img

Serikali yataka Watanzania kumpuuza Profesa Assad

April 15, 2021

 

Katibu mkuu ofisi ya rais, menejimenti ya utumishi wa umma, Dk Laurean Ndumbaro amewataka Watanzania kumpuuza aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Profesa Mussa Assad kwa kutoa tuhuma kuwa maofisa na viongozi katika taasisi za umma wana uwezo mdogo wa utendaji.

Dk Ndumbaro ametoa wito huo kwa Watanzania leo Alhamisi Aprili 15, 2021 kupitia vyombo vya habari, akimponda Profesa Assad ambaye hivi karibuni  katika mdahalo uliofanyika Chuo Kikuu cha Kiislamu  Morogoro (MUM), alidai asilimia 60 ya watumishi na viongozi wa umma nchini hawana uwezo wa kutekeleza majukumu yao na asilimia 40 wana uwezo kidogo.

Akifafanua kuhusu uwezo wa utendaji walionao watumishi, Dk Ndumbaro amesema tuhuma alizozitoa Profesa  Assad zilijikita katika hisia na maoni yake binafsi kuliko uwezo wa kiakili na kitaaluma alionao na wala hakufanya tafiti.

Amesema  watumishi na viongozi wanatekeleza majukumu yao vizuri na ndio maana nchi imepata maendeleo makubwa katika sekta za elimu, miundombinu pamoja na afya na hatimaye Taifa limeingia katika uchumi wa kati.

Amefafanua kuwa watumishi watendaji na viongozi wa umma hupanda au kuteuliwa kuwa viongozi katika utumishi wa umma kwa mujibu wa miongozo ya utumishi wa umma ambayo pamoja na mambo mengine huzingatia sifa mbalimbali za weledi na vigezo vya majukumu wanayopaswa kuyatekeleza.

Ametoa mfano wa namna Serikali inavyohakikisha inakuwa na rasilimali watu yenye sifa stahiki kwa kuzingatia ipasavyo sera ya menejimenti na ajira katika utumishi wa umma kifungu namba  4.3 (ii) ambayo imebainisha kuwa, vigezo vya uteuzi katika utumishi wa umma vizingatie uwiano kati ya taaluma na ujuzi wa kazi pamoja na sifa nyingine kama uzoefu kazini, rekodi kazini na uwezo wa kujifunza.

Dk  Ndumbaro ameuthibitishia umma kuwa, watumishi wana uwezo kiutendaji kwani wanapoteuliwa kwa mara ya kwanza kushika nafasi za uongozi katika taasisi za Serikali, hupatiwa mafunzo elekezi ya utawala na uongozi ndani ya kipindi cha miezi mitatu hivyo kuondoa uwezekano wa kuwa na viongozi wasiokuwa na uwezo wa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *