img

Waliotafuna fedha za Babati Saccos Wajiuzulu baada ya kukaliwa kooni na TAKUKURU

December 7, 2020

Na  John Walter, Manyara 

Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoani Manyara Holler Majungu amesema  wamefanikiw kurejesha shilingi milioni 19 za Babati SACCOS huku waajiriwa waliokula njama za kujichukulia fedha hizo wakijiuzulu. 

Akizungumza Leo Desemba 7,2020 Makungu amesema Agosti 12 mwaka huu, walitangaza kuanza msako mkali wa wanachama wa Babati SACCOS waliokosa uungwana wa kujisalimisha wenyewe baada ya kutakiwa kufanya hivyo Agosti 7 mwaka huu. 

Amesema katika kushughulikia suala la Babati SACCOS walibaini kuwa kulikuwa na makubaliano ya kihalifu kinyume cha kifungu cha 306 cha kanuni ya adhabu kati ya baadhi ya waajiriwa na wanachama wasio waadilifu. Amesema fedha hizo zilichukuliwa kwa nia ovu ya kutorejeshwa ili kudhulumu amana za wanachama waadilifu. 

“Baada ya uchunguzi wa TAKUKURU Mkoa wa Manyara kuingilia kati suala hili, waajiriwa waliohusika wamewajibika kwa kujiuzulu nafasi zao na baada ya kujiuzulu nafasi hizo watumishi hao tumerejesha kwa uongozi mpya shilingi milioni 19,” amesema Makungu. 

Amesema utaratibu wa mkopo katika SACCOS zote ni kuwa mkopo huo ni lazima uidhinishwe na wawakilishi wa wanachama wote ambao ni kamati ya mipango na bodi na kamati ya mkopo pia hutakiwa kujiridhisha na uwepo wa utoaji wa fedha hizo. 

Amesema kwenye suala la Babati SACCOS kamati ya mikopo ambayo ndiyo wamiliki wa mali kwa niaba ya wanachama hawakushirikishwa wakati wa utoaji wa fedha hizo. 

“Wanachama wachache wasio waadilifu, ndani ya Babati SACCOS waliamua kula njama za kuwaibia wenzao kwa nia ya kutorejesha fedha hizo hadi Mrajisi msaidizi wa ushirika Mkoani Manyara Venance Msafiri alipolalamikiwa na wanachama waaminifu naye akatoa taarifa TAKUKURU kwani kuna waliokaa na fedha hizo kwa zaidi ya miaka 10,” amesema. 

Amesema kuchukua mali inayoweza kuibiwa bila kibali cha mwenye mali au aliyepewa kusimamia mali hiyo pasipo na nia ya kurejesha hutafsiriwa kuwa ni wizi kwa maana ya kifungu cha 258 na adhabu yake chini ya kifungu cha 265 kanuni ya adhabu ni kifungo cha miaka saba jela.

 Urejejeshwaji wa fedha hizi ulikuwa na changamoto kwa kuwa hakuna kumbukumbu za dhamana ya mikopo hiyo iliyokuwa imewekwa hivyo ni imani yake viongozi wapya wa Babati SACCOS watazingatia kanuni za ukopeshaji kwa fedha ambazo TAKUKURU imewarejeshea na tatizo lililokuwepo halitajirudia tena. 

“Kwa wale ambao bado wanajificha milango bado ipo wazi wafike TAKUKURU warejeshe madeni yao kwa hiyari kama walivyofanya wenzao,” amesema Makungu. Amewakumbusha wadaiwa wote kuwa kutotii wito huo wa TAKUKURU ni makosa na watakapokamatwa na watashtakiwa kwa wizi na kula njama kinyume cha kifungu cha 258, 265 na 306 ambapo adhabu yake wakipatikana na hatia Mahakamani ni kifungo cha miaka saba.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *