img

Mwakamo ataka Waandishi watumike kutangaza kazi za Magufuli

December 7, 2020

Na Omary Mngindo, Mlandizi

MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Vijijini Mkoa wa Pwani Michael Mwakamo, amewataka Wakuu wa Idara kuwatumia Waandishi wa Habari kutangaza kazi nzuri inayofanywa na Rais Dkt. John Magufuli jimboni humo.

Mwakamo ametoa rai hiyo mwishoni mwa wiki akizungumza na Wakuu hao akiwemo Mkurugenzi Mtendaji Butamo Ndalahwa, ambapo alisema serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli imefanya mambo mengi makubwa katika sekta mbalimbali.

“Serikali yetu chini ya Rais Dkt. John Magufuli imeendelea kufanya mambo mengi makubwa, lakini cha kushangaza hayatangazwi hivyo wa-Tanzania kushindwa kutambua mazuri yanayotekelezwa na serikali yao, tuwatumie Waandishi,” alisema Mwakamo.

Alisema kuwa chini ya Rais Magufuli kuna miradi ikiwemo Ujenzi wa Bandari Kavu Kwala, Reli ya Mwendokasi inayopita jimboni humo, ukarabati wa shule ya Sekondari ya Wasichana ya Ruvu, ujenzi wa Hospitali ya wilaya, ukarabati wa Kituo cha afya Mlandizi na mingine mingi.

“Pia kuna viwanda vilivyojengwa ndani ya jimbo letu, yote yamepatikana ndani ya utawala wa awamu ya Tano chini ya Dkt. Mahufili, hayo na mengine mengi ambayo sikuyataja yanatakiwa kuandikwa, tuwatumie Waandishi,” alisema Mwakamo.

Aliongeza kuwa Waandishi wanafanya kazi kubwa, huku akishangazwa kuona mikoa mbalimbali mambo yao yanasikika lakini yanayofanyika Kibaha Vijijini jirani kabisa na Dar es Salaam yanayofanyika hayasikiki kabisa.

“Hivi Mganga Mkuu ukiwa na kazi ukishirikisha Waandishi japo wawili takuwa dhambi? kama mlikuwa na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wenu nitachukua jukumu hilo, nitahakikisha Waandishi wanaandika kazi nzuri ya Magufuli, pia nitawafungulia ofisi hapa Mlandizi,” alisema Mwakamo.

Akizungumza baada ya Mbunge huyo, Ndalahwa alisema kuwa changamoto zilizopo zinaendelea kufanyiwa kazi, na kwamba pamoja na hayo watayafanyiakazi yote aliyoyaelezea Mwakamo huku akimuondoa hofu kuhusu masuala hayo.

“Mengi umeyazungumza nami nikuhakikishie kwamba Mimi kwa kushirikiana na Wakuu hawa wa Idara tutayafanyiakazi yote, kuhusu sekta ya afya vitambulisho vya wazee na sekta ya elimu vyote tunakwenda kuyafanyiakazi,” alisema Ndalahwa.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *