img

Je, mjadala wa Magufuli kukoma bungeni baada ya kukemewa na Rais Samia?

April 19, 2021

Dakika 3 zilizopita

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan

Chanzo cha picha, Ikulu Tanzania

Ni mjadala ambao umeliteka Bunge la Tanzania, ukapamba moto mitandaoni na kwenye vyombo vya habari.

Ni mjadala ambao umeonekana ‘kumkera’ Rais Samia Suluhu Hassan.

Mjadala wenyewe ni miongoni mwa wabunge wa chama kinachoongoza dola, CCM. Wabunge ambao wamegawanyika katika makundi mawili, wanaotetea rekodi ya rais aliyepita John Magufuli na ambao wanaoonekana kukosoa baadhi ya mambo ya utawala huo.

Baada ya wiki nzima ya mjadala jana akiwa katika Kongamano la viongozi wa Dini mjini Dodoma Rais Samia alieleza kuwa hafurahishwi na mjadala huo.

Viongozi wa dini na serikali wakiomba dua

Chanzo cha picha, Ikulu Tanzania

Akizungumza katika kongamano la viongozi wa dini uliofanyika jijini Dodoma, Rais Samia lionesha kukerwa na namna bunge linavyojadili ajenda zisizo za kitaifa kwa kumlinganisha yeye na mtamngulizi wake Hayati John Magufuli.

”Inasikitisha sana kuona kwamba watu wanapiga ngoma mitandaoni, lakini ngoma ile inachezwa bungeni, kwa kulinganisha watu na sio kulinganisha ajenda za kitaifa, ajenda ya kitaifa ni moja, mnalinganisha Magufuli na Samia hawa watu ni kitu kimoja.”

”Awamu ya sita haikutokana na uchaguzi, haikutokana na chama kingine cha siasa, imetoka ndani ya chama cha Mapinduzi, imetokana na uongozi uliokuwepo wa awamu ya tano.” Alisema Rais Samia.

”Awamu ni maneno tu , lakini mambo ni yaleyale.

Je, ni makundi gani kinzani ndani ya CCM?

Kundi la kwanza ni lile ambalo linatetea kile kinachoitwa urithi wa hayati Magufuli, linasema unapaswa kutunzwa na kuelezewa kwa kina kila wakati nchini humo ikiwemo kuendeleza mipango na miradi mikubwa ya maendeleo iliyoanzishwa na Magufuli ikiwemo umeme wa Rufiji na Reli ya Kisasa.

Kundi hili ndilo ambalo linaamini katika ‘Umagufuli’ kwa kiasi kikubwa na sasa linaonekana kuwa na hofu kuwa huenda milango ikafungwa kwao kisiasa. Kundi hilo lina vinara watatu Joseph Musukuma (Mbunge wa Geita Vijijini),Livingstone Lusinde (Mbunge wa Mvumi) pamoja na Josephat Gwajima (Mbunge wa Kawe). Kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita Musukuma na Lusinde walikuwa wakitumika kuitetea na kuisemea serikali ya hayati Magufuli katika masuala mbalimbali ya kisiasa.

Kwa kiasi fulani kundi hili limepokea habari njema baada ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo Kassim Majaliwa kutangaza mpango wa serikali kununua ndege mpya tatu ikiwa ni mpango uliodhamiriwa na hayati Magufuli. Kwahiyo waliomuunga mkono hayati Magufuli wanakinzana na wale wote wanaokosoa upungufu uliooneshwa maeneo mbalimbali na kushauri serikali ya Rais Samia ifanye marekebisho au kuachana nayo kwa kuamini ni wasaliti wa serikali na chama.

Rais Samia amewataka wabunge kujikita kwenye ajenda za kitaifa

Chanzo cha picha, BUNGE

Kundi la pili ni lile ambalo wengi ni wahanga wa uongozi wa hayati Magufuli, na lina vinara wake wawili; Nape Nnauye (Mbunge wa Mtama) na January Makamba (Mbunge wa Bumbuli).

Wabunge hao wamewahi kuteuliwa kuwa mawiziri katika Wizara tofauti. Makamba alikuwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, ambapo hadi anatimuliwa uwaziri alipewa tuhuma mbalimbali zikiwemo kuchelewesha agizo la kukomesha matumizi ya mifuko ya plastiki na matumizi mabaya ya fedha.

Kwa Nape Nnauye akiwa Waziri wa Habari, Utamaduni,Michezo na Wasanii, alitimuliwa madarakani na hayati Magufuli.

Nape ndiye alikumbana na dhahama kubwa baada ya mkutano wake na vyombo vya habari kupigwa marufuku na Jeshi la Polisi jijini Dar es salaam na ndiyo siku ambayo alitishiwa bastola na mtu ambaye hakuikubainishwa mara moja kama ni askari au la.

Aprili 14 mwaka huu akizungumza bungeni wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2021/2022, January Makamba aliwakata Wabunge wanaotoa maoni na ushauri wenye nia njema wasibezwe wala kuhukumiwa kuwa ni wasaliti wa chama na serikali.

Aliongeza kuwa kusema nchi inahitaji umoja na utulivu na kwamba kauli za utengano,kutiliana shaka,kutuhumiana na kuhukumiana hazijengi bali zinawachanganya Watanzania.

Uthibitisho wa kundi hilo kuwa wahanga ni matukio ya January Makamba na Nape Nnauye kwa nyakati tofauti kutokana na kuvuja sauti zao mitandaoni wakimsema hayati Magufuli alipokuwa madarakani walalilazimika kwenda kuomba radhi Ikulu Dar es salaam kwa mitazamo na matamshi yao. Kisiasa Nape na Makamba hawakuwa na njia nyingine zaidi ya kumwangukia mwenyekiti wao huyo wa zamani.

Aidha, wanasiasa hao wawili ni zao la makatibu wakuu wawili wakubwa wa CCM katika nyakati tofauti, Abdularahman Kinana na Yusuf Makamba. Makatibu hao nao waliwekwa kikaangoni kwa madai ya kumsaliti mwenyekiti wao na hivyo walitakiwa kuomba radhi na kuwekwa chini ya uangalizi.

Kundi hili kisiasa haliwezi kujinasibu kuwa yapo mapatano ya aina yoyote na kwamba huu ni wakati wao wa kupumua na kunufaika na utawala mpya, hivyo hakuna sababu za kulinda urithi na ni wakati wa mwanzo mpya, linatafuta kukubalika.

Rais Samia Suluhu Hassan

Chanzo cha picha, Ikulu

Kundi la tatu, linajumuisha wale walioingizwa kwenye siasa za CCM na hayati Magufuli na wale ambao walikuwepo, lakini hawataki kuungana na kundi lolote liwe la wahanga wa Umagufuli au wafuasi wa Umagufuli. Ni kundi ambalo limejitenga kwa kuangalia upepo unakwendaje huku likijaribu kuweka kete yake kwa uongozi wa serikali na chama.

Hili ni lile linaundwa na wanasiasa waliohamia kutoka upinzani na baadhi waliokuwa nje ya siasa lakini kwa ushawishi wa hayati Magufuli waliingia kwenye siasa.

Je, kukosekana wapinzani bungeni ni ombwe?

Fatma Maghimbi alikuwa kiongozi wa kwanza wa Kambiya Upinzani Bungeni kati ya mwaka 1995 hadi 2000. Alikuwa mbunge wa Jimbo la Chakechake kupitia Chama cha Wananchi (CUF). Kuanzia mwaka 2000 Kambi ya upinzani iliongozwa na Mbunge wa Kigoma Mjini, Dk. Walid Amani Kabourou kutoka Chadema. viongozi walioongoza kambi hiyo kwa nyakati tofauti ni Wilfred Lwakatare, Hamad Rashid Mohammed na Freeman Mbowe.

Chini ya uongozi wao walikifanya CCM kiwe macho na siasa za ushindani zilijikita katika hoja.

Bunge la 2015 hadi 2020 lilikuwa na wabunge wengi wa upinzani, kabla ya baadhi yao kuvihama vyama vyao na kujiunga na CCM kisha kupewa fursa ya kugombea majimbo yaleyale.

Kwa kiasi fulani ilipunguza nguvu ya wapinzani bungeni. Katika Bunge la mwaka 2020-2025 lina wabunge wengi wa CCM, na kwa kiasi kikubwa Kambi ya Upinzani bungeni ni kama ‘imefutiliwa mbali’ kwa kuwa hakuna ladha ya siasa za ushindani tena, hivyo CCM wamegeukiana wenyewe kwa wenyewe kana kwamba ni shughuli yao ndani ya chama badala ya uwakilishi wa wananchi.

Uimara wa kambi ya Upinzani bungeni unakiimarisha chama tawala na serikali. Kukosekana kwa nguvu ya Kambi ya Upinzani kumesababisha wabunge wa CCM walumbane wenyewe, kiasi kwamba sasa wamehamia kwenye suala la nani ni msomi na si msomi.

Wabunge wenye elimu ya darasa la saba wanawaona wale wenye elimu kuwa ni wasaliti wa chama na serikali, lakini vilevile wabunge wasomi wanaowana wenzao wenye elimu ya chini kuwa hawana utaalamu wowote zaidi ya kusoma na kuandika.

Kwa mantiki hiyo kunyukana wenyewe kunasababisha kupoteza ushindani wa hoja na mawazo juu ya maendeleo, na yeyote anayekosoa sasa anaonekana msaliti wa chama na serikali. Ni chanzo cha CCM kuwakosoa wanasiasa wa upinzani walioko nje ya Bunge, kwa sababu ya ndani hakuna nguvu ya kambi ya upinzani, hivyo inawaathiri CCM wenyewe.

Wakati hayo yakitokea bungeni, CCM bado hakuna Mwenyekiti na Katibu Mkuu. Inatarajiwa mkutano Aprili 30 mwaka huu Samia Suluhu Hassan kukabidhiwa Uenyekiti wa chama hicho kupitia Mkutano mkuu, ambapo atasaidiana na Makamu Mwenyekiti Philip Mangula na Naibu Katibu mkuu, Dk. Abdulla Juma Sadallah.

Je ujio wa Mwenyekiti mpya utakinusuru na kurudisha nidhamu ya wabunge wa CCM? Hadi sasa dalili zote za kujaribu kumvuta mwenyekiti mpya zimeonekana. Kwamba kila mwanasiasa anajaribu kujiweka kwenye eneo la kuonesha umuhimu wake, huku macho na masikio yakielekezwa uchaguzi wa 2025. Kwa siasa za Tanzania uchaguzi mkuu wa 2025 si mbali, ni suala la kuanza mapema.

Aidha, kivuli cha Umagufuli kingalipo, wafuasi na wahanga wake hawajui hatima yao mbele ya Mwenyekiti mpya. Kutatua hilo ni lazima kuachana na kivuli hicho na kusonga mbele ama kukiendeleza ili kuzidisha minyukano zaidi, ikizingatiwa bado haifahamiki mtindo wa uongozi wa Samia Suluhu utakuwaje ndani ya chama.

Source link

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *