img

RC Zambi aagiza mwekezaji na viongozi wa serikali ya kijiji wakajisalimishe polisi

April 16, 2021

Na Ahmad Mmow, Nachingwea

Mkuu wa mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi amewataka viongozi wa serikali ya kijiji cha Mpiruka B na  mwekezaji katika mgodi wa madini wa Mpiruka wajisalimishe wenyewe katika kituo cha polisi cha Nachingwea. 

 Zambi alitoa agizo hilo jana katika kijiji cha Mpiruka B, wilaya ya Nachingwea alipozungumza na wananchi wa kijiji hicho kupitia mkutano wa hadhara. 

 Mkuu huyo wa mkoa alisema kutokana na utata uliojitokeza kuhusu ushuru wa kijiji hicho unaotokana na machimbo ya dhahabu katika mgodi wa Mpiruka kuna umuhimu wa viongozi wa serikali ya kijiji hicho na mwekezaji katika mgodi huo waende kituo cha polisi wakatoe maelezo. 

 Alisema kufuatia maelezo ya mkuu wa wilaya ya Nachingwea, Hashim Komba kuna kila sababu ya viongozi hao na mwekezaji huyo wakijisalimishe polisi ili watoe maelezo ya kwanini mwekezaji anashindwa kutimiza makubaliano na serikali ya kijiji hicho. 

 ” Mwekezaji anasema alikuwa anawapa fedha viongozi.

 Kwahiyo viongozi na mwekezaji kesho (leo) wakaripoti kwa OCD(kamanda wa polisi wa wilaya). Yeye atawapeleka TAKUKURU ( Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa) ili  wakahojiwe,” Zambi alisisitiza. 

 Alibainisha kwamba anaamini uchunguzi wa sitofahamu hiyo hautatumia muda mwingi. 

Kwani kinachohitajika ni uthibitisho kama mwekezaji aliwapa fedha viongozi, kiasi gani na lini. 

 Awali mkuu wa wilaya ya Nachingwea, Hashim Komba alimweleza mkuu huyo wa mkoa kwamba kijiji hakijanufaika na mgodi huo na hata wananchi hawajui mapato yanayotokana na mgodi huo ambao yanapatikana madini aina ya dhahabu. 

Komba alisema mwekezaji amekuwa mgumu kukamilisha malipo ya ushuru wa kijiji kwamadai kwamba kuna baadhi ya viongozi wa serikali ya kijiji walipewa fedha na mwekezaji huyo. 

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *