img

RC Njombe awa mbogo kukwama ujenzi wa chuo cha ufundi VETA

December 15, 2020

Na Amiri Kilagalila, Njombe.
Mkuu wa mkoa wa Njombe mhandisi Marwa Rubirya amemuagiza mkurugenzi wa VETA nyanda za juu kusini kuandaa taarifa itakayoonyesha lini ujenzi wa chuo cha VETA utaanza baada ya ujenzi wa chuo hicho kusimama kwa muda mrefu.
Agizo hilo amelitoa baada ya kufanya ziara katika eneo la ujenzi wa chuo hicho cha VETA lililopo kijiji cha Shaurimoyo kata ya Lugalawa wilayani Ludewa .
Amesema kufikia mwisho wa mwezi huu anahitaji kupatiwa taarifa ambayo itaonyesha hatua ambazo wamepanga kuanza nazo katika ujenzi wa chuo hicho cha VETA.
Amesema chuo hicho kinajengwa kimkakati na siyo kwa bahati mbaya kwa kuwa kinahitajika sana na wakazi wa mkoa wa Njombe na siyo Ludewa peke yake. 
“Nilikuwa nawaambia kwenye baraza huwezi kuzungumzia Njombe bila ya Liganga na Mchuchuma hivyo chuo hiki hakikuamriwa kijengwe hapa kwa bahati mbaya bali kinajengwa kimkakati” Alisema Rubirya.
 
Aliwahakikishia wakazi wa kijiji hicho kuwa mahitaji ya chuo hicho bado yapo pale pale hivyo lazima kitajengwa eneo hilo na wala hakitohama kwa kuwa wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne kijijini hapo waweze kupata mafunzo ili migodi itakapokamilika miongoni mwao waweze kupata kazi.
Aidha alimuahidi mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga  kumpatia nakala ya taarifa hiyo ili kwa pamoja waweze kusaidiana kwa pamoja ili kuhakikisha kuwa mradi huo unaendelea na utekelezaji wake.
Awali akitoa maelezo ya mwenendo wa ujenzi wa chuo hicho mwakilishi wa mkurugenzi wa VETA mhandisi Benitho Kigava alisema mradi huo wa ujenzi wa  chuo hicho ulianza januari 2017 na ulipaswa kukamilika ndani ya miezi nane pekee.
Alisema mradi huo ulikuwa ukijumuisha majengo ya karakana, madarasa, ofisi za utawala, mabweni, nyumba za watumishi, vyoo na miundo mbinu ya nje ikiwemo barabara.
Alisema katika mradi huo kiasi cha gharama ambacho kilipaswa kutumika katika chuo hicho cha VETA mpaka kukamilika kwake ni zaidi ya shilingi bilioni 9. 
Alisema mkandarasi alikabidhiwa mradi huo mwezi disemba mwaka 2016 na kuanza kazi rasmi na kuanza kazi januari 2017 hivyo alipaswa kumaliza mradi huo kwa muda wa miezi nane huku ukitarajia kukamilika ukiwa umejengwa kwa ghalama ya zaidi ya bilioni tisa kwa wakati huo.
“Nachoweza kusema mradi ambaye hakuutendea haki ni wa kwanza kabisa ni mshauri wa mkandarasi kwani ndiye aliyeshauri ili majengo yajengo.inabidi kuchimbwa ili kutafuta usawa kitu ambacho kilipoteza muda mwingi” Alisema Benitho. 

Nae mbunge wa jimbo hilo la Ludewa Joseph Kamonga alisema akiwa afisa ardhi wa wilaya ya Ludewa alishiriki katika kuandaa hati ya eneo hilo ambalo lilitolewa na wananchi kwa ajili ya ujenzi wa chuo hicho.

Alisema wananchi walitambua umuhimu wa kujengwa kwa chuo hicho lakini cha kushangaza jambo hilo limechukua muda mrefu zaidi ya miaka kumi.
“Baadhi ya wananchi walimueleza mkuu wa mkoa kwamba kama chuo hiki hakipo tena basi turudishiwe mashamba yetu ili tuendelee kuyalima” Alisema Kamonga.
Nao baadhi ya wakazi wa kijiji hicho cha Shauri moyo akiwemo Nicholaus Kayombo na Agnes Mtweve walisema wanakitegemea sana chuo hicho lakini cha kushangaza hakuna utekelezaji wowote unaoendelea. 
” Tunaiomba serikali ifanye hiyo michakato ili tuweze kunufaika sababu tulitegemea kupitia chuo hiki tutanufaika kwanza kwa kusoma watoto wetu, pili kupitia hao wanafunzi tutakuwa tunafanya biashara ndogo ndogo” Alisema Kayombo.

 

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *