img

Ajinyonga akiacha ujumbe mkewe si mwaminifu, mshirikina

December 10, 2020

 

Samweli Mbingilwa (54) almaarufu kama Kamanda amejinyonga hadi kufa akiacha ujumbe kuwa ‘mke wangu si mwaminifu katika ndoa na ananifanyia mambo ya kishirikina.’

Mwili wa Mbingilwa aliyekuwa mkazi wa Tambukareli mjini Mpanda ulikutwa kwenye kiti huku kamba ya chandarua aliyojifunga juu na kujining’iniza ikiwa kimekatika.

Mke wa marehemu, Maria Nswima alisema siku kadhaa kabla ya kujiua, mumewe alichoma moto nguo zake huku mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Tambukareli, Selestino Shauritanga akisema Mbingilwa aliwahi kunywa dawa akitaka kujiua.

Akieleza zaidi, Shauritanga alisema taarifa za tukio hilo alipata kwa watoto wa marehemu waliomweleza kuwa baba yao amefariki lakini hawakumjuza chanzo cha uamuzi huo. Hata hivyo, mwenyekiti huyo alikiri kuwa wanandoa hao walikuwa na ugomvi uliotokana na wivu wa mapenzi.

“Siyo mara ya kwanza kusuluhisha ugomvi kati yao, walikuwa wafanyabiashara wa pombe za kienyeji na kilabu kipo nyumbani kwao, kwa hiyo wateja wakinunua na kuongea na mkewe (Mbingilwa) alikuwa anachukia,” alisema Shauritanga.

Mwenyekiti huyo alifafanua kuwa marehemu, enzi za uhai wake, aliwahi kunywa dawa ili ajiue lakini akaokolewa mapema.

Kamanda wa polisi Mkoa wa Katavi, Abdi Issangu alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema “ni tukio la kweli na mwanaume huyo ameacha ujumbe unaosema, ‘mke wangu siyo mwaminifu katika ndoa na ananifanyia mambo ya kishirikina.”

Akieleza ilivyokuwa, Maria alisema Novemba 25 mwaka huu mumewe alikwenda kilabuni lakini kesho yake kuliibuka ugomvi kati yao na akamtishia maisha.

“Nilimpisha nyumbani ila saa mbili usiku nikarudi akaniambia leo ni siku yako ya mwisho, nikamuuliza kivipi akajibu ya mwisho kuishi. Kuona hivyo niliamua kwenda kwa mwenyekiti lakini sikumkuta…baada ya kurudi nyumbani nikakuta amechoma nguo zangu zote moto na kukatakata masufuria pamoja na kupasua mabakuli yote.”

Kutokana na hali hiyo, alisema “nilienda kituo cha polisi nikaeleza na kupewa wito niliompelekea balozi akampa lakini watoto wakaniambia ameichana, hii hapa. Nikavichukua hivyo vipande na kuvipeleka kwa mwenyekiti akaniambia rudi tena polisi, nikarudi…tangu siku hiyo niliamua kuishi kwa shangazi yangu,” alisema Maria.

Alisema Desemba 5 saa 11 jioni mtoto wake alikwenda kumpa taarifa kuwa baba yao amejinyonga chumbani kwake.

“Baada ya kufika nilikuta ametumia chandarua ambacho kilikuwa imekatika na yeye alikuwa amekaa kwenye kiti akiwa amefariki tayari. Ilikuwa kawaida yake kwenda kunywa pombe akirudi lazima kelele ziwepo lakini baadaye zinaisha,” alisema Maria.

licha ya uvumilivu aliounyesha kwa miak amingi waliyoishi pamoja, Maria alisema “awamu hii alizidisha, nikaamua kuondoka. Nimezaa naye watoto saba, naumia kwakuwa nilimzoea. Sikuwahi kufikiria kama anaweza kujinyonga,” alisema.

Kaka wa marehemu, Daniel Peter (75) anayeishi Kilimahewa mjini hapa alisema amemshangaa ndugu yao kuchukua uamuzi huo ambao hakuwahi kuutamka au kuonyesha dalili za kuutekeleza.

“Ni mdogo wangu wa mwisho, alikuwa dereva wa magari madogo ya abiria kwa muda mrefu lakini alipumzika, nilishangaa nilipopigiwa simu kuwa amefariki. Eti amejinyonga kwa kutumia kamba ya neti. Nilikuwa nakutana naye, kuna wakati alikua na furaha mwingine hana, baada ya kumpekua wakaona karatasi ya ujumbe wakadai nitafuatilia kwa hiyo sijui kilichokuwa kimeandikwa,” alisema Peter.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *