img

Madiwani mji wa Masasi wamchagua Meya mpya

December 14, 2020

Na Hamisi Nasri,Masasi 

  BARAZA la Madiwani la halmashauri ya mji Masasi mkoani Mtwara limewapigia kura za kishindo diwani wa kata ya Jida (CCM) Hashimu Namtumba kuwa meya wa mji wa Masasi huku Naibu wake akiwa diwani wa kata ya Mkomaindo,Ally Salvatory 

  Uchaguzi huo ulifanyika jana mjini Masasi mara baada ya madiwani 19 kula kiapo kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa majukumu yao, uchaguzi huo ulifanyika katika ukumbi wa chuo wa uuguzi na ukunga wilayani Masasi. 

  Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo,mwenyekiti wa uchaguzi huo ambaye pia ni Katibu Tawala wa wilaya ya Masasi, Mohamed Azizi  

  Alisema nafasi ya mstahiki meya (mwenyekiti) mgombea alikuwa mmoja, Hashimu Namtumba huku wajumbe waliopiga kura walikuwa 19 na kura halali zilizopigwa zilikuwa 19 na hakuna kura zilizoharibika.

  “Kwa mujibu wa kanuni na sheria za uchaguzi namtangaza rasmi, Hashimu Namtumba kuwa meya mpya wa halmashauri ya mji Masasi,”alisema Azizi 

  Aidha,Azizi alisema nafasi ya naibu meya(makamu) kuwa kura zilizopigwa zilikuwa 19 kura halali zilizopigwa ni 19 na hakuna kura zilizoharibika.

  Alisema kupitia kura hizo alimtangaza diwani wa kata ya Mkomaindo,Salvatory kuwa ndiye naibu meya wa mji wa Masasi katika halmashauri hiyo ya mji Masasi na kueleza kuwa washindi hao wanapaswa kuanza kazi mara moja kwa lengo la kuleta maendeleo.

  Azizi alisema jukumu la kwanza wahakikishe wanakuwa na mpango mkakati wa kuuweka mji wa Masasi katika kasi ya maendeleo kwa wananchi wake ikiwa ni pamoja na kutekeleza kikamilifu ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020

   Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, meya huyo,Namtumba alisema atasimamia halmashauri hiyo kwa umakini mkubwa kwa kushirikiana na madiwani wenzake pamoja na mbunge wa Masasi mjini ambaye pia ni waziri wa viwanda na biashara, Geofrey Mwambe kwa lengo kuu moja la kuifanya Masasi kuwa katika mwonekano wa kisasa na yenye hadhi bora.

  Naye naibu meya,ameahidi kufanya kazi kwa karibu na baraza la madiwani na watendaji wa halamshauri ili kuhakikisha maendeleo chanya katika mji wa Masasi yanapatikana kwa kasi katika kipindi cha miaka watakachokuwa madarakani kuiongoza halmashauri hiyo.

  Akizungumza wakati wa kuwaapisha madiwani wa halmashauri hiyo kutoka jimbo la Masasi mjini, Mbunge wa jimbo hilo, ambaye pia ni waziri wa viwanda na biashara, Mwambe aliwataka madiwani hao kushikamana pamoja na kuleta maendeleo kwa wananchi.

  Alisema wanapaswa kutoingiza mawazo binafsi kwenye mambo ya msingi jambo pekee wanalotakiwa kulifanya ni kuwabana watendaji wa halmashauri ili miradi ya maendeleo inayotekelezwa ambayo inatumia fedha nyingi za serikali inatekelezwa kikamilifu na kuwa na tija kwa jamii.

  Mkuu wa wilaya ya Masasi,Selemani Mzee alisema madiwani hao nyenzo kwa wananchi hivyo waende kutekeleza makujumu yao kwa kuangalia maslahi ya wananchi wao waliowachagua ili kutatua kero zao.

                                            

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *