img

RC Mahenge aagiza jeshi la polisi kuwakamata waliohusika wizi wa mashine kwenye kiwanda cha muwekezaji

April 20, 2021

Na Ezekiel Mtonyole – Dodoma.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt Binilith Mahenge ameliagiza jeshi la polisi Mkoa wa Dodoma kuwatafuta na kuwakamata na kuwafikisha katika vyombo vya sheria watu wote waliohusika katika wizi wa mali mbalimbali katika kiwanda cha kuchinja nyama cha S & Y Group kilichopo kata ya Zuzu pembezoni mwa jiji la Dodoma.

Dkt Mahenge ametoa agizo hilo leo April 20, 2021 wakati alipofanya ziara ya kushtukiza katika kiwanda hicho na kukuta kiwanda kikiwa hakifanyi kazi na kupata ripoti ya msimamizi kuwa kiwanda mara baada ya kusimama uzalishaji kwa muda, ndio watu wasiojulikana waling’oa baadhi ya mitambo, mashine, mot ana vifaa mbalimbali.

Amelitaka jeshi la polisi kushirikiana na makampuni yote ya ulinzi yaliyowahi kufanya shughuli za ulinzi katika kiwanda hicho kuwasaka watu waliohusika au kusababisha upotevu wa mali hizo kuwasaka na kuhakikisha mali hizo zinapatikana ili kuepusha hasara anayoweza kupata muwekezaji.

“Nikuombe RPC muwasake watu hawa wote waliohusika, kwanza muanze na makampuni haya ya ulinzi hawa ndio watawaonyesha mali zilizoibiwa zilipelekwa wapi au ziliuzwa wapi, hakikisheni mnawakamata wote waliotajwa kwenye ripoti hii” amesema Dkt Mahenge.

Amesema serikali inataka wawekezaji ndio maana ikaanzisha ofisi ya kituo cha uwekezaji na sasa imeundiwa Wizara kamili lengo ni kuwalinda wawekezaji wanaokuja kuwekeza na hivyo haitawavumilia wale wote wanaokwamisha wawekezaji kuja kuwekeza hapa nchini.

Amemtaka muwekezaji wa kiwanda hicho kukaa pamoja na kituo cha uwekezaji TIC pamoja na jeshi la polisi kushirikiana ili kumaliza tatizo la upotevu wa mali hizo kwa kutoa nyaraka mbalimbali zitakazowezesha kupatikana kwa mali zilizoibiwa.

“Hii nchi ni salama na najua muwekezaji huko aliko anasema hiyo nchi si salama kwa uwekezaji, lakini ukiangalia ni tamaa za watu wachache sasa mimi nataka mali hizo zipatikane haraka ili hata huyu muwekezaji ajue serikali ipo” amesema.

Pia ameagiza kukutana kwa kituo cha uwekezaji TIC Mkoa wa Dodoma na muwekezaji huyo ili kufanya tathmini ya uwekezaji wake ili kujua kwanini kiwanda hicho kilisimama kufanya kazi kisha watatue changamoto hizo ili kiwanda kiendelee na kazi ili watanzania wengi waendelee kupata ajira katika kiwanda hicho.

Aidha amewataka wawekezaji pindi wanapotaka kuwekeza wahakikishe wanawasiliana na mamlaka husika ili kupata kampuni za ulinzi zilizo kwenye orodha ya makampuni yaliyosajiliwa na serikali ili kuepuka vitendo vya wizi na kutapeliwa mara kwa mara.

Awali msimamizi wa kampuni ya S & Y Group inayomiliki kiwanda cha kuchinja nyama cha S & Y Garment meat product. Co LTD, na kiwanda cha kutengeneza material ya ujenzi cha S & Y Wood Product CO LTD, Bw. Titus Gembe amesema viwanda vyote viwili vilianza kunya kazi mwaka 2016.

Huku akibainisha kuwa kiwanda cha nyama kilikuwa na uwezo wa kuchinja ng’ombe 200 na mbuzi 1000 kwa siku na kilikuwa na uwezo wa kuajari wafanya kazi 100 hadi 1200, na kiwanda cha kutengeneza vifaa vya ujenzi kilikuwa na uwezo wa kuajiri wafanyakazi 45 hadi 55 katika shughuli zao.

Amesema kiwanda cha nyama kilisimama mara baada ya kukosa soko la uhakika kwa kuwa hawakupata soko la ndani bali bali bidhaa zao zote zilikuwa zikiuzwa China, amebainisha kuwa kwa sasa kiwanda kimepata afisa masoko mpya raia wa China mwenye uzoefu na masoko ya nyama katika nchi za mashariki ya kati, hivyo isingekuwa wizi wa mashine wangeanza uzalishaji.

Ametaja baadhi ya vifaa vilivyoibiwa kuwa ni jenereta kubwa, mashine za kukatia nyama, mota na betri kubwa vitu hivyo vyote vilikuwa vikitumika katika kiwanda cha nyama.

Kwa upande wake Kamanda wa polisi Mkoa wa Dodoma SACP Gilles Muroto ameahidi kutekeleza maagizo yote ya kuhakikisha mali za kampuni hiyo zinapatina na kurudishwa katika kiwanda hicho huku akishauri zinapotokea kesi za wizi watu walipoti haraka katika jeshi la polisi kwa hatua zaidi.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *