img

Mgogoro wa DRC na athari zake kwa nchi za maziwa makuu?

December 13, 2020

Dakika 4 zilizopita

DRC ndiyo taifa lenye eneo kubwa kupita yote katika bara la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Akiandika katika kitabu chake mashuhuri cha The Open Veins of Latin America, mwandishi Eduardo Galeano, alisema; “tatizo kubwa kuliko yote la Amerika Kusini ni kwamba eneo hilo ni tajiri sana”. Mwandishi huyo angeweza kuhamishia sentensi hiyo kwa taifa la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Mgogoro wowote wa kisiasa unapoibuka kutoka katika taifa hilo, tatizo hilo huwa kubwa kwa sababu ya utajiri wake na pia sababu ya ukubwa wake.

DRC ndiyo taifa lenye eneo kubwa kupita yote katika bara la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara. Kwa eneo, ni nchi ya pili kwa ukubwa katika bara zima la Afrika, ikizidiwa na Algeria pekee.

Katika mipaka yake, DRC inazungukwa na mataifa tisa tofauti ambayo ni; Sudan Kusini, Uganda, Tanzania, Jamhuri ya Congo, Rwanda, Burundi, Angola, Zambia na Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Wakati Rais Etienne Tshisekedi na mtangulizi wake katika nafasi hiyo, Joseph Kabila, wakiwa wameanza kutunishiana misuli na hivyo kutikisa ushirikiano wao teketeke wa kisiasa ambao ndiyo kwanza una miaka miwili, viongozi wa Afrika na dunia wanatazama hali hiyo kwa karibu.

Tayari Mwenyekiti wa Tume ya Afrika Mohamed Mahmat Faki, amefika DRC na kuzungumza na washirika hao wa kisiasa kujaribu kutafuta suluhu lakini inaonekana hakufanikiwa sana katika diplomasia yake hiyo.

Mara tu baada ya kuondoka kwake, Rais Tshisekedi alitangaza nia yake ya kutaka kuachana na ushirikiano wake huo na Kabila uliosababisha ashinde katika Uchaguzi Mkuu wa DRC uliofanyika miaka miwili iliyopita. Kwa sababu ya tofauti katika masuala ya kimsingi alizosema haziwezi kumalizwa, ushirikiano wa vyama vilivyounda umoja wa Cap for Change (CACH) na chama cha Kabila cha FCC (ambacho nacho ni muunganiko wa vyama vingine ndani yake) utasitishwa.

Nini chanzo cha mgogoro wa sasa?

Mgogoro wa Tshisekedi na Kabila ulikuwa uko chini chini tangu kuingia madarakani kwa rais huyo ambaye baba yake, Etienne, alikuwa na uhusiano usioridhisha na baba wa Kabila, Laurent pamoja na Kabila mwenyewe kiasi kwamba alipofariki dunia hakuweza kurudishwa kuzikwa nyumbani kwao DRC.

Tatizo kubwa la ushirikiano huu ni kwamba tangu mwanzo ilikuwa inaonekana Tshisekedi ni kama tu amemshikia nafasi Kabila akisubiri mwaka 2023 kwenye uchaguzi mwingine amwachie nafasi hiyo.

Vyombo mbalimbali vya habari vya kimagharibi, vilikuwa vikiandika kwamba kulikuwa na makubaliano rasmi kuwa Tshisekedi angetawala kwa muhula mmoja tu wa miaka mitano na kumwachia nafasi hiyo Kabila.

Kabila alikuwa akiringia wingi wake wa viti bungeni ambapo alikuwa na viti takribani 300 katika Bunge lenye wabunge 500. Tshisekedi na CACH yake ilikuwa na wabunge takribani 50 tu. Kwa sababu hiyo, ilitoa Waziri Mkuu, mawaziri muhimu katika serikali na Spika wa Bunge la DRC,

Mzozo wa kisiasa uliibuka baada ya Félix Tshisekedi kutangaza mpango wa kuvunja serikali ya muungano na wafuasi wa aliyekuwa rais wa taifa hilo, Joseph Kabila.

Wiki hii, pasipo kutarajiwa na wengi, wabunge walifanikiwa kumwondoa madarakani Spika wa Bunge, Jeanine Mabunda, kwa kupata zaidi ya nusu ya kura zote (280) – jambo lililoonyesha kwamba Tshisekedi ameingia ndani ya ngome ya Kabila na kwamba uhusiano wake mpya na wanasiasa kama Jean Pierre Bemba na Moise Katumba umeanza kuzaa matunda.

Walio karibu na Kabila wameeleza kwamba mstaafu huyu anataka kurejea katika wadhifa huo. Hatua za karibuni za Tshisekedi zinaonyesha amepania kuendelea kubaki madarakani kuzidi mwaka 2023 na kwa sababu ya ushawishi wa Kabila ndani ya jeshi na kwenye vyombo vingine vya dola; jambo hili lina dalili zote za kutoisha vizuri.

Kwanini DCR ikipiga chafya wengine wanapata mafua?

Kwa sababu ya utajiri wake wa madini na vito, DRC hutolewa macho na mataifa mengi duniani. Taifa limejaaliwa utajiri wa madini yenye umuhimu sasa na mengine katika wakati ujao. Yako mataifa makubwa duniani ambayo suala la madini haya ya DRC linahusu usalama wao kiuchumi.

Mgogoro wowote wa DRC huingiza makundi maslahi ambayo hufaidika kwa kutoa msaada kwa serikali na vikundi vya waasi ili yenyewe yajilipe kwa kuvuna utajiri huo. Wakati mwingine, makundi haya huwa ni nchi kamili.

Vikundi maslahi hivi husambaza silaha, askari wa kukodiwa na madini yanayochimbwa hushamirisha biashara ya madini na vito kwa njia za magendo. Haya ndiyo madini ambayo yalielezwa vizuri katika filamu ya Blood Diamond. Hivyo, mgogoro wowote wa DRC ni kichocheo cha kukua kwa biashara ya magendo ya madini katika eneo la maziwa makuu na kwingineko.

Ni muhimu pia kujua kwamba hali ya namna hii pia imekuwa ikisababisha matatizo baina ya nchi jirani na DRC. Mara nyingi, Rwanda imekuwa ikidai kuwa Burundi inafadhili vikundi dhidi yake vilivyoko eneo la Kivu Kaskazini. Burundi nayo imekuwa ikidai kuwa Rwanda inafadhili wapinzani wake walioko Kivu Kusini. Uganda inadai bado kuna mabaki ya kundi la Lord’s Resistance Army (LRA) walioko katika misitu ya taifa hilo.

Hali yoyote ya kulegea kwa amani katika DRC hutoa fursa ya baadhi ya mataifa haya kutaka kuingia nchini humo kwa kisingizio cha kutaka kusafisha maadui zake. Hata hivyo, kuna ushahidi kwamba wakati mwingine nchi hizo huingia kwa lengo la kuchota utajiri wa madini wa taifa hilo.

Makabiliano yalitokea baada ya Rais Tschisekedi kutangaza kuwa anataka kufanya mageuzi

Mwishoni mwa miaka ya 1990, Rwanda na Uganda ziliingia katika vita ndani ya DRC; kila nchi ikidai kutaka kupambana na waasi lakini kuna ushahidi kwamba zote zilikuwa zikitaka kufaidi utajiri huo wa taifa hilio. Kama hali hii ya Tshisekedi haitamalizwa kidiplomasia na kuishia kuwa mgogoro mkubwa, tarajia kusikia nchi jirani zikitafuta sababu ya kutaka kuingia.

Kiuchumi, DRC pia ni taifa muhimu kwa eneo la maziwa makuu. Taifa hilo halina bahari na hivyo mizigo yake mingi hupitia katika bandari za ama Dar es Salaam, Tanzania au Mombasa, Kenya. Kwa Tanzania, mizigo kutoka DRC ni muhimu kwa sababu takribani asilimia 30 ya mizigo ya nje katika bandari yake hiyo huwa inakwenda DRC.

Mgogoro wa aina yoyote wa kisiasa, hupunguza biashara katika eneo hili na maana yake ni kwamba majirani hawa wa DRC hupata athari za moja kwa moja. Ikiwa na takribani watu milioni 90; ambayo ni idadi kubwa kuliko nchi nyingine yoyote ya maziwa makuu, DRC ina soko kubwa na la uhakika kwa biashara nyingi.

DRC inazungukwa na majirani ambao baadhi yao hali zao kiusalama si nzuri sana. Majirani hao ni kama vile Sudan Kusini, Burundi, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Congo. Kuyumba kwa amani na usalama wa DRC kunafanya eneo lote la nchi hizo kuwa na wasiwasi kwa sababu ya kukua kwa biashara ya silaha za magendo.

Mgogoro wa aina yoyote ya DRC – endapo utaingia kuwa mgogoro kamili, unaweza kuwa kama mafuta ya taa au petroli katika eneo ambalo kuna moto unaowaka taratibu.

Ni muhimu kwa viongozi wa Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), kutafuta kwa haraka suluhisho la kidiplomasia la tatizo hili.

Bahati nzuri, Kabila ni kiongozi anayefahamiana na viongozi wengi wa nchi hizo na miongoni mwao yupo ambaye inafahamika ‘anammudu’. Jambo la kufanyika ni kuhakikisha usalama wa Kabila na familia yake kwa sasa na baadaye.

Kama Tshisekedi anaweza kumhakikishia Kabila, familia yake na watu wake wa karibu usalama wao na mali zao, hata wasipokuwa madarakani, hilo linaweza kushusha pumzi kwa wengi. Ni muhimu pia kwa Kabila kutafutiwa shughuli yenye hadhi ya kimataifa itakayomfanya asiwe ndani ya DRC kwa muda mrefu na ionekane ameheshimiwa.

Source link

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *