img

Matokeo ya Uchaguzi Tanzania 2020; Je, tutarajie nini katika Baraza jipya la Mawaziri wa Rais Magufuli?

December 10, 2020

  • Markus Mpangala
  • Mchambuzi, Tanzania

Dakika 3 zilizopita

BARAZA

Rais wa Tanzania, Dk. John Magufuli amewaapisha mawaziri wapya kuunda serikali yake baada ya kupita siku zaidi ya 30 bila kuwatangaza, huku akiwa ametangulia kuwateua mawaziri wa wizara mbili, Dk. Philip Mpango kuwa waziri wa fedha na Profesa Palamagamba Kabudi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje.

Magufuli anasifika kuchukua maamuzi magumu, kukemea, kufuatilia na kuwaondoa viongozi wasiomridhisha kiutendaji kwa namna yoyote ile katika serikali tangu alipoingia madarakani mwaka 2015.

Lakini sasa serikali yake inakabiliwa na kibarua cha kukidhi matarajio ikiwemo kutimiza ahadi katika sekta za Afya, elimu, kilimo, uchumi, miundombinu, kubadili taswira hasi ya serikali, pamoja na ushirikiano miongoni mwa mawaziri.

Duru za kisiasa zinasema Magufuli akiwa ameanza ngwe ya pili kutokana na uwingi wa matarajio ndani ya nchi hiyo anaelekea kuzidisha utumbuaji, kudhibiti mamlaka na uhuru wa mawaziri ambapo ilitengeneza udhaifu mkubwa katika Baraza lililopita kutokana na hofu ya wateule kukosa ubunifu.

Mtindo wa uongozi wake ni ule ambao unamfanya kufuatilia kila hatua, kukosoa hadharani makosa ya wasaidizi wake, pamoja na mawaziri wenyewe kushindwa kwenda sambamba na kasi ya kiongozi huyo.

Desemba 9 mwaka huu wa 2020 wakati akiwaapisha mawaziri amedhihirisha hilo kuwa John Magufuli ni yule yule, hulka zile zile, uamuzi wa haraka,ujumbe mkali, kutema nyongo.

Lakini duru za kisiasa zinatafsiri kuwa mwenendo wake umekuwa wa kujaribu kuwa kila mahali kutokana na anavyoshughulikia matatizo ya kila wizara na waziri husika.

Mathalani kutengua uteuzi wa Naibu waziri wa Madini Frank Ndulane hadharani imewahi kutokea kwa baadhi ya wateule wake akiwemo aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es salaam, Wilson Kabwe ambaye alitumbuliwa hadharani wakati wa uzinduzi wa Daraja la Kigamboni jijini humo.

Hii ni taswira yenye kuashiria umadhubuti uliopindukia hivyo kujenga dhana ya uongozi wa hofu pamoja na kufifisha nyota za mawaziri wake.

Ni upi uimara na udhaifu wa baraza jipya?

baraza

Maelezo ya picha,

Baraza jipya la mawaziri nchini Tanzania

Kwanza baraza jipya halina uwiano katika wizara kati ya pande mbili za Zanzibar na Tanzania Bara ambazo zinaunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Rais Magufuli amefanikiwa katika upande wa uwiano wa kikanda; Kanda ya Kusini, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Kati na Magharibi, Kanda ya Mashariki na Kaskazini kumekuwa na taswira nzuri.

Hata hivyo udhaifu umejitokeza katika Muungano, ambapo katika Baraza hili hakuna mawaziri kamili katika wizara zinazounda muungano kama vile Wizara ya Mambo ya Ndani, Muungano,Mambo ya Nje na Wizara ya Ulinzi.

Kimsingi mtindo wa utawala wa Magufuli ndio unaoamua mienendo ya mawaziri wake.

Matokeo ya hilo ni kuibua wasiwasi juu ya mawaziri walioteuliwa iwapo wanaweza kuwa wabunifu katika wizara zao kwa kuwa wengi ni wenye hofu kiuongozi.

Wengi huhangaika kuridhisha mamlaka za uteuzi wala si kuilinda Katiba na kutetea maslahi ya umma.

Hayo ni mambo ambayo yaliharibu taswira ya mawaziri kipindi cha kwanza cha miaka mitano iliyopita.

Je tumbua tumbua kujirudia baraza jipya?

Je tumbua tumbua kujirudia baraza jipya?

“Wote nimewaangalia hata wewe uliyeshindwa kuapa na tutateua mtu mwingine ambaye ataweza kuapa vizuri, najua Waziri Mkuu ananiangalia kwa sababu Lindi wametoka yeye na huyu aliyeshindwa kuapa, sasa tutamteua mwingine na wewe tutacheki digrii yako vizuri” alisema Rais Magufuli akielezea tukio la Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Francis Nduland kushindwa kuapa.

Ni uthibitisho kuwa ukali na rungu la Rais Magufuli litaendelea kuwang’oa mawaziri mbalimbali kama ambavyo amewahi kufanya kwa miaka mitano iliyopita.

Hoja hiyo inaungwa mkono na Wakili Stanislaus Kigosi ambaye amebainisha kuwa uwezekano wa kuibuka tumbua tumbua na kwamba kutokana na Rais kusimamia mchakato wa uteuzi wa wagombea ubunge wa ndani ya CCM, ni dhahiri ameunda baraza madhubuti, lakini rungu lake likawapiga mawaziri wengi kuliko miaka mitano iliyopita.

“Hili ni baraza madhubuti zaidi kwa sababu wateule wote wamepitia hatua zote toka mwanzo mpaka mwisho chini ya usimamizi wa Rais mwenyewe.

Zoezi lote kuanzia kura za maoni ndani ya chama mpaka kwenye kupitishwa na vikao vya juu vya chama rais alihusika na hata wale waliokatwa, basi walikatwa kwa ridhaa ya Rais Magufuli.

Pia kuna waliokatwa lakini vikao vya juu vya chama ambavyo Rais Magufuli ndiye alikuwa anaviongoza viliwarudisha, mfano Patrobas Katambi aliyegombea Shinyanga Mjini.

Kwahiyo umadhubuti unahitaji mawaziri imara ambao wanatakiwa kuwa tayari kutupwa nje ya baraza wakishindwa kazi ama maamuzi yoyote ya mamlaka,”

Kumbukumbu zinaonesha kuwa Aprili mwaka 2016 aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anne Kilango-Malecela aliondolewa madarakani siku 26 pekee toka kuanza kazi hiyo.

Anne Kilango-Malecela aliadhibiwa baada ya kutangaza kwenye vyombo vya habari kuwa mkoa wake haukuwa na watumishi fekis. Uchunguzi wa Ikulu baadae ulionesha kuwa walikuwepo watumishi feki 45.

Mwezi Mei 2016, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani Charles Kitwanga alifutwa kazi kwa tuhuma za kuingia Bungeni akiwa amelewa. Mawaziri wawili Profesa Sospeter Muhongo (Nishati na Madini) George Simbachawene (Ofisi ya Rais) walifutwa kazi kufuatia sakata la mchanga wa madini (makinikia) wa kampuni ya Acacia.

Julai mosi mwaka 2018 Mwigulu Nchemba alitumbuliwa katika wizara ya Mambo ya Ndani.

Rais Magufuli alitaja sababu 13 kumwondoa waziri huyo ikiwemo ajali za barabarani na matumizi mabaya ya fedha za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa. Hata hivyo alirejeshwa madarakani miaka miwili baadaye, na sasa amekuwa Waziri wa Katiba na Sheria 2020-2025.

Je, ni upi uhuru wa mawaziri wateule?

Rekodi zinaonesha kuwa Ilani ya CCM ya 2015-2020 ilibainisha kuwa watoto wanaopata ujauzito wataruhusiwa kurejea shuleni.

ikulu

Wakati Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na aliyekuwa Waziri wa Afya,Jinsia na Maendeleo ya watoto na Wazee, Ummy Mwalimu wakinadi mwelekeo wa serikali kuboresha afya na elimu juu ya watoto waliopata ujauzito kurudi shuleni, siku chache baadaye akiwa kwenye mkutano wilayani Bagamoyo mkoani Pwani, Rais Magufuli alipiga marufuku watoto waliopata mimba kurejea shule za serikali.

Tamko lile lilikwenda kinyume na chama chake kilichounda serikali, na zaidi waziri wake ambaye alishaanza kazi ikiwemo kuhitaji vibonzo vya sanaa ili kuelimisha madhara ya mimba za utotoni na wanafunzi.

Mantiki inaonesha kuwa Waziri Ummy Mwalimu ‘aliporwa’ uhuru na mamlaka kwa nafasi yake.

Malumbano kati ya Waziri wa Fedha, Dk. Philip Mpango na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda kuhusu Makontena yaliyosota bandarini kwa kile ambacho kiliitwa ‘Makontena ya Mkuu wa Mkoa”.

Makontena 20 yenye jina la Makonda yalitajwa kuwa yamebeba vifaa vya walimu vilivyochangiwa na Watanzania wanaoishi nchini Marekani, ambapo mkuu huyo wa mkoa wa zamani aliomba msamaha wa kodi na kukataliwa na Waziri wa Fedha mwenye dhamana ya kuamua msamaha wa kodi.

Hata hivyo Makonda hakutii amri ya Waziri Mpango wala Mamlaka ya Mapato (TRA) iliyotangaza kusudio la kupiga mnada makontena hayo kutokana na kutotolewa bandarini kama sheria inavyoagiza. Agosti 24, mwaka 2018 Rais Magufuli aliingilia kati sakata hilo akiwa katika mkutano na Madiwani wa wilaya ya Chato mkoani Geita.

Kuingilia huko kisiasa kulitafsiriwa kuwa mgogoro ndani ya serikali moja huku waziri mwenye dhamana akikosa uhuru kimamlaka.

Cassian Mbunda, mtaalamu wa Sayansi ya Siasa na Utawala bora, amemwambia mwandishi wa makala haya,” Udhaifu ulioonekana ni baadhi ya mawaziri kukosa ubunifu. Kwa mfano Wizara ya Maliasili na Utalii ambayo waziri wake ameondolewa, lakini pia ni hofu ama niseme uoga wa kufanya maamuzi kwa haraka miongoni mwa mawaziri kwa kipindi cha miaka mitano, kuanzia 2015 hadi 2020 na hilo limethibitishwa na Rais Magufuli mwenyewe katika hotuba yake ya kuapishwa mawaziri wapya tarehe 9 mwaka 2020. Kuna ujumbe hapo kwenye matamshi ya Rais, kwamba tumbua tumbua itaendelea kutumika kwenye baraza hilo.”

Kutamatisha muktadha huu, baraza jipya linakabiliwa na kibarua kigumu kufuta nyayo zote zenye migogoro,malumbano serikalini,kuibua ubunifu,utendaji wenye kiwango cha juu bilka kuhofia uamuziwa mamlaka juu ya mienendo yao iliyoko chini ya sheria.

Matarajio ya wengi ni kwamba Baraza jipya la mawaziri litahakikisha linaondoka na taswira hasi mbele ya wananchi, kinyume cha hapo linaweza kuenenda makosa yaleyale.

Source link

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *