img

Upi mustakabali wa Zanzibar baada ya kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa?

December 7, 2020

Dakika 6 zilizopita

Maalim Seif

Maelezo ya picha,

Maalim Seif ameamua kurudi tena kuwa makamu, kwa sasa akiwa chini ya Dkt. Hussein Ali Mwinyi.

Haitakua mara ya kwanza kwa mkongwe wa siasa za Tanzania, Maalim Seif Sharif Hamad kuwa makamu wa kwanza wa Rais katika serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).

Kabla ya mtafaruku wa kisiasa baada ya kufutwa matokeo ya uchaguzi wa 2015, Maalim Seif akiwa Chama cha Wananchi (CUF) alihudumu katika nafasi hiyo kutoka 2010 hadi 2015. Wakati huo Dkt. Ali Mohammed Shein wa Chama cha Mapinduzi (CCM) akiwa Rais.

Maalim ameamua kurudi tena kuwa makamu, kwa sasa akiwa chini ya Dkt. Hussein Ali Mwinyi. Swali linaloulizwa na wengi, kipi kikubwa anakwenda kuinufaisha upinzani kwa kuwa sehemu ya serikali?

Dkt. Mwinyi ameshusha tanga la safari ya kuiongoza Zanzibar chini ya muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK). Ni punde tu tangu taifa hilo lenye mamlaka ya ndani, kutoka katika uchaguzi uliogubikwa na mizengwe mingi.

Dkt Mwinyi

Ndoa hii mpya ya kisiasa itakuwa ndio mwanzo wa enzi mpya ya siasa safi katika visiwa vya Zanzibar? Viongozi hao watashirikiana vyema kwa maslahi ya Zanzibar, ama ni ndoa ya kuogopana na kutoaminiana?

Miaka mitano sio mingi kusubiri jawabu ya maswali hayo.

Historia ya Umoja wa Kitaifa

Siasa za Zanzibar daima ziko moto. Hata kabla ya Mapinduzi ya 1964 zilikuwa za ushindani mkubwa. Baada ya kurudishwa kwa mfumo wa vyama vingi 1992 ushindani wa kisiasa ukarudi kama awali.

Kwa mujibu wa ripoti ya Human Rights Watch, maandamano ya Januari 2001 yaliondoka na roho za waandamanaji 35 katika kisiwa cha Pemba. Wafuasi wa chama kikuu cha upinzani kwa wakati huo, CUF waliingia barabarani kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2000.

Vikosi vya usalama vya Tanzania vikiongozwa na Jeshi la Polisi viliyazima maandamano hayo kwa risasi za moto na kupelekea vifo, majeruhi na wakimbizi.

Hata kabla ya vurugu hizo, siasa za Zanzibar zilikuwa zimeshawaacha watu na makovu.

Kuna ambao walifukuzwa kazi kisiasa, wapo wanafunzi waliofukuzwa shule. Pia kulikuwa na vitendo vya kibaguzi.

Kadhia hizo zilitokana na aina ya siasa zilizokuwepo.

Tume ya Uchaguzi Zanzibar ilifuta matokeo ya uchaguzi mwaka 2015

Maelezo ya picha,

Tume ya Uchaguzi Zanzibar ilifuta matokeo ya uchaguzi mwaka 2015

Ndipo ikaundwa kamati ya maridhiano chini ya Mwenyekiti, marehemu Hassan Nassor Moyo. Ikiwa na wajumbe kutoka CCM na CUF, ilikaa kitako kwa ajili ya kuyapatia muafaka mizozo ya kisiasa inayoikumba visiwa hivyo vya bahari ya Hindi.

Moja ya jambo kubwa lililoafikiwa ni kuwepo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK). Lengo kuu ni kuileta pamoja Zanzibar iliyogawika na kuiondoa katika mkwamo wa muda mrefu uliokuwepo.

Serikali ya muundo huo ilipigiwa kura ya maoni na Wazanzibari wenyewe, ikapita kwa wingi wa kura kwa zaidi ya asilimia 60. Kwa mara ya kwanza baada ya uchaguzi wa 2010 SUK ilianza kufanya kazi.

Ilisaidia pakubwa uchaguzi wa mwaka huo kufanyika kwa amani bila fujo lolote. Wafuasi wa CUF na CCM waliingia pamoja barabarani kufurahia ushindi. Ushindi ulikuwa wa Wazanzibari wote.

Ni upi umuhimu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa utawala?

Baadhi ya wadadisi wa mambo wanaamini Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964, yangeweza kuepukikia ikiwa Chama cha Zanzibar Nationalist Party (ZNP) na kiongozi wake Ali Muhsin wangeikubali rai ya kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa na chama cha Afro-Shirazi Party baada ya uchaguzi wa 1963.

Mapinduzi yalikuja katika nyakati ambazo Zanzibar haikuwa na utulivu wa kisiasa. Chinjachinja waliokosa huruma waliziteketeza roho za mamia ya raia wa kawaida. Wengi wa raia hao waliponzwa na rangi ya ngozi, asili zao na misimamo yao ya kisiasa.

Katika mazingira ya sasa ya siasa za Zanzibar, muundo huu wa serikali utasaidia pakubwa utawala wa Dkt. Hussein Mwinyi kuiongoza nchi hiyo ikiwa katika mshikamano wa kijamii na utulivu wa kisiasa.

Zanzibar ina historia ya mparaganyiko katika jamii yake kila baada ya uchaguzi kuisha. Uhasama, ubaguzi, kukosekana maelewano huzuka kwa sababu ya matokeo ya kisiasa ambayo huliacha kundi kubwa katika nchi likiwa halijaridhika na kilichotokea.

Kwanini upinzani umejiunga na Serikali ya Umoja wa Kitaifa?

Chama kipya cha upinzani Zanzibar, ACT Wazalendo hakikuridhika na namna uchaguzi ulivyo kwenda. Chama hakikuyakubali matokeo ya Ubunge na Uwakilishi, wala tangazo la ushindi lililotolewa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), kumtangaza Dkt Mwinyi kuwa Rais.

Kuonesha kuwa uchaguzi huo haukuwa huru na haki, chama hicho kilitoa ripoti yenye orodha ya majina ya watu wanaoelezwa kuuwawa na kujeruhiwa na vikosi vya usalama wakati wa uchaguzi.

Mkusanyiko wa mambo hayo yote, unazusha swali; kwa nini chama hicho kimekubali kujiunga na serikali ambayo wanaamini haipo madarakani kihalali?

ACT Wazalendo itakuwa na kazi kubwa ya kuwaeleza sababu ya maana ya kwa nini Maalim Seif amekuwa makamu wa kwanza wa Rais. Kuna faida gani ama maslahi gani ya kisiasa chama hicho itayapata?

Wapo wanaoamini, upinzani utakuwa na nafasi nzuri zaidi kisiasa ya kujiandaa kwa uchaguzi wa 2025 wakiwa ndani ya SMZ kuliko wakiwa nje.

Je, uamuzi wao utaweza kuleta suluhu kwa matatizo yaliyowakumba wafuasi wao wakati wa uchaguzi mkuu?

Je, upinzani utaweza kushinikiza mageuzi katika mfumo wa uchaguzi kwa faida ya uchaguzi ujao?

ACT Wazalendo haijaweka wazi ikiwa iliweka masharti au kuna makubaliano yoyote wamekubaliana na utawala wa Dkt. Mwinyi kabla ya kukubali kuwa sehemu ya serikali yake.

Kwa maana hiyo, sababu zipi hasa zimewasukuma upinzani kukubali kuwa sehemu ya serikali ya Dkt. Mwinyi baada ya kukataa ushindi wake na ushindi wa nafasi nyengine za wagombea, zinabaki kuwa kitendawili kinachosubiri jawabu.

Source link

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *