img

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Ndumbaro ampa masharti mwekezaji ili kufungua Ranchi ya Wanyamapori

April 19, 2021

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro amemtaka Mwekezaji wa hoteli iliyopo pembezoni mwa ziwa Chala katika wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro kuhakikisha anawasilisha mchoro wa ramani ya eneo lake  utakaoonyesha mipaka ya eneo lake, pamoja na njia itakayoruhusu wananchi kuweza kufika katika ziwa  hilo pasipo kupita katika eneo la hoteli hiyo kabla ya kupewa kibali cha  kufungua Ranchi ya wanyama katika eneo hilo.

Akizungumza mara baada ya kutembelea nao katika  eneo hilo kuwa nia, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.  Damas Ndumbaro  ambaye aliambatana na Naibu waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Mary Masanja, Katibu Mkuu, Alan Kijazi, Waziri wa Kilimo Prof Adolf Mkenda ambaye  pia ni mbunge wa jimbo hilo, pamoja na wataalamu mbali mbali wakutoka TAWIRI, TANAPA na TAWA.

Amesema kwa mujibu  kwa sheria za Tanzania ziwa ni  mali ya umma hivyo  kila mwananchi anayo  haki   ya kunufaika  na ziwa  hilo bila  kuathiri mfumo wa ikolojia wa ziwa hilo.

“Eneo hilo la Mwekezaji lipo ndani ya Ushoroba wa Wanyamapori unaounganisha Hifadhi ya Tsavo (Kenya) na Kilimanjaro (Tanzania), na kwa mujibu wa Kanuni zinazosimamia Ushoroba, shughuli zinazoruhusiwa ni zile ambazo zinaendana na uhifadhi, hivyo Mwekezaji ameshauriwa kuomba leseni ya kuendesha Ranchi ya Wanyamapori ambayo inaendana na matakwa ya Kanuni hiyo ya Ushoroba ya mwaka 2020, “alisema Waziri

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mary Masanja  amesema  Wizara imedhamiria kuhakikisha   inalinda na kuhifadhi rasilimali za utalii ikiwa ni mbinu pekee ya kuongeza wigo wa  kuvutia Utalii.

“Sisi kama wizara  kanuni yetu  ni kuhifadhi na kutunza utalii ikiwa ni pamoja na kuhakikisha  kwa kushirikiana na wadau wa sekta binafsi kuongeza vivutio vya utalii na kuweka mazingira bora kwa wawekezaji  katika sekta hii, “alisema Naibu Waziri Masanja

Amesema  wapo kwenye mazungunzo ya kina na nchi jirani ya Kenya ili kuona namna watakavyomsaidia mwekezaji  huyo  kufungua  ranchi ya wazi itakayosaidia kuingiza wanyama wote.

Aidha Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Dkt. Anna Mghwira, alisema kumalizika kwa mgogoro huo kutasaidia ongezeko la utalii na kukuza pato la nchi.

” Endapo Mwekezaji atakamilisha maelekezo ya mchoro kwenye ramani ya hekari zaidi ya 570  ataweza kupewa leseni itakayomsaidia kufungua Ranchi itakayosaidia wanafunzi kujifunza, ongezeko la watalii na kukuza uchumi wa nchi,” alisema.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo hilo, Prof Adolf Mkenda alisema lengo la kumaliza tatizo hilo ni ili kumpa fursa kuwa na mazingira mazuri ya uwekezaji, kuongeza mapato kwanzia ngazi ya Halmashauri  hadi taifa.

 

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *