img

Kinyang’anyiro kikali cha kumchagua Seneta chaendelea Georgia kati ya Republicans na Democrats

January 6, 2021

Kinyang’anyiro katika jimbo la Georgia kinachotarajiwa kuamua nani atakuwa na udhibiti wa bunge la Seneti kinaendelea kuwa na ushindani mkali huku vituo vya kupiga kura vikiwa vimefungwa.

Kituo cha habari cha CBS News mshirika wa BBC kimesema vyama vyote viwili vinakaribiana mno. Matokeo yanatarajiwa kuanza kutangazwa saa kadhaa tokea sasa lakini ikiwa matokeo yataendelea kuonesha ukaribu wa namna hiyo huenda matokeo ya mwisho yakachukua muda kutangazwa.

Rais mteuliwa Joe Biden wa chama cha Democrats anahitaji kushinda uchaguzi huu ili aweze kupata udhibiti wa mabunge yote mawili.

Wakati huohuo, rais wa chama cha Republican anayeondoka madarakani Donald Trump anahitaji kushinda kiti kimoja tu ili adhibiti bunge hilo la Seneti.

Wabunge wa Republican Kelly Loeffler na David Perdue sasa hivi ndio wanaoshikilia viti hivyo viwili. Bi. Loeffler anakabiliana na Reverend Raphael Warnock huku Bwana Perdue akipambana na aliyekuwa mwanahabari Jon Ossoff.

Hakuna kati ya wagombea hao ambaye alipata asilimia 50 ya kura zilizopigwa kama inavyohitajika kuibuka na ushindi wa moja kwa moja katika uchaguzi uliofanyika Novemba hatua iliyolazimisha kufanyika kwa duru ya pili kulingana na sheria za uchaguzi za jimbo la Georgia

Sasa hivi chama cha Republican kinashikilia viti 52 kati ya 100. Na ikiwa Democrats watapata ushindi, bunge la Senati litakuwa limegawanyika nusu kwa nusu hatua itakayomuwezesha makamu rais wa chama cha Democratic Kamala Harris kufanya maamuzi ya upigaji wa kura.

Hili litakuwa muhimu katika upitishaji wa ajenda za Joe Biden bungeni ikiwemo masuala ya msingi kama vile afya na udhibiti wa mazingira – sera ambazo zinapingwa vikali na Republicans.

Bunge la Seneti pia lina nguvu ya kuidhinisha au kukataa baraza la mawaziri lililochaguliwa na Bwana Biden pamoja na nyadhifa za majaji.

Ikiwa Bwana Ossoff na Warnock watashinda, Ikulu ya Marekani, bunge la Seneti na bunge la Wawakilishi yote yatakuwa chini ya udhibiti wa chama cha Democratic kwa mara ya kwanza tangu kuchaguliwa kwa rais Barack Obama mwaka 2008.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *