img

Mbilinyi kuratibu Ligi ya Mbunge Mwakamo

December 9, 2020

Na Omary Mngindo, Mlandizi

MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Vijijini Mkoa wa Pwani Michael Mwakamo, amemteua Nassoro Shomvi Maarufu Mbilinyi kuwa Mratibu wa michuano ya Mbunge jimboni humo.

Akizungumza na Mwandishi wa habari mjini hapa, Mwakamo alisema kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa ahadi yake ya kuwepo kwa ligi ya Mbunge, itayochezwa katika kipindi chote cha miaka mitano ya kwanza inayoanzia 2020/2025.

Alisema kwamba Mbilinyi aliyekuwa mratibu katika harakati za Kampeni, amempatia nafasi hiyo atayoshirikisha na wadau maarufu wa michezo akiwemo mchezaji mkongwe Charles Kilinda, Katibu Mstaafu wa timu za JKT Ruvu Ivan Chenga na wengine kadhaa.

“Nilipokuwa katika Kampeni nikiinadi Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), niliahidi michezo ambayo ipo ndani ya ilani, nitaitekeleza kwa vitendo kipindi cha miaka mitano ya kwanza, nimemteua Mbilinyi aanze kuratibu zoezi hilo,” alisema Mwakamo.

Alisema kuwa ameamua kuanza na soka kutokana na kuwa na wapenzi wengi katika maeneo yote ya nchi na duniani kwa ujumla, na kwamba wakati ligi hiyo ikianza atatafuta wadau wa mchezo wa Netiboli na michezo mingine, lengo ni kuibua na kuendeleza vipaji vya michezo mbalimbali.

Akizungumzia uteuzi huo, Mbilinyi alimshukuru Mbunge huyo huku akisema kuwa ameshaanza mazungumzo ya awali na wadau wa mchezo huo akiwemo Kilinda na Chenga, ili kuweka mambo sawa, hatimae malengo ya Mbunge huyo yatekelezwe kama dhamira yake ya kucheza mpira.

“Binafsi nampongeza Mbunge kwa kuona ninafaa kusimamia kitengo cha kuratibu michezo ya Jimbo, tayari nimeshaanza mazungumzo ya awali na wakongwe Charles Kilinda na Ivan Chenga, nina imani kubwa kwamba watakuwa msaada wa kufanikisha malengo hayo,” alisema Shomvi.

Mratibu huyo alimalizia kwa kuwataka viongozi wa vilabu jimboni humo kuendelea na maandalizi ya vilabu vyao, tayari kwa kinyang’anyiro cha Ligi ya Mbunge ambayo inaweza ikaanza wakati wowote baada ya maandalizi yake.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *