img

Jeshi la polisi latumia nguvu kuwatawanya wafanyabiashara Unguja

April 15, 2021

Na Thabit Madai,Zanzibar

JESHI la Polis Mkoa wa Mjini Magharib Unguja limelazimika kutumia Mabomu ya Machozi kuwatawanya wafanyabiashara katika eneo la Michenzani, Darajani, Vikokotoni na mchangani baada ya kukaidi agizo la Serikali la kuhamia katika eneo la kibandamaiti.

Agizo hilo la Serikali  limekuja mara baada ya kukamilika kwa eneo la muda lilitengwa na Serikali kuu  kwa wafanyabiashara hao.

Mapema leo Asubuhi, wafanyabiashara hao walijikusanya katika ofisi kuu za Chama cha Mapinduzi CCM Kisiwandui Unguja huku wakiwa na mabango mbalimbali yaliyokuwa yakionensha kupinga agizo la Serikali kuhamia kibandamaiti na kuomba kuonana na Rais Dk Mwinyi kueleza kilio chao.

Wakizungumza na Mwandishi wetu kwa nyakati tofauti tofauti wafanyabiashara hao wameeleza kwamba, Serikali kupitia viongozi wa Manispaa hawakutumia njia sahihi ya kuwaondoa katika maeneo yao ya  biashara ukizingatia wapo katika mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani ambapo ndio kipindi cha biashara watu wengi.

Waliomba Serikali iwaachie wamalize mfungo wakiwa katika maeneo yao ya awali ya biashara baada ya hapo watahamia katika eneo la kibandamaiti.

 “Wamekuja kutuondosha hapa na kutuambia twende kibandamaiti sehemu ambayo ni mpya na ngumu kwa biashara ukizingatia watu wengi wamezoea kuja mjini kuchukua mahitaji yao,” alisema Khamis Nassor Ali Mfanyabiashara katika eneo la vikokotoni.

Khamis alieleza kuwa walipokwenda katika eneo la kibandamaiti Uongozi wa eneo hilo uliwaambiwa kuwa warudi sehemu zao za awali na watafuatwa kwa kuorodheshwa na kupatiwa maeneo.

“Ukiniuliza hapa sehemu yangu ipo wapi huko kibandamaiti siijui maana tumekwenda huko tumeambiwa turudi huki kisha Mkuu wa Mkoa atakuja kwa kuchukua majina yetu na kupewa maeneo huko kibanda maiti,” alieleza Khamis.

Nae Razia Ali Mfanyabiashara wa nguo eneo la Michenzani alisema kwamba, wao hawakukaidi agizo la Serikali kuhamia kibandamaiti ila hawakuwekewa utaratibu mzuri wa kupatiwa maeneo katika eneo hilo na kubaki katika maeneo yao ya awali.

Alisema Viongozi kupitia Jeshi la Polisi limeshindwa kuwaelewa na kutumia nguvu ya kuwahamisha.

“Sisi tunahitaiji kwenda kibandamaiti ila hatuna sehemu huko, hauwezi kuenda tu tukifukuzwa, kwa sasa tunamuhitaji Rais aje kututetea kama alipovyokuja wakati wa kampeni,” alisema.

Nae Juma fadhili alisema kitendo cha Jeshi la Polisi kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya hakikuwa cha kiungwana kutokana na Serikali kushindwa kuweka utaratibu mzuri wa wao kuhamia.

“Raia wa kawaida tunashikiwa bunduki tumekosea wapi, mwanzo tulipelekwa kijngwani kumetushinda na sasa wanatuambia twende kibandamaiti napo hatupawezi mitaji yetu itafilisika,”alisema Juma fadhili

“Huko kibandamaiti hilo eneo limetengenezwa kwa wafanyabiashara wa mbogamboga na vyakula, sisi tunaouza nguo inakuwa ni ngumu kwetu kulingana na hilo eneo lilivyo,” alieleza Juma fadhili mfanyabiashara wa nguo.

Akizungumza kwa njia ya Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharib Unguja, Idrissa Kitwana Mustapha alisema Serikali imechukua uwamuzi  huo kwa makusudi kutokana kuwa wapo katika utaratibu wa kusafisha mji

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ina nia safi kwa wafanya biashara wadogo wadogo Zanzibar na kuamua kuwaweka katika eneo maalum la kibandamaiti.

Mkuu huyo wa Mkoa alieleza kwamba, tayari utaratibu uliwekwa kwa wafanyabiashara hao kuhamia kibandamaiti na matangazo mbalimbali kupitia viongozi waliofika katika maeneo yao ya biashara.

“Ndugu yangu mwandishi Serikali ikifanya mambo yake haibahatishi, tulisema kwamba tuwaache wafanya biashara hao kwa muda kasha tukachukua hesabu katika eneo la kijangwani, Darajani na maeneo mengine ya waliokuwa wakifanya biashara kwa lengo la kuwakweka kibandamaiti,”alieleza Mkuu wa Mkoa Mjini Magharib.

Hata hivyo alisema kwamba katika maeneo ambayo wafanyabiashara hao wanahamishwa kupisha miradi mbalimbali ya maendeleo kwa faida ya wafanya biashara hao.

“Inabidi tuchukue maamuzi ambayo hatulazimiki kuyachukua,Serikali ina nia safi nao ndo maana tunawahmisha kupisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa faida yao wafanyabiashara,” alieleza.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *