img

Othman: Nitashirikiana na Dk Mwinyi masheikh wa uamsho watendewe haki

April 16, 2021

 

Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Othman Masoud Othman amesema yupo tayari kushirikiana na Rais wa Zanzibar,  Dk Hussein Mwinyi kuhakikisha masheikh wa Uamsho  waliokamatwa na kushtakiwa kwa tuhuma za ugaidi wanatendewa haki.

Akizungumza leo Ijumaa Aprili 16, 2021 kwenye msikiti wa Maghfira uliopo mtaa wa Mchangani mjini Unguja, Zanzibar, Othman amesema anaendeleza juhudi zilizoanzishwa na mtangulizi wake, Hayati Maalim Seif Sharif Hamad aliyetaka suala hilo lipatiwe ufumbuzi.

“Wakati wa uhai wake Maalim Seif  alishirikiana vyema na Rais Mwinyi na walifanya juhudi kubwa kuhakikisha suala la masheikh wa Uamsho linapatiwa ufumbuzi na kwa kweli juhudi hizo zinaeleka kupata mafanikio.”

“Na mimi nitaendelea kuungana na Rais Mwinyi kulipatia ufumbuzi jambo hilo ambalo limekuwa likiwaumiza wananchi wengi wa Zanzibar mbali ya wao wenyewe na familia zao,” amesema.

Amebainisha kuwa sifa za waja wema ni kusema ukweli na kutenda haki, ikiwa ni pamoja na kutimiza dhamana wanazokabidhiwa.

“Kwangu ni amana na dhamana maana nafasi hii ya umakamu wa kwanza wa rais niliyonayo nimeachiwa na mtangulizi wangu, kwa hiyo nina dhamana kuhakikisha yale aliyoyaanza yeye katika kuwasaidia ndugu zetu hawa kupata haki yao,” amesisitiza.

Masheikh waliopo mahabusu ni Farid Hadi Ahmed, Jamal Swalehe, Nassoro Abdallah, Hassan Suleiman, Anthari Ahmed, Mohammed Yusuph, Abdallah Hassan, Hussein Ally na Juma Juma.

Wengine ni Saidi Ally, Hamisi Salum, Saidi Amour Salum, Abubakar Mngodo, Salum Ali Salum, Salum Amour Salum, Alawi Amir, Rashid Nyange, Amir Hamis Juma, Kassim Nassoro, Said Sharifu, Sheikh Mselem Ali Mselem na Abdallah Said Ali.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *