img

Ujerumani yarefusha hatua kali za kupambana na maambukizi ya corona

January 6, 2021

Ujerumani imerefusha muda wa hatua kali za kupambana na kusambaa kwa virusi vya corona hadi tarehe 31 Januari. Uamuzi huo umefikiwa baada ya mkutano kati ya Kansela Angela Merkel na viongozi wa majimbo ya shirikisho.

Akitangaza hatua hizo Jumanne usiku Kansela Angela Merkel amesema vikwazo vikali zaidi vitawekwa kuzuia watu kutangamana ili kudhibiti ongezeko la maambukizi.

Masharti yatakayotekelezwa nchini kote Ujerumani ni pamoja na kuendelea kuzifunga shule, hali kadhalika biashara na huduma zote zisizo za lazima hadi mwishoni mwa mwezi huu wa Januari. Masharti hayo ambayo yaliwekwa katikati mwa mwezi uliopita wa Desemba yalitarajiwa kumalizika tarehe 10 Januari.

Kansela Merkel amesema aina mpya ya virusi vilivyotoka nchini Uingereza, na msimu wa baridi vinaleta changamoto inayohitaji hatua kali za kukabiliana navyo.

”Nimesema mara kwa mara kwamba miezi ya msimu wa baridi, kama walivyotueleza wataalamu jana, ni wakati ambapo athari za janga hili zinaongezeka,” amesema Kansela Merkel, na kuongeza kuwa kuwepo ”kirusi kilichojibadilisha ambacho tayari kimeonekana nchini humu, inatulazimu kuchukua hatua kali za tahadhari.”

Tangu kuibuka kwa virusi vya corona, Ujerumani imekwishasajili visa milioni 1.8 vya maambukizi, na vifo 36,000 kutokana na virusi hivyo, hiyo ikiwa ni kwa mujibu wa takwimu za Chuo Kikuu cha Johns Hopkins.

Hatua mpya zilizotangazwa zinawataka wakazi katika katika maeneo yenye idadi kubwa ya maambukizi kutosafiri umbali wa zaidi ya km 15 kutoka nyumbani kwao bila sababu inayoeleweka.

Kila wilaya moja kati ya sita nchini Ujerumani inakidhi viwango vya kuwa eneo la maambukizi makubwa, ambayo kipimo chake ni maambukizi 200 kwa kila wakazi laki moja kwa muda wa juma moja.

Watu wa makundi maalumu yenye udhaifu ndio watapewa kipaumbele katika kupata dozi za kwanza za chanjo

Mikutano ya hadhara itaendelea kuzuiliwa, na kila familia itaruhusiwa kutembelewa na mtu mmoja tu kutoka nje.

Waajiri wamehimizwa kuwarahisishia watumishi wao kufanyia kazi nyumbani, na kuwapa likizo yenye malipo ya angalau siku kumi, wazazi wenye watoto wachanga ambao hawawezi kuwapeleka katika vituo vya kuwatunza wakiwa kazini.

Aidha, Bi Merkel amesema anaamini watu wa makundi yanayokabiliwa na hatari zaidi ndio wataweza kupata chanjo mnamo robo ya kwanza ya mwaka 2021, akiongeza kuwa dozi za kutosha kuwachanja watu wengine wengi yumkini zitapatikana mnamo robo ya pili ya mwaka huu.

Nchini Uingereza nako, serikali imesema masharti mapya ya kupambana na virusi vya corona huenda yakaendelea kuwepo hadi mwezi Machi, baada ya waziri mkuu Boris Johnson kusema usiku wa kuamkia leo kuwa moja kati ya wakaazi 50 wa Uingereza amepatwa na maambukizi ya corona.

Amesema matumaini ya kulishinda janga hilo yanawekwa katika operesheni ya chanjo, akiarifu kuwa tayari watu milioni 1.3 wamekwishapatiwa chanjo dhidi ya virusi hivyo hatari.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *