img

DC Ndemanga ‘ awakalia kooni’ madiwani wa halmashauri ya manispaa ya Lindi

December 14, 2020

Na Ahmad Mmow, Lindi.

Mkuu wa wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga amewatahadharisha madiwani wa halmashauri ya manispaa ya Lindi wanaodhani udiwani ni ajira wajue kwamba wadhifa huo siyo ajira bali ni uongozi wa umma.

Ndemanga alitoa angalizo hilo wakati wa kikao cha kwanza cha baraza la madiwani la halmashauri hiyo lililo keti hivi karibuni katika ukumbi wa mikutano wa kanisa katoliki la Mtakatifu Andrea Kagwa lililopo manispaa ya Lindi.

Kwakuzingatia ukweli huo Ndemanga aliwataka wenye fikra hizo wajue kwamba udiwani ni wadhifa ambao hauwazuii kufanya shughuli za kiuchumi, kwani hata wenye ajira wanafanya kazi za ziada zinazo waingizia vipato.Kwahiyo  wafanye kazi halali zikiuchumi zitakazo waingizia vipato.

Alisema ni aibu kuona diwani ambaye anawahimiza wananchi anaowaongoza wafanye kazi ili wajiletee maendeleo lakini mwenyewe hafanyi kazi. Akiweka wazi kwamba diwani aina hatoshi kuwa kiongozi wa umma.

Katika hali ambayo ilionesha mkuu wa wilaya huyo aliamua kutoa ya moyoni kwa madiwani hao alisema licha ya baadhi ya madiwani kudhani kwamba wadhifa huo ni ajira lakini wapo wengine wanashindwa kutekeleza kikamilifu wajibu wao. Badala yake wanakwepa.

Alisema ipo migogoro ya kijamii inayotokea kwenye kata zao, ambayo wanauwezo wa kumaliza. Hata hivyo wanashindwa kufanya hivyo. Tena wengine wanadiriki kuwapa nauli wananchi ili waende kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya.

” Yaani unajiuliza, hupati jibu. Migogoro mingine ingeweza kumalizwa na mheshimiwa diwani lakini inaletwa kwenye Ofisi ya mkuu wa wilaya na baadhi ya migogoro inachangiwa na baadhi ya madiwani, ” Ndemanga alisema.

Mbali na hayo,  Ndemanga aliwataka madiwani hao wafuatilie na kusimamia kikamilifu miradi inayotekelezwa katika kata zao badala ya kuwalaumu wataalamu inapotekelezwa chini ya kiwango.

Alisema ni aibu kusikia diwani analalamika miradi kutekelezwa chini ya kiwango au kuharibika wakati muda wa utekelezaji wa mradi huo alikuwepo na alikuwa yanayofanyika tangu mwanzo hadi mwisho wa utekelezaji.

” Lakini pia naomba mshirikiane vema na watumishi wa halmashauri. Acheni kufikiria kuwaazimia  bali wapeni ushirikiano kwa maslahi ya halmashauri na wananchi na mkatatue kero za wananchi,”  Ndemanga alionya na kutoa darasa.

Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Lindi, Hamida Abdallah alitahadharisha kwamba tofauti za mila na desturi baina ya wananchi wa majimbo ya Lindi na Mchinga zisiwe kikwazo cha maendeleo ya halmashauri hiyo. Bali washirikiane kwa moyo mmoja ili kusukuma mbele halmashauri ya manispaa ya Lindi kimaendeleo.

Alisema kunaweza kuwepo tofauti za mila na desturi baina ya wananchi wa majimbo hayo. Hata hivyo isiwe sababu ya kukwamisha utekelezaji wa mipango ya maendeleo.

Mheshimiwa Hamida aliweka wazi kwamba jimbo la Mchinga kuingizwa katika halmashauri ya manispaa ni jambo lenye tija kwa wananchi wa majimbo hayo. Kwani kiwango cha mapato ya halmashauri hiyo yataongezeka iwapo madiwani wote watashirikiana bila kubaguana.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *