img

RC Njombe asitisha vibali vya ujenzi maeneo ya karibu na uwanja wa Ndege

January 9, 2021

Na Amiri Kilagalila, Njombe

Halmashauri ya mji wa Njombe imeagizwa kusitisha utoaji wa vibali vya ujenzi wowote kwa wananchi maeneo ya karibu na uwanja wa Ndege ili kupisha utekelezaji wa mradi wa uwanja wa kisasa mkoani humo.

Agizo hilo lilitolewa na mkuu wa mkoa wa Njombe mhandisi Marwa Rubirya katika kikao cha bodi ya barabara ya mkoa kilichofanyika mjini Njombe

Amesema miradi inayotekelezwa na serikali inachukua muda kukamilisha maandalizi yake na Ilani ya Chama cha mapinduzi inaonyesha ni miongoni mwa viwanja ambavyo vipo kwenye mpango wa kujengwa upya na hata mwaka jana Rais Dkt, John Pombe Magufuli akifungua bunge alilizungumza hilo.

“Tukiruhusu wananchi kuendelea kujenga sisi wenyewe tutakuwa tunakwamisha utekelezaji wa mradi huu” Alisema Rubirya.

Ameelekeza halmashauri ya mji wa Njombe kusitisha utoaji wa vibali na kuhakikisha kuwa hakuna ujenzi unaoendelea kwenye eneo hilo.

Amesema mpaka sasa eneo pekee lililokubalika kujengwa uwanja wa ndege ni hapo ulipo na iwapo yatatokea maamuzi mbadala basi eneo hilo litabadilishwa matumizi na litatumika kwa shughuli zingine.

“Kwasababu hatujawa na mabadiliko ya matumizi ni bora tukazingatia maelekezo haya ambayo tuliyatoa kwenye kikao chetu ambayo naona yalikuwa maagizo halali kwa ajili ya maendeleo ya mkoa wetu” Alisema Rubirya.

Mkuu wa wilaya ya Njombe Ruth Masafiri amesema kumekuwa na maelezo ya muda mrefu kuwa uwanja huo utajengwa kwa kiwango cha lami ili ndege ziwe zinatua na kuruka uwanjani hapo lakini limekuwa kwenye mazungumzo tu.

Amesema matokeo yake majirani wanaendelea kukarabati nyumba na kuziongezea thamani ambapo kwa namna moja au nyingine suala hilo linaleta mgogoro huku mahitaji ya uwanja wa ndege katika mkoa huo hayazuiliki kwa kuwa kasi ya wananchi kujiletea maendeleo yao ni kubwa.

Alisema ndege inapotua Iringa robo tatu ya abiria wanaoshuka kwenye uwanja huo ni wananchi wa Njombe ambao baada ya hapo wanalazimika kupanda magari kuelekea mkoani Njombe.

“Kutokana na hilo naona tunahitaji sana kiwanja chetu kiliko kutegemea viwanja vingine” Alisema Ruth.

Awali mbunge wa jimbo la Njombe mjini Deo Mwanyika alitaka ufafanuzi juu ya zuio la ujenzi katika maeneo hayo ni kwa magorofa pekee au hata ujenzi wa kawaida.

Alisema kumekuwa na zuio kwa wananchi kusitisha ujenzi lakini kama mbunge zuio hilo lililenga aina gani za majengo kabla ya kupata ufafanuzi uliotolewa.

“Nataka nielewe kwasababu sijui stop order inazungumzia magorofa tu kwakuwa ndiyo naona yamesimama ujenzi lakini naona katika ujenzi wa kawaida maeneo mengine unaendelea” Alisema Mwanyika.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *