img

Mambo muhimu ya kuzingatia kabla ya kuomba mkopo

December 9, 2020

 

Kutokana na kipato cha watu wengi kutokutosheleza mahitaji yao, hujikuta wakilazimika kukopa. Wapo waliofanikiwa sana kwenye mipango yao kutokana na mikopo, lakini wapo pia waliofilisika kutokana na mikopo.

Kwa hakika swala la mikopo linahitaji umakini mkubwa pamoja na mipango na mikakati stahiki ili lisije likakuingiza kwenye madeni yasiyokwisha.

Ikiwa una mpango wa kukopa, basi fahamu mambo matano muhimu ya kuzingatia kabla ya kuomba mkopo.

1. Bainisha uwezo wako wa kifedha
Ili upate na utumie mkopo vyema, ni muhimu ufahamu uwezo wako wa kifedha. Ikiwa uwezo wako wa kifedha ni shilingi milioni moja, ukikopa mkopo wa bilioni 1 hutoweza kuupata wala kuurejesha.

Hakikisha unatathimini kipato chako pamoja na uwezo wako wa kutumia pesa ili usije ukatumbukia kwenye madeni.

2. Andaa mpango wa matumizi na marejesho
Watu wengi hushindwa kupata mkopo au kurejesha mkopo kutokana na kutokuwa na mpango mzuri wa matumizi na urejeshaji wa mkopo.

Hakikisha kabla ya kukopa unaandaa mpango mzuri na unaotekelezeka na namna utakavyotumia pamoja na kurejesha mkopo wako. Usikope ndipo upange, bali panga ndipo ukope.

3. Fahamu kuhusu riba
Benki ni taasisi zinazofanya biashara ili zipate faida; benki hufanya biashara hasa kwa kupitia mikopo. Ni muhimu kufahamu vyema kiwango cha riba utakachotozwa kutokana na mkopo uliokopa.

Watu wengi wameingia kwenye matatizo makubwa baada ya kujikuta wakikopa mikopo yenye riba kubwa sana. Hakikisha unafahamu riba utakayotozwa na utathimini kama utaweza kuimudu.

4. Fahamu muda wa mkopo
Kadri mkopo unavyokuwa wa muda mrefu ndivyo na kiwango chake cha kulipa kwa mwezi huwa kidogo. Hivyo ni muhimu sana kuchunguza muda wa kurejesha mkopo ili uone kama unaweza kumudu kurejesha mkopo huo ndani ya muda husika.

5. Fahamu gharama nyingine za mkopo
Mara nyingi mikopo huambatana na gharama nyingine kama vile gharama ya kuchakata mkopo, gharama ya kurejesha mapema zaidi, gharama ya kujiondoa mapema, n.k.

Ni vyema ukafahamu gharama hizi ili uone kama utazimudu vyema. Hakikisha waraka wa mkopo unaopewa unausoma na kuuelewa vyema kabla ya kuidhinishiwa kupokea mkopo ili kuepusha matatizo yoyote mbeleni.

Kwa hakika mikopo imewasaidia wengi lakini pia imewafilisi wengi kutokana na kutokufahamu mambo ya muhimu ambayo wangepaswa kuyazingatia kabla ya kuomba mkopo.

Hakikisha hukopi pesa kwa ajili ya matumizi ya anasa au yasiyokuwa ya msingi kwani utatumbukia kwenye madeni makubwa yasiyolipika.
,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *