img

TAKUKURU Manyara yaokoa Mamilioni ya Fedha za Mstaafu

December 14, 2020

Na John Walter-Manyara.

Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa  wilayani Kiteto Mkoani Manyara, imeokoa shilingi milioni 6.6 za Bakari Omary Lugage mstaafu alizokuwa ameporwa na moja ya taasisi ya fedha.

Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Manyara Holle Makungu  alisema taasisi nyingi zinafanya kazi bila sheria na kanuni zinazoongoza utendaji wao wa kazi hali inayofanya wamiliki kujiamulia bila kujali madhara kwa wananchi.

Makungu alisema Serikali kupitia Bunge kwa kuona udhaifu huo lilitunga sheria ya huduma ndogo ya fedha ya mwaka 2018 na kufuatiwa na kanuni zake zilizotangazwa kwenye gazeti la Serikali  Na. 679 la tarehe 13.09.2020.

Aidha Mkuu huyo wa Takukuru Mkoa alisema udhaifu huo umefanya mzee mstaafu Bakari Omary Lugage aliyekuwa amekopa mil 1.4 mwaka 2018 kwa moja ya kampuni Kiteto kulipa mil 8.

Alisema Takukuru ilibaini mzee huyo mstaafu kipindi cha mwishoni mwa mwaka 2018 alianza kukopa fedha kati ya 50,000 hadi 100,000  kwa nyakati tofauti huku dhamana yake ikiwa ni kadi ya Benki (ATM).

Baada ya kiinua mgogo chake kuingia kampuni hiyo ya kifedha iliyopo Kiteto ilichukua kiasi cha mil 8 kwenye akaunti yake na alipofuatilia kwa muda mrefu hakufanikiwa ndipo akafika kuomba msaada Takukuru.

Akimkabidhi fedha hizo kiasi cha tsh mil 6.6, Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Kanali Patrick Songea aliwaasa wananchi kuwa makini na taasisi za kifedha na kuwataka kusoma na kuielewa mikataba kabla.

“Wananchi kuweni makini katika mikataba kwa makampuni haya kwani ni wengi wanalalamika na wakati mwingine ni kutoona umuhimu wa kuwa na mikataba jambo ambalo ni la msingi” alisema Kanali Songea

Kwa upande wake Bakari Omary Lugage baada ya kukabidhiwa fedha zake alishukuru Taasisi hiyo kuwa imekuwa msaada mkubwa kwani pamoja na kufuatilia kwa muda aligonga mwamba.

“Hata mipango yangu ilikufa sikuwa na la kufanya maana hela zangu zilishapotea ila sasa itabidi nijipange tena upya kuanzisha mipango yangu ya maendeleo”alisema Lugage

 

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *