambo kumaliza tofauti zao,” amesema Daniel Davis, luteni kanali wa jeshi la Marekani aliyestaafu ambaye alikuwa Afghanistan mara mbili. “Walipoteza fusa hiyo.”

Pengine huenda ikawa kutatua mgogoro wa nchini humo kwa njia ya kijeshi kusiwe suluhu la kudumu lakini pia uamuzi wa Biden wa kujiondoa nchini humo bila masharti yoyote kunaweza kuwa uamuzi wa kushindwa.

Hatua hiyo inaweza kuchukuliwa kama ushindi kwa kundi la Taliban na kuonesha kufeli kwa Marekani.

Giza linaloandama Afghanistan

Hatma ya kisiasa nchini Afghanistan ikoje?

Vita vya wenyewe kwa wenyewe, mauaji ya makumi ya maelfu ya raia wa Afghanistan kila mwaka huenda kukapungua. Lakini ikiwa kundi hilo litachukua uongozi na kuendeleza mfumo wake wa awali, bila shaka yoyote, mkondo wa kisiasa, haki za kibinadamu, uhuru kwa raia ni miongoni mwa vitakavyo athirika.

Wakati huo huo, Taliban inaendelea kupinga kufanyika kwa uchaguzi kwa njia ya demokrasia ambako kunaweza kuwaondoa madarakani na badala yale linapendelea mfumo sawa na wa Iran wa kiongozi mkuu wa kidini.

Pia Taliban inataka kujumuisha wapiganaji wake katika jeshi la Afghanistan na kikosi cha ujasusi.

Hadi kufikia sasa kumekuwa na tetesi kwamba kundi hilo limeanza kuingia katika maeneo mengine ya nchi hiyo na hilo linaendelea kuzua wasiwasi wa kuzuka kwa vita vya wenyewe wenyewe.

Sasa je, hatua iliyochukuliwa na Biden inaashiria kushindwa kwa Marekani?

Source link

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *