img

Kuvunjika kwa ushirikiano wa Tshisekedi na Kabila kuna maana gani?

December 8, 2020

Dakika 3 zilizopita

Joseph Kabila na Felix Tshisekedi

Kwa baadhi ya wachambuzi wa siasa za nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), uswahiba wa kisiasa baina ya Rais Felix Tshisekedi na mtangulizi wake, Joseph Kabila, ulikuwa wa mashaka tangu siku ya kwanza.

Kwa sababu hiyo, haishangazi kwamba mwishoni mwa wiki iliyopita, Rais Tshisekedi aliamua kutangaza kuvunjika kwa ushirikiano wa kisiasa uliomweka madarakani miaka miwili iliyopita – uhusiano ambao sasa umedhihirika kwamba ulikuwa na matatizo kwa karibu kipindi chote.

Ili kushinda dhidi ya aliyekuwa mpinzani wake katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2018 nchini humo, Martin Fayulu, Tshisekedi aliunda ushirikiano wa vyama vya upinzani uliojulikana kwa jina la Cap for Change (CACH) ambao uliungana na chama tawala cha FCC cha Kabila huku kufanikisha lengo hilo.

Hata hivyo, katika taarifa yake kwa umma aliyoitoa Desemba 6 mwaka huu, Tshisekedi alisema uhusiano huo sasa utashindwa kwa sababu ya tofauti ya kimaono katika namna ya uendeshaji wa serikali.

Rais huyo ambaye ni mtoto wa aliyekuwa mwanasiasa mashuhuri wa upinzani wa DRC, Etienne Tshisekedi, alisema mambo ambayo ushirikiano huo ulishindwa kupata uelewa wa pamoja ni masuala ya ulinzi na usalama, kinga dhidi ya wafanya maovu, rushwa na mabadiliko ya uendeshaji wa uchaguzi.

Uamuzi huo wa Tshisekedi ulitarajiwa na wengi lakini umeibua mjadala mkubwa kwa sababu ya athari za kisiasa zinazoweza kutokea na sasa kila mfuatiliaji wa siasa za DRC anatazama ni kwa vipi kiongozi huyo mchanga ataweza kuchanga karata zake.

Atapataje wingi wa wabunge bungeni?

Mtihani wa kwanza kwa Tshisekedi ni namna atakavyoweza kupata wajumbe wengi ndani ya Bunge la DRC lenye wabunge takribani 60. Hadi sasa, alifanikiwa kuendesha mambo kwa sababu aliungana na FCC cha Kabila chenye wabunge zaidi ya 300.

Kuendelea kuwa kinara wa serikali, itamlazimu Rais huyu atafute namna ya kuwa na wingi wa viti bungeni. Yeye na wenzake katika CACH wana idadi ya viti takribani 50 bungeni na hivyo anahitaji kutafuta namna ya kuongeza wabunge wake.

Endapo itashindikana kufanya hivyo, Tshisekedi atalazimika kuvunja Bunge na kuitisha uchaguzi upya; jambo ambalo ingawa ni gumu kulifanya, wachambuzi wa siasa za DRC wanaamini ni kitu kinachowezekana kufanyika.

Hata hivyo, kwa mujibu wa vyombo mbalimbali vya habari vya DCR na vya kimataifa, Tshisekedi – kimyakimya, ameanza mikakati ya kujiongezea wabunge kwa kutafuta muungano mpya na vinara wengine wa upinzani wa taifa hilo.

Majina yanayotajwa kuhusishwa na kuungana na Kabila ni Moise Katumbi – Gavana wa zamani wa Jimbo la Katanga, na mwanasiasa maarufu, Jean Pierre Bemba. Wawili hao pekee, wanaweza kumpa Tshisekedi wabunge wapya takribani 100 ndani ya bunge hilo.

Mtihani wa kwanza kwa Tshisekedi ni namna atakavyoweza kupata wajumbe wengi ndani ya Bunge la DRC

Tatizo ni kwamba, hata kama atasaidiwa na akina Bemba na Katumbi, Tshisekedi atakuwa na wastani wa wabunge 150 tu na hivyo bado FCC cha Kabila kitakuwa na wabunge takribani mara mbili yao hata kwa kuungana kwao huko.

Ndiyo sababu, kuna minong’ono ndani ya DRC kwamba Tshisekedi na akina Bemba tayari wameanza kumtongoza kiongozi wa chama cha Alliance for Democratic Forces of Congo and Allies (AFDC-A), Modeste Bahati Lukwebo – ambacho ni mojawapo ya ngome za FCC ambayo kimsingi nayo ni muunganiko wa vyama tofauti.

Lukwebo, ambaye chama chake pia kina wabunge wengi ndani ya FCC, aliingia katika mzozo na Kabila baada ya rais huyo wa zamani kuamua kumuunga mkono Alexis Thambwe Mamba, katika kinyang’anyiro cha kutafuta Rais wa Bunge la Seneti la DRC.

Hii maana yake ni kwamba mkakati mwingine wa Tshisekedi ni kutafuta namna ya kushawishi baadhi ya wabunge walioko ndani ya FCC ili kupunguza idadi yao ndani ya Bunge.

Tangu alipoingia madarakani, mkakati wa Tshisekedi dhidi ya Kabila umekuwa ni kuepuka mapambano ya moja kwa moja na mtangulizi wake huyo na badala yake amekuwa akiendesha chinichini pasipo kupiga kelele hadharani.

Kama atafanikiwa kuwa na wingi wa wabunge bungeni – kwa mbinu yoyote atakayotumia, Tshisekedi ataendelea kuongoza taifa hilo hadi mwaka 2023 ambako uchaguzi mwingine umepangwa kufanyika. Kama atashindwa kufanywa hivyo, atakuwa hana ujanja zaidi ya kuitisha uchaguzi mwingine.

Katiba ya DRC inampa Rais siku 30 kwa ajili ya kupambana kuongeza wabunge na tayari Tshisekedi ametangaza kumteua “Informateur” – yaani mtu ambaye kisheria kazi yake itakuwa ni kuongoza zoezi la kutongoza wabunge wa vyama vingine kuingia katika uhusiano na serikali iliyo madarakani ili kuendelea kubaki.

Kama Informateur atashindwa kushawishi wabunge wajiunge na CACH kutengeneza muungano mpya wa kuunda serikali, itabidi Tshisekedi aandike barua kwa Tume ya Uchaguzi ya DCR (CENI) kuitaka iitishe uchaguzi mwingine katika kipindi cha siku 60 tangu kuandikwa kwa barua hiyo.

Mmoja wa wapambe mashuhuri wa Kabila ambaye pia ni Waziri wa Mazingira na Maendeleo Endelevu katika Serikali ya Rais Tshisekedi, Claude Nyamugabo, tayari amezungumza hadharani kuwa suala la rais huyo mstaafu kuwania tena kutaka kurejea madarakani si “michapo tu ya mtaani, bali ni suala la hakika na tayari tunalifanyia kazi ili lifanikiwe”.

Baada ya ukimya wa muda mrefu katika siasa za hadharani, Kabila alijitokeza katika Bunge la nchi hiyo Septemba 15 – katika tukio lililoendeshwa kwa usiri mkubwa lakini kutangazwa sana siku lilipotokea. Ingawa alipewa hadhi ya Seneta wa Maisha wa Bunge la DRC, Kabila alikuwa hajawahi kuingia humo tangu aondoke madarakani.

Wachunguzi wa masuala ya kisiasa wa DRC waliona hatua hiyo ikiwa na lengo kutangaza kwamba bado yupo katika ulingo wa siasa za taifa hilo lakini pia kutaka kusimika ngome yake ndani ya mhimili huo wa dola.

Katika wiki zilizofuatia tukio hilo, Kabila pia amekutana na wanasiasa wengine mashuhuri nchini humo akiwamo aliyewahi kuwa Spika wa Bunge la DRC, Leon Kengo wa Dondo, katika mkutano ambao haukufanywa siri kwa lengo la kuonyesha mawanda ya ushawishi wa kisiasa wa mtoto huyo wa Rais wa zamani wa nchi hiyo, Laurent Desire Kabila.

Aliyekuwa rais wa DRC Joseph Kabila

Wawili hawa ni watoto wa wanasiasa mashuhuri wa taifa hilo waliokuwa vinara wa kupinga utawala wa dikteta Mobutu Sseseko – kila mmoja kwa namna yake. Baba wa Kabila, Laurent, aliamini katika matumizi ya nguvu za kijeshi lakini mzazi wa Felix, Etienne, aliamini katika mapambano ya kutumia sanduku la kura.

Kwa sababu ya upinzani huo wa wazazi wao, vijana hawa wametumia sehemu kubwa ya maisha yao ya ujana nje ya nchi yao; Felix akiishi zaidi Ubelgiji huku Joseph akiwa ameishi zaidi nchini Tanzania.

Kwa sababu hiyo, ingawa wote ni Wakongomani, Felix anazungumza lugha ya Kifaransa kwa ufasaha wakati Kabila akiwa anazungumza Kiswahili kwa ufasaha. Wakongamani wanazungumza lugha nne tofauti na zote hutokana zaidi na eneo analotaka mtu. Lugha hizo ni Kiswahili, Kikongomani, Kilingala na Kifaransa. Kuna lugha nyingine ndogo ndogo lakini kwa wastani Mkongomani wa kawaida atazungumza mojawapo ya lugha hizo nne.

Nini maana ya ujio wa akina Bemba?

Baadhi ya wapambe wa Kabila wameanza kuzungumza hadharani kwamba kulikuwa na makubaliano baina yake na Tshisekedi kwamba rais huyo wa sasa ataongoza kwa muhula mmoja tu na kisha kumwachia Joseph katika uchaguzi ujao wa mwaka 2023.

Kuvunjika kwa muungano wa CACH na FCC kunamaanisha kwamba makubaliano haya – kama yalikuwepo, hayatakuwa na maana tena. Lakini kuna picha nyingine kubwa zaidi katika sakata hili.

Sababu mojawapo iliyomfanya Kabila amuunge mkono Tshisekedi ilikuwa kwamba hakuwa akiamini usalama wake binafsi na familia yake endapo Fayulu – aliyekuwa akiungwa mkono na akina Katumbi, angeshinda katika uchaguzi ule.

Familia ya Kabila inadaiwa kumiliki ukwasi mkubwa ndani ya taifa hilo na suala la uhakika wa usalama wa uhai na mali zao ni la muhimu linapokuja jambo la nani atafaa kuwa rais wa taifa hilo tajiri kwa rasilimali.

Akina Katumbi waliwahi kukimbia nchi wakati wa utawala wa Kabila na pasi na shaka rais huyo za zamani na watu wake wana wasiwasi kuwa endapo ushirikiano wa aina yoyote unaowahusisha mahasimu wake hao wa zamani, utafanikiwa kuingia madarakani, maisha yake na watu wake wa karibu yanaweza kubadilika.

Sehemu ya kwanza kuzuia hilo lisitokee ni bungeni na ndiyo sababu aliamua kufanya ziara ya kushtukiza katika chombo hicho miezi mitatu iliyopita.

Kama mmoja wa wapambe wa Kabila alivyonukuliwa katika mojawapo ya magazeti ya kimataifa akisema; “Kabila anaamini mwaka 2023 utafika haraka sana”.

Kwa sasa, kazi iko kwa Tshisekedi.

Source link

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *