img

Uganda: Upinzani wazindua jukwaa la kufuatilia uchaguzi

January 6, 2021

Upinzani na mashirika ya kiraia wamekosoa utawala wa kulihusisha jeshi moja kwa moja katika mchakato wa uchaguzi. Wana mtazamo kuwa hatua hii itawatia hofu wananchi na kuhisi kuwa shughuli hiyo itagubikwa na vurugu. 

Jukwaa hilo lijulikanalo kama UID litahusisha matumizi ya teknolojia na nyenzo zingine kuhakikisha kuwa takwimu za matokeo ya uchaguzi kutoka sehemu mbalimbali za nchi yanahakikiwa iapsavyo.

Soma zaidi: Viongozi wa dini Uganda wataka uchaguzi uahirishwe

Hii ina maana kuwa wawakilishi wa vyama vyote vya kisiasa kwenye vituo watashirikiana katika kutoa taarifa kuhusu hali ilivyo kuanzia mwanzo hadi mwisho, hasa wakifuatilia vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu. Mwanasiasa mkongwe Paul Semwogerere aliyewahi kuwania kiti cha urais mwaka 1996 ndiye mratibu wa jukwaa hilo.

“Tumetambua masuala machache ya kimuundo na wapinzani wako tayari kuyashughulikia kwa pamoja ili waweze kurekebisha muundo wa kisiasa katika nchi hii.”

Daktari Kizza Besigye ambaye amewahi kugombea kiti cha urais mara nne na kushindwa na rais Museveni amekariri kwamba ijapokuwa upinzani ulishindwa kuungana kuwa na mgombea mmoja, muungano huu ni muhimu sana kuweza kukabiliana na jaribio lolote la wizi wa kura.

“Ikiwa unakwenda vitani lazima umhusishe kila mtu, si vyema kwenda vitani mkiwa mmegawanyika tarehe 14.”

Upinzani wakosoa utawala kwa kulihusiha jeshi katika zoezi la uchaguzi

Viongozi hao wa upinzani aidha wamekosoa hatua ya utawala kuwahusisha moja kwa moja wanajeshi katika zoezi la kiraia. Kulingana na taarifa za jeshi, askari 1,300 watashughulikia zoezi hilo na 6,000 kati yao wamekwisha pelekwa kushika doria katika mji mkuu, Kampala na vitongoji vyake. Semwogerere amesema: “Nikizungumzia jukumu la kijeshi katika siasa za Uganda ninakumbushwa kuhusu athari zake. Majeshi yafanye kazi yao ya kuhakikisha nchi haivamiwi kutoka nje.”

Mashirika yasio ya kiserikali yameunga mkono hatua hii ya upinzani. Yanaitaka tume ya uchaguzi kufafanua kuhusu teknolojia itakayotumiwa kupokea na kuhifadhi na kuwasilisha taarifa za matokeo.

Hadi sasa tume hiyo haijafafanua kuhusu mfumo gani wa teknolojia utakaotumiwa ili kuhakikisha uchaguzi huru na haki ambapo matokeo ya uchaguzi hayataweza kughushiwa. Sarah Birete ni mkurugenzi wa shirika la CCG.

“Rais ametamka mara mbili kwamba alifuta tume ya uchaguzi ya awali kutokana na masuala ya ufisadi katika zabuni ya teknolojia. Hatujui kama teknolojia mwafaka imepatikana.”

Kwa sasa, zoezi la wananchi kwenda kwenye vituo vya kuhakiki majina yao kwenye daftari la wapiga kura linaendelea. Idadi kubwa ya wanaojitokeza kufanya hivyo ni vijana. Kwa jumla idadi kubwa ya watu wameazimia kushiriki katika uchaguzi huu kuliko hapo awali.

 

 

 

 

Source link

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *