img

Makanisa na Mashirika ya Kikristo Marekani yamuandikia barua kwa Joe Biden

January 8, 2021

Makanisa mbalimbali na Mashirika ya Kikristo nchini Marekani yameandika barua ya pamoja kwa Rais Mteule, Joe Biden kuhusu uvamizi wa Israeli na athari zake kwa Wapalestina wakimtaka atekeleze sera mpya na kusimama kidete kuunga mkono harakati za kuleta amani na haki katika ardhi takatifu ili jamii ya Kikristo iliyopo katika ardhi takatifu pamoja na wakazi wote waweze kuishi kwa amani na usalama. 

Miaka minne ya Rais wa Marekani anayemaliza muda wake, Donald Trump imeshuhudia mabadiliko makubwa katika sera mbalimbali za nchi ya Marekani hususani sera za Mashariki ya Kati ikiwa ni pamoja na kutoa msaada mkubwa kwa nchi ya Israeli kuendelea kuwakandamiza Wapalestina na kuwanyanganya ardhi yao kitendo ambacho ni kinyume na sheria za Kimataifa.

Kwa hivyobasi, makanisa yamemsihi Rais Mteule, Joe Biden kwanza, asisitize azma ya Marekani ya kuunga mokono juhudi za kuleta amani ya haki na ya kudumu kwa mzozo huu kati ya Wapalestina na Waisraeli na kubadili sera ya nchi katika Mashariki ya Kati.

Makanisa hayo na mashirika ya Kikristo pia yamemsihi Rais mteule, Joe Biden kuhakikisha kuwa pande zote mbili (Palestina na Israeli) zinaheshimiwa na kujumuishwa katika mazungumzo ya amani chini ya misingi ya sheria za kimataifa. Makanisa yamemuomba raisi Joe Biden kurudisha mahusiano na Wapalestina ambayo ni pamoja na kuruhusu kufunguliwa tena kwa ofisi za uwakilishi wa Mamlaka ya Palestina mjini Washington ambazo zilifungwa na Raisi Trump, na pia Marekani kufungua tena ofisi za uwakilishi mjini Jerusalem na kuhakikisha upatikanaji wa huduma za kibalozi kwa Wapalestina bila kizuizi, kama ilivyokuwa hapo awali. Walibaini kuwa, bila ushirikiano na Waplestina na Waisraeli kwa pamoja, hakuna mabadiliko ya maana yanayoweza kutokea.

Katika barua hiyo, Makanisa hayo pia yamemtaka Rais Mteule, Joe Biden kurudia msimamo wa Marekani kwamba makazi ni haramu chini ya Sheria ya Kimataifa na kuchukua hatua kuhakikisha kwamba Israeli inaadhibiwa kisiasa kwa ujenzi wowote wa Makazi katika ardhi ya Wapalestina. Utawala wa Raisi Donald Trump ulitangaza mnamo mwaka 2019 kwamba Marekani haizingati tena Makazi ya Israeli katika mji wa West Bank kama kinyume cha sheria za Kimataifa.

Kwa kuongezea, makanisa pia yamemuomba Rais Mteule, Joe Biden kurudisha msaada na ufadhili kwa Mamlaka ya Palestina, Shirika la Usaidizi na Kazi la Umoja wa Mataifa (UNRWA) pamoja na taasisi mbalimbali za Umoja wa Mataifa na za Haki za Binadamu zinazofanya kazi mjini West Bank na hata Gaza, hususani katika wakati huu mgumu ambapo ulimwengu unapambana na janga la ugonjwa wa Covid-19.

Makanisa pia yamemuomba Rais Mteule. Joe Biden kuhakikisha uwajibikaji kwa ukiukwaji wowote wa Haki za Binadamu unaofanywa na Israeli na kuhakikisha kuwa Ufadhili wa Marekani kwa Israeli hautumiwi kuendeleza kazi hiyo au kusaidia ukiukwaji wa Haki za Binadamu unaofanywa dhidi ya Wapalestina.

Israeli ni mpokeaji mkubwa wa misaada kutoka nchi ya Marekani, ikipokea takriban dola bilioni 3.8 za msaada wa kijeshi kila mwaka. Ufadhili huu uisaidia serikali ya Israeli kudumisha uvamizi wa maeneo ya Wapalestina na kuifanya Marekani ijumuike katika matendo ya Israel dhidi ya watoto wa Palestina katika magereza ya kijeshi na ubomoaji wa nyumba na jamii za Wapalestina.

Rais Mteule Joe Biden pia ameombwa arudie msimamo wa Marekani kwamba maeneo yote yaliyochukuliwa na Israeli baada ya vita ya mwaka 1967 ikiwemo Jerusalem ya Mashariki na Golan Heights hayatambuliki kama sehemu ya nchi ya Israeli kama ilivyo chini ya sheria za kimataifa.

Kwa kumalizia, makanisa hayo na mashirika ya Kikristo yalimsisitiza Raisi Mteule, Joe Biden kutekeleza mchakato wa amani kwa uaminifu na uwazi kwa pande zote mbili, yaani Palestina na Israeli ili kuleta amani yenye haki na yakudumu.

Miongoni mwa Makanisa na Mashirika ya Kikristo yaliyotia sahihi katika barua hiyo ni; Alliance of Baptists, American Friends Service Committee, Christian Church (Disciples of Christ), Christian Reformed Church in Northern America, Office of Social Justice, Church of the Brethren, Office of Peace Building and Policy, Church World Service, Churches of Middle East Peace, The Episcopal Church, the Evangelical Lutheran Church in America, the Friends Committee on National Legislation, Maryknoll Office for Global Concerns, Mennonite Central Committee US Washington Office, National Council of Churches of Christ in the USA, Presbyterian Church (USA), Reformed Church in America, United Church of Christ, and the United Methodist Church-General Board of Church and Society.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *