img

Waridi wa BBC: ‘Tulitengana miaka mitatu lakini baadae tukarudiana’

December 9, 2020

Dakika 2 zilizopita

Virginia Muthoni

Maelezo ya picha,

Virginia Muthoni na mumewe David Wahome walitalakiana na kisha kurejesha ndoa yao

Ndoa ni baraka, na wanawake wengi hufurahia kumpata mume ambaye hutarajia kujenga maisha ya furaha kwa pamoja.

Lakini kwa upande wa Virginia Muthoni, mwanamke kutoka nchini Kenya aliyempata mume mwaka 2011 hali ndivyo sivyo.

Safari yao ya ndoa inafanana na simulizi kwenye filamu, lakini ni matukio halisi waliyoyapitia.

Ilikuwaje maisha ya furaha yakageuka kisa?

Mwanzo wa yote

Kwa mujibu wa Virginia, ndoa hiyo ilianza kukumbwa na misukosuko na ugomvi.

“Wakati mwingi mume wangu alikuwa anafika nyumbani na kuanza kunipiga makofi kwa makosa madogo madogo ambayo tungeliyasuluhisha bila kupigana,” anasema.

Virginia Muthoni

Aidha, mumewe alianza pia kunywa pombe na nyumbani kukawa hakukaliki.

Mwanamke huyu anasema kuwa kwa mtazamo wake hakuona kikubwa ambacho kilikuwa kinamsukuma mume wake kumpiga kila wakati na kunywa pombe kupita kiasi.

Masaibu katika nyumba hiyo yalianza kupungua pindi mwanamke huyo alipopata ujauzito wake wa kwanza.

Mume wa Virginia, David Wahome, alijawa furaha iliyodhihirika mbele ya jamii kwani hakuficha furaha hiyo kwa kila mmoja aliyekuwa karibu naye.

Mume wa Virginia alibadilika na kuwa mume mwema na mwenye busara kwa mke wake.

Misukosuko ilikoma na akawa mtu mwenye utulivu huku akisubiri baraka ya kuzaliwa kwa kifungua mimba wake.

Nini kilichotokea baada ya mtoto wao kuzaliwa?

”Furaha ya mume wangu iligubikwa na wingu jeusi pale nilipofikishwa hospitalini kujifungua mtoto ambaye tulikuwa tumemsubiri kwa miezi tisa.

Nilijifungua mtoto wa kiume ambaye alifariki ghafla baada ya kuzaliwa, lilikuwa pigo kubwa kwetu.

Kila mmoja wao alianza kuomboleza kivyake. Mume wake alianza tena kunywa pombe kupita kiasi, huku akiwa na wapenzi wengine nje ya ndoa.

Hali ambayo Virginia anasema ilizidisha kidonda cha maumivu ya kumpoteza mtoto aliyedhani angeleta mabadiliko katika familia hiyo changa.

”Ugomvi na kichapo vilianza tena, mume wangu alinilaumu kwa kusababisha kifo cha mtoto wetu. Alikuwa amesubiri kwa hamu kuzaliwa kwa mtoto huyo, nadhani alikuwa na msongo wa mawazo na nafikiri hiyo ndio iliyokuwa sababu yake kunipiga kila wakati,” anakumbuka Virginia.

Virginia aliamua kushika mimba kwa haraka akitumaini kuwa mambo yangetulia kwa mara nyingine pale nyumbani. Mungu akajibu ombi lake na akapata ujauzito kwa mara ya pili.

Je, uja uzito wa pili ulileta afueni?

Muthoni

Alishika mimba bila matatizo na hatimaye wakaajaliwa mtoto wa pili aliyekuwa mtoto wa kike. Kwa mujibu wa na mama huyu mume wake alionekana kuridhika na kurejesha fahari ya kuwa baba kwa mara ya pili.

”Mume wangu alifurahi sana, nadhani hakuna hata rafiki yake mmoja ambaye hakufahamu kuwa nilikuwa nimejifungua mtoto. Huyu mtoto alileta amani na furaha katika nyumba iliyokuwa imejawa na malumbano ya kila siku,” anakumbuka Virginia.

Ila amani ile haikudumu. Mume wake alianza tena tabia ya kunywa pombe huku akifululiza na kumpiga Virginia mara kwa mara.

Tayari Virginia alikuwa ametoroka mara zisizohesabika na kurudi mambo yakitulia nyumbani .

Kulingana na mwanamke huyu mume wake alikuwa na tabia ya kuwa na uhusiano wa nje na wanawake wengine, na Virginia anasema kuwa mmojawapo wa sababu kuu ya ndoa yao kupata misukosuko ilikuwa ni vimada ambao walikuwa wanatawala maisha ya mume wake .

Kwa mfano anasema kuwa kila wakati alikuwa anapokea simu kutoka kwa wanawake ambao walikuwa marafiki wa mume wake na kumkejeli .

Muthoni

Virginia anasema kuwa mume wake alikuwa na marafiki ambao walikuwa wanasaidia kusambaratisha ndoa yao.

Kwa mfano anasema kuwa badala ya kumpatia mawaidha ya kujenga alikuwa anapata mawaidha ya jinsi ya kuondoka kwenye ndoa yao.

Kwa hivyo Virginia alijipata akiwa mpweke katika ndoa ile.

Na katika pilikapilika hizo aliamua kuondoka nyumbani kwake na kuanza maisha upya.

Hii ilikuwa wakati ambapo mmoja wa marafiki wa mume wake ambaye alikuwa mwanaume alikuwa na mazoea ya kutembea huko na kulala usiku kucha.

Virginia hakuwa anafurahia mtindo huo na alipojaribu kumshawishi mumewe kumfukuza rafiki yake, mambo yaligeuka na kukawa na vita pale nyumbani.

“Badala ya mume wangu kumfukuza rafiki yake aliamu kunifukuza mimi. Niliamua kuondoka bila chochote, kumwachia nafasi ya kufikiria iwapo ndoa yetu ilikuwa muhimu kuliko rafiki yake wa kiume au la, ila nilipoondoka hakuna aliyenitafuta,” anasema Virginia.

Mfarakano na kimada

Baada ya siku kadha aliamua kurejea nyumbani kwake kuchukua nguo zake pamoja na mtoto wao, ila alichokipata pale ni kuwa mumewe alikuwa amechukua mmoja wapo wa vimada aliokuwa nao, na kumuweka nyumbani kwao kama mke.

Ilitokea fujo kuu pale nyumbani, Virginia anasema.

“Ni vigumu kuamini kuwa kimada wa mume wangu ndiye alikuwa anazitoa na kutupa nguo zangu pamoja na za mtoto wetu nje ya nyumba. Yule binti alikuwa na kasi kuu kuliko hata mume wangu. Nilitamaushwa na yaliokuwa yanafanyika na ghafla nikaamua kuichoma ile nyumba yetu,” Virginia anakumbuka.

Kulingana na mwanadada huyu aliwasha moto ambao ulichoma baadhi ya vitu ila watu walifanikiwa kuuzima.

Hivyo ndivyo Virginia alianza maisha yake upya baada ya ndoa kuonekana kana kwamba imekwisha.

Muthoni

Alihama mbali na nyumbani kwake huku akijikusanya na kuanza maisha mapya yeye na mwanae wa kike.

Virginia alikiri kuwa hakufahamu alikuwa anapitia msongo wa mawazo katika kipindi cha miaka mitano aliyokuwa kwenye ndoa.

Kutokana na matukio mengi pale, kichapo, ugomvi wa kila mara na hata kupoteza mwanae wa kiume baada ya kuzaliwa.

Alipitia ushauri nasaha na pia alijihusisha katika masuala ya kidini na kuamua kumcha Mungu.

Wakati huo wote Virginia anasema kuwa hakuwa ameacha ndoa yake kimawazo na kwenye moyo wake .

Amini usiamini wawili hawa walitengana na kuamua kila mtu aende kivyake hali iliyodumu kwa miaka mitatu.

Mumewe aliamua kuoa mmoja ya wanawake waliokuwa vimada wa nje akidhania kuwa angepata amani na utulivu wa moyo, ila ilisalia kuwa wangerudiana na kuanza ndoa upya.

Baada ya dhiki faraja?

Baada ya miaka mitatu Virginia aliamua kumpigia simu mumewe kumjulia hali, ila sauti aliyoisikia kutoka upande wa pili wa simu ilikuwa ya kutamausha sana.

Mume wake alijibu kwa huzuni na upweke mwingi .

“Nilipompigia simu na tukakutana alinieleza kuwa tangu nitoke kwenye nyumba yetu, maisha yalikosa ladha na kuwa hakuna hatua zozote chanya aliweza kuzipiga katika kipindi hicho walipokuwa wametengana, pia yule kimada aliyemfukuza alikuwa tayari ameondoka pale nyumbani kwangu,” Virginia alisimulia.

Hatimaye Virginia na mumewe walianza maisha upya wote wakiwa wamepiga moyo konde na kuamua kujenga ndoa upya, Ndoa ambayo imepitishwa kwenye moto, ndoa ambayo imestahimili yote na kuamua kuweka msamaha mbele.

Maoni yake mume wa Virginia ambaye pia alizungumzia hali hii ni kuwa wakati mwengine marafiki wa nje huwa na uwezo wa kuathiri ndoa za wenzao kupitia maneno na matendo wanayoyafanya na kuyasema .

“Wakati mwengine unapata kuwa wale ambao wako karibu na wewe hata jamaa wako ndio wale wale ambao wanaangamiza ndoa za watu bila ufahamu wa wahusika, jambo jingine ni kuwa yule kimada ambaye niliamua kuishi naye hakunitosheleza kwa vyovyote kumaanisha kuwa mtu wako ni wako hata ufanye nini yule ambaye Mungu amekuwekea hata ufanye nini lazima mtarudiana kwa wakati mmoja,” alisema David mumewe Virginia.

Mumewe Virginia anasema kuwa alijaribu sana kuishi na kimada wake, lakini bado zile fujo zake na Virginia zilianza kunyemelea nyumbani kwake.

Alikuwa na matumaini kuwa pengine akiacha matumizi ya pombe mambo atayaacha lakini bado ilionekana kuwa changamoto, na la zaidi kichapo na fujo kati yake na kimada zilikuwa ndivyo kibwagizo chao.

Muthoni

Bwana David anasema kuwa alikuwa ameamua kuanza maisha mapya na mwanamke mwingine akitumaini kuwa angerejesha amani katika maisha yake , ila mambo yaliharibika zaidi.

Anakiri kuwa alidhani kuwa Virginia alikuwa sio mke mwema kwani ugomvi na vita vilikuweko asijue kuwa hata yeye pia alikuwa na mchango wake katika kuharibika kwa ile ndoa .

“Wakati nilipoamua kukaa na kimada, nilimchukua akiwa na mtoto mmoja wa nje, baada ya muda alishika mimba, japo kwa bahati mbaya ili mimba ilitoka.

Kuachana kwetu kulikumbwa na vurumai kubwa mno kiasi cha kwamba ilibidi tuachanishwe kwenye kituo cha polisi ni kumaanisha kuwa Virginia ndio mke wangu halisi na yale niliyokuwa n yajaribu kule nje yalikuwa ni maigizo,” alisema David.

Source link

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *