img

Uchaguzi wa Uganda 2021: Tawala za Kifalme zina nguvu gani katika siasa nchini

January 6, 2021

Dakika 5 zilizopita

Mfalme wa Rwenzururu Wesley Mumbere
Maelezo ya picha,

Mfalme wa Rwenzururu Wesley Mumbere

“Ukabila una nguvu na ni hatari kuliko chama cha kisiasa. Watu huchagua kumfuata na kumuunga mkono mtu fulani, si kwa kuwa ni kiongozi mzuri au mwaminifu, ila ni kwa sababu anatoka kabila moja na wao.”

Ni maneno ya mpiga muziki (DJ) na mwandishi wa kitabu cha “The Theory of 46 Be,” Kyos Magupe, kutoka Afrika Kusini.

Mauaji ya Kimbari yaliyotokea Rwanda 1994, ulikuwa ni mzozo mbaya wa kikabila kuwahi kutokea katika eneo la Afrika Mashariki tangu uhuru. Maelfu ya roho za watu ziliteketezwa kwa sababu tu ya asili yao. Mzozo huo ulikuwa kati ya Wahutu na Watutsi.

Katika baadhi ya nchi za Afrika Mashariki bado makabila yana ushawishi mkubwa wakati wa upigaji kura kwenye uchaguzi. Kenya ni mfano ulio hai. Licha ya kusifika kuwa na taasisi huru zinazosimamia chaguzi lakini bado hisia za ukabila hutawala katika majukwaa ya kisiasa.

Kwa pande mwingine hata hivyo, kuna mataifa ingawa ni machache, ambayo ukabila hauna nafasi. Tanzania ni mfano mmoja wapo. Licha ya kuwa na mapungufu makubwa katika demokrasia yake, mapungufu hayo hayahusiani na ukabila.

Ni juhudi kubwa za Rais wake wa kwanza Mwalimu Julius Nyerere kukemea ukabila zilizosaidia kuepukana na hilo. Mchango mwingine mkubwa ni lugha ya Kiswahili, licha ya kuwepo makabila mengi lugha hiyo inazungumzwa na kila kabila.

Hali ikoje nchini Uganda?

Ni taifa la Afrika Mashariki lenye wakaazi milioni 42.72 kwa mujibu wa ripoti ya Benki ya Dunia ya 2018. Likiwa na makabila takribani 54. Dini kuu ni Ukristo kwa zaidi ya asilima 80 ya wakaazi wote.

Mchambuzi wa maswala ya siasa kutoka Uganda, Ali Mutasa anazungumzia hali ya sasa katika muktadha wa makabila na siasa, pia nguvu za falme zilizopo na ushawishi wao katika siasa za nchi hiyo.

“Makabila yapo, kisheria yana ruhusiwa. Hisia za kikabila zinabaki mioyoni mwa watu, lakini hazina nguvu kisiasa. Makabila hujiendesha kwa mujibu wa tamaduni zao bila ya kuingilia mambo ya kitaifa. Taifa liko juu.”

Kwa upande wa Falme anasema, “Falme zinabaki kuwa na ushawishi kijamii. Atakachosema Mfalme fulani wafuasi wake watafuata, lakini zinapokuja siasa za kitaifa kila mmoja anakuwa na fikra zake na atajaza anavyotaka, hasa kwa kuwa uchaguzi ni siri ya mtu.”

Wakati alipokuwa madarakani Rais wa zamani wa Uganda, Milton Obote, alifanikiwa vyema kukandamiza siasa za kikabila. Lakini kiongozi huyo hakuweza kuvidhibiti vyombo vya usalama. Na hali hiyo ilidhihirika baada ya kupinduliwa 1971.

Rais Yoweri Kaguta Museveni anayetawala tangu 1986, ameyamudu mambo yote mawili. Vyombo vya usalama viko chini yake. Pia zile falme za kitamaduni haziko katika vuta nikuvute na serikali. Hali ya Uganda sio mbaya ikilinganishwa na baadhi ya nchi za Afrika Mashariki ambako bado makabila ni sehemu ya migogoro ya kisiasa.

Wakati Rais Museveni anaendesha vita vya msituni, wapiganaji wake walikuwa ni vijana kutoka makabila mbali mbali ya Uganda. Hili limesaidia pakubwa baada ya kuunda serikali, ule mshikamano wa wakati ule bado umeendelea kuwepo.

Pia kiongozi huyo alijenga maridhiano kati ya utawala wake na tawala za kifalme. Wakati wa utawala wake tawala hizo zilitambuliwa tena baada ya kupigwa marufuku na utawala wa Milton Obote.

Ni wakati gani falme zilikuwa na nguvu katika siasa?

“Ukitazama historia, baadhi ya hizi falme zilikuwa na ushawishi mkubwa wa kisiasa. Wakati Uganda inapigania uhuru, Buganda kwa mfano ilikuwa mpinzani mkubwa wa ukoloni wa Uingereza. Na kabila la Acholi lilitumika sana katika jeshi,” anaeleza Ali Mutasa.

Historia ya Afrika inaonesha Falme za kikabila zilifanya kazi kubwa ya kuendesha mapambano dhidi ya Ukoloni. Baada ya Uganda kupata uhuru kutoka kwa Uingereza 1962. Ufalme wa Buganda uliunda chama cha kisiasa cha Kabaka Yeka (KY).

Chama cha Uganda People’s Congress (UPC) chake Milton Obote kilishirikiana na Kabaka Yeka na kuunda serikali ya mseto baada ya uchaguzi wa 1962. Obote akawa Waziri Mkuu mtendaji wa taifa hilo, na Edward Mutesa, Mfalme wa Buganda na kiongozi wa Kabaka Yeka akawa Rais.

Ndoa ya kisiasa kati ya UPC na KY haikuwa ya masikilizano. 1966 hadithi ya ndoa hiyo iliishia kwa Obote kujitangaza Rais, kushambulia kasri la Kabaka na Mfalme wa kabila hilo akakimbilia uhamishoni Uingereza. Hatimaye katiba mpya ikapiga marufuku Falme zote za kijadi nchini Uganda.

Obote alichagua kuwa hasimu wa Falme za Uganda. Uwepo wa chama cha Kabaka Yeka ulidhihirisha nguvu ya Ufalme na kabila hilo katika siasa na serikali ya wakati huo. Mivutano ya Obote na KY ilichangia pakubwa kuzifanya siasa za kikabila kutamalaki.

Siasa za sasa

Kuelekea uchaguzi mkuu mwezi huu, kampeni zimefanyika. La kuvutia, wagombea hawakuendesha kampeni wakinadi makabila yao au kushambulia makabila mengine. Mivutano mikubwa iliyotokea inatokana na vyombo vya usalama na vyama vya upinzani.

Tatizo la Uganda ya sasa halipo katika makabila ya raia wake, bali demokrasia ya taifa hilo ndiyo yenye mashaka. Hakuna uhuru wa kutosha wa kuendesha siasa kwa vyama vya upinzani kama kinavyopata chama tawala.

Uchaguzi utafanya wakati huku nyuma wafuasi kadhaa wa upinzani tayari wamesha uwawa na wengine kutiwa nguvuni. Kampeni za wagombea wa upinzani zimetatizwa mara kadhaa na vyombo vya usalama, huku wengine wakikamatwa.

Museveni kafanikiwa kwa kiasia kikubwa kuiweka nchi hiyo katika amani dhidi ya machafuko na mizozo ya kikabila. Upande mwingine wa shilingi uhuru wa kisiasa na demokrasia ya kuchagua bado iko kizani.

Source link

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *