img

Wauza Mananasi Kiwangwa walilia soko la kuuzia zao hilo

December 15, 2020

 

Na Omary Mngindo, Kiwangwa Des 15

WAKAZI wa Kijiji cha Kiwangwa, Kata ya Kiwangwa wanaojihusisha na kilimo cha Mananasi, wanauomba uongozi wa Halmashauri ya Chalinze Bagamoyo Mkoa wa Pwani, kuwajengea soko la kuuzia zao hilo.

Aidha wamelalamikia ubovu wa miundombinu ya barabara inayotokea mashamani, hali inayosababisha wenye magari wakati mwingine kugoma kwenda au kuwatoza nauli kibwa wakihofia kuharibika kwa magari yao.

Wakizungumza kwa niaba ya wenzao, Athumani Wema, Hungiro Rajabu, Hidaya Mnazi, Bernard Barnard, Kimungu Boi dalali akiwemo dereva Octavian Benard, walisema kuwa zao la Namasi lina soko kubwa lakini kutokuwepo na eneo maalumu la kuuzia imekuwa tatizo.

Wema alisema kuwa pamoja na wakazi wa Kiwangwa kujikita katika kilimo hicho, lakini hawana eneo la kuuzia bidhaa zao hivyo kulazimika kukaa kandokando ya barabara ya Bagamoyo Msata, ambalo ni eneo la akiba la Wakala wa Barabara nchini TANROAD’S.

“Zao la nanasi likivunwa likinyeshewa mvua tu linaharibika, kukosekana kwa soko kunachangia wakulima na wafanyabiashara kupata hasara kubwa, kama mnavyotuona hapa ndio soko letu la kuuzia nanasi, wateja wetu ni abiria wanaopota katika mabasi,” alisema Wema.

Hungiro Rajabu alisema kuwa mwaka huu wamepata hasara kubwa kutokana na mvua, huku akisema kuwa ametumia gharama kubwa ya mbolea na palizi lakini kutokana na mvua mwanzoni aliuza kwa bei ya hasara, huku mengine yakiharibima mashambani.

Dalali wa zao hilo Kamungu alisema kuwa nanasi linapelekwa sana nje ya nchi, sanjali na mikoa mbalimbali hapa nchini ikiwemo jijini Dar es Salaam, lakini wakulima na wafanyabiashara hawana soko la kuuzia.

Diwani wa Kata hiyo Malota Kwaga alikili kuwepo kwa changamoto hiyo, huku akieleza kwamba kukosekana kwa soko la kuuzia zao hilo imekuwa changamoto kubwa kwa wakazi hao, huku akizungumzia viwanda vya matunda kutopokea nanasi wakidai haikawii kuharibuka.

“Wamiliki wa viwanda hawapokei nanasi wakidai kwamba haikawii kuharibika, jambo ambalo ni kinyume na matarajio yaliyokuwepo awali ya kwamba uwepo wa viwanda vingekuwa wakombozi kwa wakulima wa mazao ya matunda ikiwemo nanasi,” alisema Kwaga.

Akizungumzia miundonbinu ya barabara, Kwaga alisema kuwa Halmashauri inaendelea na uboreshaji wa miundombinu hiyo, huku akiigusia barabara ya Kiwangwa kuelekea shule ya Sekondari na kwamba changamoto zingine zinaendelea kupatiwa ufumbuzi.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *