img

Naibu Waziri Ndejembi awataka madiwani wa Jimbo lake kuzingatia maadili

December 11, 2020

UADILIFU, Maadili na Utendaji kazi uliotukuka ni mambo ambayo Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deo Ndejembi amewataka madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino kuwa navyo ili waweze kutekeleza yale yote yaliyoahidiwa wakati wa kampeni.

Naibu Waziri Ndejembi ametoa kauli hiyo leo wilayani Chamwino wakati wa uapisho wa Baraza la Madiwani ambalo yeye ni miongoni mwa madiwani kutokana na kuwa Mbunge wa Jimbo hilo la Chamwino.

Akizungumza baada ya uapisho huo, Ndejembi amesisitiza suala la maadili kwa madiwani wote kutoka majimbo mawili ya Halmashauri hiyo ambayo ni Jimbo la Chamwino ambalo yeye ndio Mbunge na Jimbo la Mvumi ambalo Mbunge wake ni Livingstone Lusinde ‘Kibajaji’.

Ndejembi amewataka madiwani hao kutanguliza mbele maslahi ya wananchi ili kuilinda imani waliyopewa na wananchi kwenye uchaguzi mkuu uliopita.

Leo tumeapa kuwa madiwani wa Halmashauri yetu, ni wazi tumeaminiwa na wananchi ili tuweze kuwatumikia na kuhakikisha tunaivusha Halmashauri yeti kutoka hapa ilipo na kuweza kuendana na hadhi ya Ikulu, hii ni kazi yetu wote tusikae majumbani twendeni zilipo kero na changamoto za wananchi kwa pamoja na watalaamu wa Halmashauri ili tukazitatue.

Niwaahidi ushirikiano, kama ambavyo tulishirikiana kwa pamoja kutafuta Kura za Rais Magufuli na zangu ndivyo inatupasa kushirikiana kuinyanyua Chamwino yetu, tuzingatie maadili na zaidi ya yote tumsaidie kazi Rais ya kuwatumikia wananchi wetu,” Amesema Naibu Waziri Ndejembi.

Kwa upande wake Mbunge wa Mvumi, Livingston Lusinde ‘Kibajaji’ amempongeza Ndejembi kwa kuteuliwa na Rais Magufuli kuwa Naibu Waziri katika ofisi yake jambo ambalo limeipa heshima kubwa Halmashauri yao ya Chamwino.

“Wabunge wote tuko zaidi ya 300 baraza la mawaziri lina mawaziri 21 na manaibu 22 Sisi kwenye Wilaya yetu kumpata miongoni mwetu mmoja akaaminiwa na Rais ni heshima sana, tunaamini uwepo wako kama Naibu Waziri utakua na manufaa kwa Serikali, Taifa letu na wananchi wa Chamwino kwa ujumla, tunamshukuru sana Rais Magufuli,” Amesema Lusinde.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *