img

Kim Jong-un aahidi kuendeleza mpango wa silaha za nyuklia Korea Kaskazini

January 9, 2021

Dakika 6 zilizopita

North Korean leader Kim Jong-un speaks during the eighth congress of the Workers' Party in Pyongyang, North Korea

Maelezo ya picha,

Kiongozi wa Korea KaskazinKim Jong-un amesema sera za Marekani juu ya nchi yake “hazitawahi kubadilika”

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un amesema kuwa Marekani ndio “adui wake mkubwa” na kwamba hatarajii nchi hiyo kubadilisha sera yake kwa Pyongyang – haijalishi nani ndiye atakayekuwa rais.

Akizungumza katika kikao nadra sana cha chama chake tawala cha Workers’ Party, Bwana Kim pia ameahidi kupanua mpango wake wa silaha za nyuklia Korea Kaskazini na uwezo wa kijeshi wa nchi hiyo.

Alisema kuwa mipango ya utengenezaji nyambizi za nyukilia iko karibu kukamilika.

Matamshi yake yanawadia wakati ambapo Rais Mteule Joe Biden anajitayarisha kuingia madarakani.

Wachambuzi wanasema maneno ya Bwana Kim ni juhudi za kuongeza shinikizo kwa rais mteule wa Marekani ambaye ataapishwa Januari 20.

Bwana Kim alifurahia uhusiano mzuri kati yake na rais Donald Trump anayeondoka madarakani, hata ingawa ni hatua ndogo tu iliyopigwa katika majadiliano juu ya mpango wa nyuklia wa Korea Kaskazini.

Katika hotuba yake ya hivi karibuni kwa chama cha Workers’ Party – ambacho ni cha nane katika historia – Bwana Kim amesema Korea Kaskazini haina nia ya kutumia silaha zake za nyuklia pengine “pande hasimu” ziwe zinapanga kutumia silaha hizo dhidi ya Korea kaskazini kwanza.

Kim alisema Marekani ndio nchi ambayo ni “kikwazo kikubwa kwa mapinduzi yetu na adui yetu mkubwa… haijalishi ni nani atakayekuwa madarakani, uhalisia wa sera yake dhidi ya Korea Kaskazini hautabadilika,” Shirika la habari la KCNA linalomilikiwa na serikali limesema.

Hotuba yake iliorodhesha silaha ambazo ingependa kuwa nazo ikiwemo makombora ya masafa marefu yenye uwezo wa kurushwa kutoka ardhini au baharini na “makombora makubwa mno”.

Korea Kaskazini imefanikiwa kuendeleza mpango wake wa nyuklia kwa kiwango kikubwa tu hata ingawa imewekewa masharti makali.

Mapema wiki hii, Bwana Kim alikubali kuwa mpango wake kiuchumi wa miaka mitano kwa nchi hiyo iliyojitenga ulishindwa kufanikiwa katika “karibu kila sekta”.

Korea Kaskazini ilifunga mipaka yake Januari mwaka jana kuzuia kusambaa kwa ugonjwa wa virusi vya corona licha ya kwamba inadai haijawahi kupata maambukizi hayo.

Biashara na nchi jirani ambayo pia ni washirika wake China imepungua kwa karibu asilimia 80.

Vimbunga na mafuriko vimeharibu nyumba na mazao huko Korea Kaskazini ambayo imewekewa vikwazo chungu nzima vya kimataifa ikiwemo juu ya mpango wake wa nyuklia.

Source link

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *