img

Mazungumzo ya Trump ya siri Georgia kujaribu kubadilisha uchaguzi yanaswa

January 4, 2021

Rais wa Marekani Donald Trump amerekodiwa akimwambia afisa mkuu wa uchaguzi Georgia atafute kura za kutosha kuwezesha kubadilishwa kwa matokeo ya uchaguzi.

“Nataka tu kupata kura 11,780,” Bwana Trump alimwambia katibu wa chama cha Republican Brad Raffensperger jimboni humo katika mazungumzo yaliyorekodiwa na kutolewa na gazeti la Washington Post.

Bwana Raffensperger anasikika akijibu kuwa matokeo ya uchaguzi ya Georgia yalikuwa sawa.

Joe Biden alishinda uchaguzi wa Georgia pamoja na majimbo mengine muhimu na kumuwezesha kupata kura 306 za wajumbe dhidi ya Bwana Trump aliyepata kura 232.

Tangu uchaguzi uliofanywa Novemba 3, Bwana Trump amekuwa akidai kuwa kura ziliibwa bila kutoa ushahidi wowote unaothibitisha madai yake.

Majimbo yote 50 yamethibitisha matokeo ya uchaguzi huo baadhi ya vituo ikiwa ni baada ya kura kuhesabiwa tena au pia kwasababu ya kesi zilizowasilishwa mahakamani kupinga matokeo.

Hadi kufikia sasa, Marekani imetupilia mbali kesi 60 zilizokuwa zimewasilishwa kupinga ushindi wa Bwana Biden.

Aidha bunge linatarajiwa kuidhinisha rasmi matokeo ya uchaguzi huo Januari 6.

Bwana Biden wa chama cha Democrat, anatarajiwa kuapishwa kama rais wa Marekani Januari 20.

Pia, wapiga kura huko Georgia wanatarajiwa kupiga tena kura Jumanne kuchagua maseneta wawili wa jimbo hilo na matokeo ya uchaguzi huo huenda yakaweka sawa jinsi nguvu ya uongozi itakavyokuwa katika bunge la Seneti.

Ikiwa washindani wawili wa chama cha Democrat watashinda, kunamaanisha kwamba kutakuwa na idadi sawa ya wabunge wa vyama vya Republican na Democratic na makamu mteule wa chama cha Democratic Kamala Harris ndiye atakayekuwa na usemi katika kura ya kufanya maamuzi.

Bwana Biden wa chama cha Democrat tayari anadhibiti bunge la wawakilishi.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *