img

Kigwangalla aomba radhi, aeleza alivyoonja kifo

December 9, 2020

Aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamis Kigwangalla, ameomba radhi kwa yoyote ambaye alimkwaza kwani halikuwahi kuwa lengo lake kukwaza watu, bali ilikuwa ni katika jitihada zake za kujaribu kufanya mambo yafanikiwe.

Dkt. Kigwangalla ameandika hayo hii leo Desemba 9, 2020, kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Instagram, ambapo pia ametumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Magufuli kwa imani yake pamoja kumpongeza mrithi wa nafasi yake ya Uwaziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro.

“Mimi sina kinyongo na mtu, na naomba sana niliowakwaza wanisamehe, nimempongeza Dkt. Damas Ndumbaro,Waziri wa Maliasili na Utalii na nakusudia kesho kwenda kumkabidhi rasmi ofisi, nawapongeza mawaziri wote na nawaahidi ushirikiano wangu wakati wote”, ameandika Dkt. Kigwangalla.

Aidha akielezea safari yake ya maisha wakati wa uongozi wake, Dkt Kigwangalla, amesema kuwa miaka mitano iliyopita haikuwa rahisi kwake, kwani kilikuwa ni kipindi kilichojaa furaha na maumivu, uhai na mauti.

“Ni kipindi nilichonusa kifo na kufufuka, ni kipindi nilichoshangilia na nilicholia machozi ni kipindi nilichopata ulemavu wa milele na maumivu yasiyoisha wala kusahaulika, siwezi kumlalamikia Mungu kwa lolote lile zaidi namshukuru kwa kuwa hai, na kwa nyakati zote nilizopitia, za kiza totoro na za mwangaza”, ameandika Dkt. Kigwangalla.

“Kipindi hiki nilipewa heshima ya kuwa msaidizi wa Rais kwa nafasi nyeti serikalini (Afya na Maliasili na Utalii), naomba nitumie fursa hii kumshukuru Rais Dkt. Magufuli, kwa imani yake kubwa kwangu, kwa maelekezo na usimamizi wake, si tu alikuwa kiongozi wangu mkuu bali pia alikuwa Mwalimu na Baba, sintosahau huruma na upendo alionionesha nilipopata ajali na msiba wa mwanangu”, ameongeza.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *