img

Sakata la Kichuya, Simba yatoa tamko

December 10, 2020

 UONGOZI wa Simba umesema kuwa suala la mchezaji wao wa zamani ndani ya timu hiyo Shiza Kichuya kufungiwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa, (FIFA) pamoja na wao kutakiwa kulipa faini ya dola za kimarekani 130,000( M.300) bado hazijafika mezani kwao.

Habari zinaeleza kwamba Kichuya aliyesajiliwa na Simba kwenye dirisha dogo msimu wa 2019/20 kwa dili la miezi sita bado alikuwa ni mali ya timu yake ya zamani ya Pharco ya Misiri ambayo iliinasa saini ya nyota huyo kutoka Simba msimu wa 2018/19.

Nyota huyo alikuwa ameshitakiwa na Klabu ya Pharco ya Misri iliyoinasa saini yake msimu wa 2019 kutokana na madai ya kukatisha mkataba wake ndani ya timu hiyo kisha akajiunga na Simba Januari, mwaka huu.

Shauri hilo lilikuwa linafanyiwa uchunguzi na Kamati maalumu ya DR Congo iliyo chini ya FIFA kabla ya kutoka kwa maamuzi ya faini hiyo ya Kichuya kufungiwa.

Kaimu Mwenyekiti wa Simba, Mwina Kaduguda amesema:”Taarifa hizo bado ni mpya kwetu, Bodi ya Wakurugenzi hatujapokea taarifa rasmi kutoka kwa Ofisa Mtendaji Mkuu wetu, Barbara Gonzalez, hivyo tunasubiri taarifa rasmi ifikishwe kisha tutakaa kuijadili.

“Ila tunawaomba mashabiki wa Simba wawe watulivu kwa sababu maamuzi kama haya yanafanyika lakini hayamaanishi kuwa yapo sahihi.

“Kuna wakati maamuzi yanaweza kufanyika na yasiwe sahihi na ndiyo maana ipo nafasi ya kuweza kukata rufaa na maamuzi yakabadilishwa baada ya kupitiwa upya, nisingependa kuongea mengi kwa sasa tusubiri Barbara atalitolea ufafanuzi,” amesema.

Kwa sasa Kichuya anacheza ndani ya Namungo ambayo inashiriki Kombe la Shirikisho na Ligi Kuu Bara ikiwa chini Kocha Mkuu, Hemed Morroco.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *