img

Mbaroni tuhuma za kumuua mwanafunzi

December 8, 2020

 

Jeshi la Polisi mkoani hapa linamshikilia Hamis Omary (19) kwa tuhuma za mauaji ya Vicent Renatus, mwanafunzi wa kidato cha pili Sekondari ya Katunguru.

 Jana, kamanda wa mkoa, Jumanne Muliro alisema tukio hilo lilitokea Desemba mosi saa 5:00 asubuhi katika Mtaa wa Msumbuji.

Kamanda Muliro alisema mwanafunzi huyo alikutwa ameauawa chumbani kwake huku mwili wake ukiwa na majeraha shingoni.

“Baadhi ya vitu vya mwanafunzi huyo vilivyokuwamo chumbani kwake viliporwa ikiwamo runinga na redio aina ya sub-woofer,” alisema Muliro.

Baada ya hapo, alisema jeshi lilianza kufanya msako mkali likitumia taarifa za kiintelijensia na kufanikiwa kumtia mbaroni Omary ambaye ni mkazi wa Nyasaka Msumbiji jijini hapa anayetuhumiwa kutenda kosa hilo.

Baada ya kuhojiwa kwa kina, alisema mtuhumiwa alikiri kutenda kosa hilo na akawaonyesha vitu vilivyoporwa kwa marehemu.

Baada ya uporaji huo, Omary alienda kuviuza vitu hivyo kwa Erasto Jackson (22), mkazi wa Kitangiri ambaye naye alikamatwa.

Jackson alikamatwa kwa tuhuma za uhalifu sugu wa kupokea mali za wizi.

Muliro alisema wanaendelea na uchunguzi kubaini wahusika wengine wa tukio hilo kabla ya kuwafikisha watuhumiwa wote mahakamani.

Katika tukio jingine, Jeshi la Polisi mkoani hapa limewakamata watu wawili waliokuwa wakijitambulisha kuwa watumishi wa Idara ya Usalama wa Taifa kisha kutapeli watu waliokutana nao.

Wawili hao, kamanda Muliro alisema walikuwa wakijinadi kuwa wao ni maofisa kipenyo wa idara hiyo nyeti ya Serikali.

Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Severine Edward Mayunga (32) ambaye alikutwa na kitambulisho kinachoeleza kutolewa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Idara ya Usalama wa Taifa kitengo cha kikosi maalumu.

Mtuhumiwa huyo alikuwa na namba za kijeshi, MT 82863 akiwa ni ofisa kipenyo. Mwingine ni Abel Mboja wote wakazi wa Kishili jijini hapa.

Baada ya kuwahoji, kamanda Muliro alisema watuhumiwa walikiri kuhusika na utapeli na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu hivyo wanakamilisha utaratibu wa kuwafikisha mahakamani kwa hatua zaidi.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *