img

Mzozo wa madereva wa malori Dangote kutafutiwa suluhu

April 20, 2021

Waziri wa viwanda na biashara wa Tanzania, na mwenzake anaeshughulikia uwekezaji wamefika katika kiwanda cha uzalishaji wa saruji cha Dangote Mkoani Mtwara kusini mwa nchi hiyo, kwa ajili ya kusuluhisha mzozo wa madereva wa malori wapatao 500 waliogoma kufanya kazi ya kusambaza saruji nchi nzima kwa siku 12, kutokana na madai ya kuwepo kwa vitendo vya ukandamizaji. 

Mawaziri waliofika Mkoani hapa ni waziri wa viwanda na Biashara Profesa Kitila Mkumbo na Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji Geofrey Mwambe ambapo wamefanya mazungumzo yaliyodumu kwa zaidi ya saa sita na pande zote tatu ambazo ni uongozi wa kiwanda cha Dangote, mawakala wa ajira na madereva.

Madereva wamefanya mgomo huo wa siku 12 kutokana na kuwepo kwa madai kumi ambayo hayakufanyiwa kazi kwa muda mrefu na mengine wakidai tangu kiwanda hicho kianzishwe miaka minne iliyopita, huku uongozi wa kiwanda hicho ukishitumiwa kwa vitendo vya unyanyasaji, kutishia usalama, kutowalipa kwa wakati, kutowalipia faini za barabarani na kadhalika.

Uongozi wa kiwanda hicho wakubali kushughulikia malalamiko yaliyotolewa na madereva

Kutokana na mazungumzo hayo uongozi wa kiwanda hicho umekubali kutekeleza madai nane kati ya kumi yaliyokuwa yanalalamikiwa na madereva hao, huku waziri wa viwanda na biashara Profesa Kitila Mkumbo akisema serikali inawathamini wafanyakazi hao na itaendelea kutetea haki zao.

“Kuna majukumu ya serikali na kuna majukumu yenu nyie wafanyakazi na majukumu ya mwekezaji, ukiacha hilo ambalo sisi serikali tunaliangalia sana, tunataka sheria na haki za watu zizingatiwe kikamilifu”

Kwa upande wake Waziri wa Uwekezaji Geofrey Mwambe amezungumzia umuhimu wa kuthamini uwekezaji nchini Tanzania.

“Wakati tunawashawishi wawekezaji, kwamba njooni muweke Tanzania, mazingira ni mazuri, watanzania ni wa pole, waelewa tunachapa kazi, sio watu wa visingizio kila siku tunaumwa, mtapata faida, huwa tunasema hivyo tukienda huko nje. Aah.. tukasema kwamba ni haki kwa watumishi kusema kitu kwa mwajiri wao kwa namna hiyo tukajuwa mnaongea na FS ambao ndio waajiri wenu ingawa baada ya kupata taarifa ikaonekana kwamba kumbe mgomo huo umesimamisha kabisa shughuli za usafirishaji wa saruji sasa tukasema anayehumia sio FS anayeumia ni Dangote ambaye ametumia kama Trilion 1.4 hiki kiwanda chote” ameeleza Mwambe.

Abillahi Babaa ni mtendaji mkuu wa kiwanda cha Dangote ameahidi kutekeleza yote waliyokubaliana na madereva hao.

“Muna nguvu kubwa sana sana katika shughuli yetu hii ya biashara, nataka kuwahakikisha kwamba makubalianao yote yaliyofanywa ambayo nimeshika orodha yake yote yatatekelezwa nukta hadi nukta”

Madereva nao wanasema nini juu ya hatua hiyo?

“Naomba kama tunaamua kurudi kazini ili litambulike kwamba tunarudi kazini tufanye kazi wakati tunajuwa kwamba Dangote wamefanya nini na wataendelea kufanya nini, sasa mimi kama mimi nawasihi wafanyakazi wenzangu kama tuko ridhaa na kuendelea na kazi basi tuendelee na kutokana na mwitikio wa majina yetu nadhani kila mtu yuko tayari kuendelea na kazi”.

Hata hivyo, baada ya mazungumzo hayo madereva waliokuwa tayari kuendelea na kazi walitakiwa kujiorodhesha kwenye orodha maalumu na kuanza kazi mara moja.

 

 

 

Source link

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *