img

Mbunge Mchafu awahimiza wananchi mkoani Pwani kujikinga na magonjwa ya mlipuko

January 6, 2021

 

NA VICTOR MASANGU, PWANI

JAMII imetakiwa kuhakikisha kwamba inajenga tabia ya kunawa mikono mara kwa mara kwa ajili ya kuepukana na magonjwa mbali mbali ya milipuko ikiwemo kuumwa na tumbo na badala yake wazingatie maelekezo ambayo yanatolewa na wataalamu wa afya ili kuupukana na  hali hiyo.

Kauli hiyo imetolewa na Mbunge wa viti maalumu Mkoa wa Pwani Hawa Mchafu wakati alikuwa akizungumza na baadhi ya wananchi kuhusiana na masuala mbali mbali ya kimaendeleo pamoja na kujadili namna ya kuweza kukabiliana na magonjwa ya mlipuko amabyo yamekuwa yakiwakumba baaadhi ya wananchi.

Mchafu alisema kwamba kwa sasa nia ya serikali ya awamu ya tano ni kuboresha huduma ya afya katika maeneo mbali mbali ikiwemo Zahanati, vituo vya afya pamoja na hospitali ili kuweza kuwapatia huduma iliyo bora  kwa wananchi sambamba na kuhakikisha kwamba wanahudumiwa bila ya kupata usumbufu wowote.

“Kikubwa ninachowaomba wananchi pamoja na jamii kwa ujumla ni lazima tubadilike kwa kuhakikisha kwamba tunakuwa na utaratibu wa kunawa mikono yetu katika vipindi tofauti na tukifanya hivi nina imani kubwa tutaweza kabisa kuepukana na magonjwa mabali mbali ya milipuko ambayo imekuwa ikijitokeza katika maeneo ambayo tunaishi hivyo ni vema tukazingatia mwongozo unaokuwa ukitolewa na wataalamu wetu wa afya,”alisema Hawa.

Kadhalika aliongeza kuwa ni lazima pia wananchi wawe na utaratibu wa kusafisha maeneo yao mbali mbali amabyo wanaishi pamoja na kufyeka nyasi na kufikia madimbwi ya maji ambayo ndio yamekuwa ni chanzo kikubwa na kusababisha kutokea kwa magonjwa mbali mbali ya milipuko ikiwemo ugonjwa wa kipindupindu.

Aidha Mbunge huyo aliahidi kuendelea kushirikiana na wananchi pamoja na wataalamu wa afya katika kuweka mipango madhubuti ya kutoa elimu ya mara kwa mara hasa katika maeneo ya vijijini ili kuweza kutoa elimu ambayoitaweza kuwa ni moja ya msaada na mkombozi mkubwa wa kuwasaidia wananchi kujikinga na magonjwa ya mlipuko.

Nao baadhi ya wananchi Wilayani Kibaha wamempongeza Mbunge huyo kwa kuweza kuwatembelea katika maneo yao na kuwapa elimu inayohusiana na magonjwa ya mlipuko na kwamba maelekezo hayo watayafanyia kazi ili kuweza kuondokana kabisa na hali hiyo ya kuumwa magonjwa  hayo na kwamba wameiomba serikali ya awamu ya tano kuwaboreshea huduma zaidi ya matibabu katika maeneo ya vijijini.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *