img

Nana Akufo-Addo ashinda awamu ya pili ya urais wa Ghana

December 10, 2020

Rais wa Ghana Nana Akufo-Addo ameshinda awamu ya pili madarakani kufuatia kinyang’anyiro kikali cha uchaguzi wa urais. Tume ya uchaguzi imetangaza Jumatano Akufo-Addo amemshinda mpinzani wake wa muda mrefu John Mahama.

Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi wa Ghana, Jean Adukwei Mensa, amesema Akufo-Ado wa chama New Patritiotic, NPP, kinachofuata siasa za wastani za mrengo wa kulia, kimepata kura 6,730,413 sawa na asilimia 51.59. Mahama wa chama cha National Democratic Congress, NDC, kinachofuata siasa za wastani zinazoegemea mrengo wa shoto, kimejikingia kura 6,214,889 sawa na asilimia 47.36 ya kura.

Matokeo ya uchaguzi wa bunge katika majimbo yote 275 ya uchaguzi bado hayajatangazwa, lakini vyama vinatarajiwa kukabana koo.

Mahama, mwenye umri wa miaka 62, na Akufo-Addo, mwenye umri wa miaka 76, ni wasiasa wakongwe mahasimu ambao wamewahi kupambana mara mbili katika uchaguzi. Mahama alikuwa rais kwa miaka minne hadi 2016, kabla kurithiwa na Akufo-Addo. Chaguzi zote mbili walizochuana walitofautiana kwa idadi ndogo ya kura.

Idadi kubwa ya wapiga kura

Licha ya janga la virusi vya corona, idadi kubwa ya watu walijitokeza Jumatatu huku jumla ya watu 13, 434, 574 wakipiga kura, ikiwa ni sawa na asilimia 79 ya wapiga kura waliosajiliwa katika daftari la wapiga kura kwa mujibu wa tume ya uchaguzi.

Ghana | Präsidentschaftswahlen

Wafuasi wa chama cha NDC nje ya barabara kuu ya tume ya uchaguzi mjini Accra (08.12.2020) wakisubiri matokeo.

Ingawa kwa kiwango kikubwa upigaji kura ulifanyika kwa amani, polisi ilisema Jumatano kwamba watu watano waliuliwa kwenye machafuko yanayohusiana na uchaguzi,  hali inayoleta kiwingu katika taifa linalosifiwa kwa demokrasia yake thabiti.

Ghana imefanikiwa kukabidhi madaraka kwa njia ya amani mara saba tangu demokrasia iliporejea nchini humo zaidi ya miaka 30 iliyopita. Malalamiko ya baada ya uchaguzi kila mara yameshughulikiwa katika mahakama, jambo ambalo ni la nadra katika eneo la Afrika magharibi lililogubikwa na hali ya kuyumba kisiasa.

(afp)

Source link

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *