img

Super League: Kwanini vilabu vikubwa vya soka vinaanzisha ligi mpya?

April 20, 2021

Saa 4 zilizopita

MICHAEL REGAN

Chanzo cha picha, MICHAEL REGAN

Mpango wa baadhi ya vilabu vikubwa duniani kuanza Ligi Kuu ya Ulaya (ESL), umesababisha upinzani mkubwa na kutishia kusambaratisha nia ya vilabu hivyo vya bara Ulaya .

Vilabu vinavyohusika vimesema ESL itakuwa na manufaa katika soka kwa ujumla lakini wakosoaji wanasema hatua hiyo imetokana na ulafi.

Ni timu gani zinazotaka kujiunga na Ligi Kuu ya Ulaya (ESL)

Vilabu 12 tayari vimetia saini – sita kutoka Ligi Kuu ya Uingereza.

Arsenal, Chelsea, Liverpool, Manchester City, Manchester United na Tottenham zitajiunga na AC Milan, Atletico Madrid, Barcelona, Inter Milan, Juventus na Real Madrid.

Vilabu hivyo vinataka kuwepo na michuano mingine ya mashindano katikati ya wiki na kuendelea kushindana katika ligi za taifa.

ESL itakuwa na timu 20. Kati ya hizo, 12 ni waanzilishi pamoja na tatu ambazo bado hazijajiunga – zitakuwa za kudumu na hazitawahi kushushwa daraja.

Nyingine tano zitakuwa zinafuzu kuingia kila mwaka.

Ligi mpya itakuwa ni wapinzani wa mashindano Ligi ya Mabingwa ya sasa, moja ya michuano mikali baina vilabu katika soka.

Kwanini mpango huo unapingwa?

Hatua hiyo imeshutumiwa na mashabiki, wachambuzi na pia kwa sababu bodi nyingi za soka hazikuhusishwa.

Kukiwa na timu 15 katika ESL ambazo hazipiganii kufuzu au kuhofia kushushwa daraja, wakosoaji wanasema hilo litasababisha kundi fulani katika ngazi ya juu ya soka.

Ligi ya Primia imesema “itadhuru kanuni za michuano na faida za mchezo huo”.

Katibu Oliver Dowden amesema mipango hiyo inatishia mfumo wa soka Ulaya, “ambako pesa kutoka Ligi ya Primia ambayo imekuwa na mafanikio makubwa duniani zimekuwa zikielekezwa hadi ligi zingine na hadi kwenye jamii”.

Pia kuna hofu kuwa ESL itapata mashabiki wengi duniani kushinda ligi zilizopo kama vile Ligi ya Primia ya Uingereza na Serie A ya Italia.

Kwanini timu zinataka Ligi Kuu ya Ulaya?

Inaonekana pesa ndio kichocheo kikubwa.

Vilabu vya soka vimeathirika pakubwa kimapato kutokana na janga la virusi vya corona ambalo lilisababisha kuahirishwa kwa baadhi ya mechi na pia mechi zimechezwa bila watazamaji.

Vilabu vikubwa vina wachezaji nyota ambao wanapokea mamilioni ya pauni na wanahitaji kulipwa.

Vilabu waanzilishi vinachochewa na mgao wa €3.5bn (£3bn) kama ruzuku zinazotolewa na benki ya JP Morgan.

ESL inasema kuwa ligi mpya “itasaidia katika ukuaji mkubwa wa uchumi na kuunga mkono soka ya Ulaya”.

Je Ligi Kuu ya Ulaya itaendeshwa vipi?

Chini ya pendekezo hilo, ESL itaanza Agosti kila mwaka huku kukiwa na mipango ya kuizundua “haraka iwezekanavyo”.

Ligi hiyo ya timu 20 itagawanywa katika makundi mawili ya timu 10, zikicheza dhidi ya kila mmoja nyumbani na ugenini.

Timu tatu za kwanza katika kila kundi zitafuzu robo fainali huku timu za nambari nne na tano zikicheza mechi ya mikondo miwili kwa sehemu mbili zilizobaki.

Kuanzia hapo na kuendelea, itakuwa na muundo sawa na ule wa Ligi ya Mabingwa wa mechi za mikondo miwili kabla ya fainali ya awamu moja mwezi Mei.

Kipi kinafanywa kusitisha ESL?

Uefa, bodi ya soka Ulaya imekuwa na matumaini kuwa mipango ya Ligi ya Mabingwa ya timu 36 – yatasitisha uundaji wa Super League.

Bodi za michezo zimesema “zitaendelea kushirikiana” kwa kujaribu kusitisha ligi kwa kutumia njia ya kisheria na hatua za kimichezo ikiwa kutakuwa na haja ya kufanya hivyo.

Rais wa Uefa ameonya kuwa vilabu vitapigwa marufuku kushiriki michuano mingine yoyote nyumbani na kimataifa.

Pia wachezaji watazuiwa kuwakilisha timu zao za taifa katika Kombe la Dunia.

Je serikali ina uwezo wa kusitisha timu za Uingereza kushiriki ligi hiyo?

Waziri Mkuu Boris Johnson amesema serikali “itafuatilia na kufanya kila inaloweza na mamlaka ya soka kuhakikisha hatua hii aiendelei kwa namna ilivyopendekezwa”.

Alipoulizwa ikiwa serikali inaweza kuondoa mikopo iliyochukuliwa wakati wa virusi vya corona na vilabu msemaji wa Downing Street alisema inafuatilia machaguo yote.

Nini kinafuata?

Itategemea zaidi na timu gani nyingine zitakazosaini.

Bayern Munich, Borussia Dortmund na Paris St Germain – vilabu vikubwa Ujerumani na Ufaransa – bado havijathibitisha kushiriki.

Shirikisho la soka duniani , Fifa, awali lilikuwa limesema halitatambua na kuwezesha kuanzishwa kwa ligi hiyo.

Fifa imeonesha “kutounga mkono” ligi hiyo na kutoa wito kwa “washiriki wote kujadiliana kwa utulivu, kwa namna yenye kuleta tija na usawa kwa manufaa ya mchezo”.

Wakati huo huo, ESL itajitahidi kuzuia vikwazo vyovyote kutoka Uefa na Fifa ambavyo kuwekwa ili kuzuia kuanzishwa kwa ligi hiyo.

Source link

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *