img

Uchaguzi Uganda 2021: Ni nani walio wahusika wakuu?

December 11, 2020

Dakika 9 zilizopita

ug

Waingereza wana msemo mmoja mashuhuri; ‘It takes two to Tango’, kwamba ili kunogesha dansi la muziki wa aina ya Tango wenye asili yake nchini Argentina, ni lazima kuwe na madansa wawili wanaocheza.

Kama ulivyo muziki wa Tango, uchaguzi pia ni jambo ambalo kufanyika kwake kunategemea kuwapo kwa mchezaji zaidi ya mmoja.

Wakati wananchi wa Uganda wakiwa wanajiandaa kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Januari 14 mwaka huu, ni vema kufahamu ni akina nani hasa watakuwa wahusika wakuu katika tukio hilo.

Kuna wahusika wa moja kwa moja katika mifumo yote ya kidemokrasia duniani kote – lakini pia kuna wahusika ambao ni mahususi kwenye muktadha wa chaguzi za taifa hilo la Afrika Mashariki linalokadiriwa kuwa na idadi ya watu milioni 43.

Watu binafsi

mseven

Mtu wa kwanza mwenye ushawishi mkubwa katika uchaguzi huu ni Rais wa sasa wa Uganda na mgombea wa nafasi hiyo kupitia chama tawala cha National Resistance Movement (NRM), Yoweri Museveni.

Yeye ndiye Mkuu wa Nchi, Mkuu wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu wa Uganda.

Kwa vyeo vyake hivyo, yeye ndiye atakayeamua uchaguzi ama uwe wa kiungwana na kiustaarabu au kihuni na usioheshimika.

Sura na tafsiri yoyote utakayoipata kuhusu uchaguzi wa Uganda popote pale ulipo, itatokana na namna Rais huyo atakavyoamua iwe. Mara nyingi, uchaguzi wa nchi huakisi aina ya kiongozi au serikali iliyo madarakani.

Ukiutazama uchaguzi wa Marekani uliofanyika Novemba mwaka huu, unapata taswira ya Rais Donald Trump. Kwa vyovyote vile, na kwa kuangalia yote yanayoendelea sasa nchini humo, hivyo ndivyo namna Museveni anavyotaka iwe.

Mtu mwingine muhimu katika uchaguzi huu wa Uganda ni mgombea urais kupitia chama cha upinzani cha NUP, Robert Kyagulanyi Ssentamu, maarufu kwa jina la Bobi Wine.

Kama mshindani mkuu wa Museveni, mwanasiasa huyu ni mmoja wa wahusika wakuu katika uchaguzi huu.

Bobi Wine anaweza kuwa mpinzani mkubwa zaidi wa utawala wa Museveni tangu kuruhusiwa kwa mfumo wa vyama vingi katika taifa hilo mnamo mwaka 1996.

m

Katika taifa ambalo wastani wa umri wa watu wake ni miaka 16 na asilimia 80 ya wapiga kura wana umri wa miaka kati ya 18 hadi 40, Bobi Wine ni mwanasiasa ambaye anashindana na Museveni kwa umaarufu na ushawishi miongoni mwa watu wa kundi hili.

Wiki chache zilizopita, kitendo cha Wine kukamatwa na msafara wake kupigwa mabomu ya machozi, kulisababisha vurugu katika maeneo mbali kabisa na alilokuwa kiasi cha kusababisha vifo vya watu.

Kwa mara ya kwanza, Museveni anashindana na mtu ambaye kuna kundi kubwa la watu linamuona kama alama ya upya wa uongozi na mwelekeo ambao taifa hilo linahitaji kwa sasa.

Mtu mwingine muhimu ni Kizza Besigye. Yeye hawanii urais katika uchaguzi wa mwaka huu lakini ndiye mgombea pekee wa upinzani kuwahi kupata asilimia 37 ya kura dhidi ya Museveni.

Kama Besigye atatangaza hadharani kwamba wafuasi wake wampigie kura Wine na kwamba yeye anamuunga mkono kwa asilimia 100, hilo linaweza kumaanisha mwanamuziki huyo wa zamani kupata kura nyingi kumzidi Kizza nap engine – kinyume cha matarajio ya wengi, kumshinda Museveni.

Ifahamike kwamba mshindi wa uchaguzi wa Uganda anatakiwa kupata asilimia 50 na zaidi kidogo ili kutangazwa mshindi. Kama Wine atazidi kidogo kura za Kizza na halafu washindani wengine tisa wa Museveni wakapata walau asilimia 10 ya kura zote, uchaguzi unaweza kwenda hatua ya pili na hapo lolote linaweza kutokea.

Janga la corona

Uganda inafanya kitu kinachoitwa “Uchaguzi wa Kisayansi”. Unaitwa hivyo kwa sababu Tume ya Uchaguzi iliamua kwamba kwa sababu ya ugonjwa wa Corona (Covid 19), taratibu za mikusanyiko kama ilivyozoeleka wakati wa kampeni hazitakuwepo tena.

Hii maana yake ni kwamba washindani sasa wanafanya zaidi kampeni kupitia vyombo vya habari kuliko mikutano ya hadhara kama ilivyozoeleka.

Jambo hili lina faida zaidi kwa chama tawala kuliko wapinzani.

Chama tawala kinatumia vyombo vya habari vya umma kujipigia kampeni wakati wapinzani hawana fursa hiyo.

Mikutano ya hadhara ni muhimu kwa vyama vya upinzani kuliko chama tawala kwa sababu zaidi ya moja.

bobi

Kwa mfano, Sensa ya Watu na Makazi ya Uganda ya mwaka 2014 ilionyesha kwamba ni watu milioni moja tu ndiyo wanamiliki televisheni na wengine milioni 3.4 ndiyo wanamiliki redio.

Katika nchi yenye watu zaidi ya milioni 40, hii ni sawa na asilimia juu ya kidogo ya nchi.

Kwa sababu hiyo, watu wengi zaidi wanakosa kufanya maamuzi baada ya mikutano kuliko kama ingeruhusiwa kama zamani.

Kwa sababu ya umaarufu wake kama mwanamuziki mashuhuri, Bobi Wine pia angekuwa na fursa ya kujaza watu wengi katika mikutano yake ya kampeni – jambo ambalo lingempa ushawishi zaidi kwa watu na pia angalau kusikilizwa.

Kwa sababu hiyo, ugonjwa wa Corona – kwa namna moja au nyingine umepunguza kidogo uhondo wa uchaguzi kama ambavyo ilikuwa imezoeleka na kwa namna fulani unampa faida mgombea wa chama tawala.

Taasisi kama wahusika katika uchaguzi huu

Taasisi kama wahusika katika uchaguzi huu

Uchaguzi wa Uganda unasimamiwa na Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo.

Kama zilivyo tume nyingi za Afrika, nayo pia imejiweka katika mazingira ambayo haionekani kuwa ni huru.

Watendaji wake wakuu akiwemo Mwenyekiti wake, Simon Byabakama, ni wateule wa Rais Museveni ambaye ni mgombea katika uchaguzi huu.

Mojawapo ya sifa kuu za nchi ambazo angalau watawala walio madarakani walishindwa katika chaguzi zao ni zile zilizokuwa na ama tume huru au Mahakama huru.

Katika mazingira ya Uganda, ni vigumu kuona ni namna gani tume ya uchaguzi inaweza kuhakikisha wagombea wote wanapata haki sawa za kisheria.

Taasisi nyingine muhimu katika uchaguzi wa Uganda mwaka huu ni vyombo vya habari.

Katika uchaguzi ambao mikutano ya hadhara haifanyiki kama kawaida, ni wajibu wa vyombo vya habari kuandika taarifa kwa ukweli, usahihi na bila upendeleo.

Hata kama kungekuwa hakuna ugonjwa wa Corona, bado umuhimu wa vyombo vya habari ungekuwapo kwa sababu hizo lakini uchaguzi huu wa “kisayansi” umefanya umuhimu wa vyombo vya habari kuwa mkubwa zaidi.

Viongozi wa jadi

Uganda ni mojawapo ya mataifa ya Afrika ambayo viongozi wa jadi bado wana umuhimu mkubwa. Yako makabila makubwa ambayo yanaongozwa na wafalme na machifu ambao wanasikilizwa na jamii zao kuliko hata viongozi wa serikali na vyombo vingine vya dola.

Kwa bahati mbaya, wengi wao hawafanyi maamuzi yao hadharani bali kwa kutumia njia zao zinazoeleweka kwa watu wao.

Kama watu wa kabila la Baganda wataambiwa kwamba mfalme wao, Kabaka, anamtaka mgombea fulani, bila shaka huyo ndiye atakuwa chaguo lao. Hali iko hivyo kwa viongozi wa makabila mengine ambao wengi wao wananchi wao ndiyo wale wasio na redio wala televisheni majumbani mwao.

Vyombo vya Dola

h

Nchini Uganda, vyombo vya dola vina kazi kubwa mbili wakati wa uchaguzi; kazi ya kwanza ni kufanya vitendo vya kutisha wananchi kwa kuwapiga na wakati mwingine kuwabagaza wapinzani lakini pili kuwafanya wanaopenda upinzani wawe na huruma kwa viongozi wao wanaoteswa.

Tabia hii huwa ni kama mapanga yanayokata kuwili; ikifanyika kwa kiasi, inaweza kuwafanya watu wasiende kupiga kura kwa woga na pia kuwaona wanaotaka madaraka kuwa ni watu dhalili lakini ikifanyika sana, inaweza kutia watu hasira na kuwa mbaya kwa serikali kama ilivyokuwa wiki chache zilizopita.

Vyovyote vile itakavyokuwa, vyombo hivi vya dola vitahusika na matokeo yoyote yatakayotangazwa na tume ya uchaguzi katika uchaguzi huo.

Source link

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *