img

Serikali kuzindua Afua ya upimaji wa Malaria ngazi ya Kaya katika maadhimisho ya siku ya Malaria

April 19, 2021

Serikali kupitia wizara ya afya  inatarajia kuzidua utekelezaji wa afua ya kupambana na ugonjwa wa malaria nchini kwa kuanzisha upimaji wa malaria kwa wananchi katika kaya baada ya 

mmoja wao kugundulika ana maambukizi ya ugonjwa huo katika kituo cha afya.

Haya yamesemwa na Dkt Samwel Lazaro naibu meneja mpango wa kuthibiti malaria wakati akifunga mkutano wa waandishi wa habari kuelekea maadhimisho ya siku ya malaria duniani ambayo kitaifa yanatarajiwa kufanyika mkoani Arusha ambapo alisema kuwa Afua hiyo itazinduliwa na waziri wa afya maendeleo ya jamii, jinsia, wazee ma watoto Dkt Doroth Ngwajima.

Dkt Samwel alisema kuwa mikoa itayoanza na utekelezaji wa afua  hiyo kwa awamu ya kwanza ni Arusha, kilimanjaro na Manyara ambapo mwakani wataongeza mkoa wa Njombe na mwaka 2023 wataongeza mkoa mwingine wa Iringa.

“Afua hii mpya inalenga kuhakikisha mikoa hii mitano inafikia kiwango cha maambukizi ya malaria kwa asilimia 0 ifikapo mwaka 2025 ambapo katika utelelezaji wake itakuwa  ni kupima watu katika kaya  ambapo kitakachofanyika ni mgonjwa atakapogundulika ana malaria atakapoenda kupima katika kituo cha kutolea hutuma basi kutakuwa na ufuatiliaji katika ngazi ya kaya kwa wanakaya wote kupimwa ili kutibu na kuzuia kuendelea kusambaa kwa ugonjwa huo,” Alieleza Dkt Samwel.

“Pia ikigundulika kuwa kunamazalia au chanzo cha mbu katika jamii hiyo kutakuwa na afua nyingine ya kuhakikisha hayomazalia aidha ni madimwi yatapigwa dawa ili kuua mazalia hayo na mwisho wa siku ile jamii tutakuwa tumeikinga na maambukizi ya malaria,” Alifafanua.

Aidha aliiomba jamii kushiriki kikamilifu kuhakikisha wanautokomeza ujonjwa wa malaria katika mikoa hiyo ifikapo mwaka 2025 ambapo mpango huo unawataka kupunguza malaria kufikia chini ya asilimia 3.5 kama nchi kwenye mikoa 5 ambayo iko chini katika maambukizi ya ugonjwa huo itahusika katika utokomezaji wa malaria kwa miaka mitano.

Kwa upande wake Mkuu wa ufuatiliaji na tathimini kitengo cha malaria Dkt Sejenunu Aron alisema kuwa wanataka wafikie malengo ya Tanzania kutokuwa na malaria kabisa ambapo hadi sasa wameweza kupunguza  wingi wa watu wanaopata malaria kwa asilimia 50 kutoka asilimia 14.8 ya mwaka 2015.

“Sambamba na hayo  idadi ya vifo vitokanavyo na malaria imepungua kwa asilimia 61 huku mikoa ya Kigoma,Geita , Kagera,Mtwara na Ruvuma ikiea na kiwango cha juu ya asilimia 9 ya maambukizi ya Malaria,”Alisema Dkt Sijenunu.

Alifafa nua kuwa Kigoma maambukizi yapo kwa asilimia 24.4, Geita 17.3, Kagera 15.4, Mtwara 14.8 na Ruvuma 11.8, huku mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Mbeya na Songwe wakiwa chini ya asilimia 1.

kwa upande wake Charles Mwalimu kutoka wizara ya afya kitengo cha uthibiti wadudu wanaoeneza magonjwa alisema alisema kuwa lengo la udhibiti ni kupunguza maambukizi ya malaria kutoka kwa mbu  kwenda kwa binadamu.

“Mikakati yetu ni kuweza kumuua mbu au kumzuia asiweze kumfikia binadamu kwa kuhimiza matumizi ya vyandarua vilivyowekwa viuatilifu vya muda mrefu, unyunyuziaji wa viuatilifu kwenye kuta za nyumba pamoja na udhibiti wa mazalia ya mbu katika mazingira na hizi ni njia zilizoonyesha kuwa na uwezo mkubwa,” Alisema.

Naye mkuu wa kitengo cha vipimo, matibabu na dawa kinga za malaria Dkt Abbdallah Lusasi wanataka wapunguze vifo vitokanavyo ma malaria kwa asilimia 85 hasa kwa makundi hatarishi ya wajawazito na watoto kwani madhara ya malaria kwa mjamzito ni pamoja na kupata upungufu wa damu, mimba kuharibika, kujifungua mtoto njiti au mwenye uzito pungufu, kujifungua mtoto mfu, afya ya mama kudhoofika ikiwa ni pamoja na kuweza kutokea kifo kwa  mama na mtoto.

“Wajawazito wapo katika hatari zaidi ya kupata maambukizi ya ugonjwa wa malaria kuliko watu wengine kutokana na mwili wake kupunguza nguvu ya kupambana na magonjwa ambapo vimelea vya malaria vinaweza kujificha kwenye kondo la nyuma la mama na kuathiri ukuaji wa mtoto,”Alieleza Dkt Lusasi.

 

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *