img

Wananchi wasaka maji usiku wa manane wilayani Rombo

December 6, 2020

Wananchi wa Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji hali inayowasababishia kukesha mtoni usiku kwa zaidi ya saa tisa wakigombania maji ambayo hata hivyo sio safi na salama kwa matumizi ya binadamu.

Wakizungumza na Mwananchi jana wananchi hao walisema kuwa kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliana na changamoto ya maji hasa wakati wa kiangazi.

Siku zote wananchi hao wamekuwa wakitegemea maji ya kwenye mito ambayo pia wanaeleza hulazimika kutembea umbali mrefu kwenda kuyasaka.

Hapiness Vitalisi, mkazi wa Tarake alisema kuwa wakati wa kiangazi wanalazimika kugombania maji na wakati mwingine wanakesha mtoni kwa zaidi ya saa tisa kwa ajili ya kuchota maji jambo ambalo wameiomba Serikali iwasaidie angalau wapate unafuu wa maji.

“Upatikanaji wa maji katika wilaya ya Rombo imekuwa ni changamoto kubwa na ya muda mrefu. Sisi wanawake wa Rombo tuna changamoto kubwa ya maji, wakati mwingine hasa kipindi cha kiangazi tunakaa mtoni tukigombania maji hadi saa nane au saa tisa usiku, tunaomba Serikali itusaidie tunateseka mno,”alisema Hapiness

Jesca Mrosso, mkazi wa Tarakea aliiomba Serikali kuwatazama kwa jicho la pili, kwani wanapitia changamoto kubwa ya maji na kusema kuwa wanaamini mbunge wa jimbo hilo kwa kushirikiana na viongozi wa Serikali wataenda kuwatetea na kupata maji ya uhakika.

“Tunaomba Serikali itusaidie angalau tupate unafuu wa maji maana sisi kina mama tunapitia changamoto kubwa na tunateseka. Tumekuwa ni watu wa kunywa maji ya mtoni na wakati mwingine haya maji tunayotumia yanatuletea maradhi ya tumbo, kwani sio salama”alisema.

Kauli ya mbunge

Kutokana na kilio hicho, mbunge mteule wa jimbo hilo, Profesa Adolf Mkenda alilazimika kwenda kugagua maeneo yenye vyanzo vya maji katika msitu wa Rongai uliopo tarafa ya Tarakea kuangalia namna wananchi wa wilaya hiyo watakavyooondokana na changamoto hiyo ya maji.

Alisema kuwa mwaka jana Serikali ilitenga bajeti ya mradi wa maji wa Ziwa Challa kiasi cha Sh36.9 bilioni ili kumaliza changamoto ya maji katika wilaya hiyo, lakini mpaka sasa hakuna fedha yoyote ambayo imetolewa kwa ajili ya kutekeleza mradi huo.

Profesa Mkenda alisema kuwa endapo mradi huo wa maji ukikamlika vijiji 41 kati ya 66 wilayani humo vitanufaika na maji hiyo ambapo alisema changamoto ya maji wilayani humo itakuwa historia.

“Kwenye ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi ahadi ipo ya kupambana na changamoto ya maji wilaya ya Rombo na mwaka 2019 bajeti ilitengwa kiasi cha Sh36.9 bilioni kwa ajili ya mradi wa maji wa ziwa Challa ambao una vyanzo vingi vya maji. Tuna matumaini makubwa na Serikali yetu kwamba fedha hizo zitaanza kutolewa na tutaanza kuiona miradi hii ikienda kwa kasi,”alisema.

Aliongeza: “Tuna matumaini makubwa sana kwamba Rombo tutasalimika na hii adha ya maji; naona kuna mwanga mkubwa sana chini ya uongozi makini wa Rais Magufuli na maono yake na bidii zake. Naamini hili suala la Rombo kutopata maji wakati tuna vyanzo vingi vya kutosha litaisha.’’

Hata hivyo, Profesa Mkenda alisema kuwa licha ya wilaya hiyo kuwa na vyanzo vingi vya maji, vyanzo hivyo vinanufaisha nchi jirani.

Alisema tatizo sio maji hayo kunufaisha wananchi wa nchi jirani, lakini kuna haja ya kujua namna mikataba ya kutumia vyanzo hivyo ilivyo.

Alieleza kuwa kwa sasa kuna jumla ya vyanzo 11 vya maji ambavyo vyote vinapeleka maji kwa wananchi wa nchi jirani.

“Wanasema mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe, lakini sisi kama hatujipendi hatuchukui maji yetu na tukagawa kwa wananchi wa Rombo sisi inakuwaje tunakuwa na upendo mkubwa zaidi wa namna hii wakati sisi bado tunapata changamoto ya maji,”alihoji Profesa Mkenda.

Aliongeza: “Hatuna ugomvi maji kwenda kwa wenzetu lakini tunahitaji Warombo wapate maji haya na wanufaike nayo kwanza. Huwezi kumpenda jirani yako wakati wewe kwanza haujajipenda, tutakuwa watu wa ajabu sana kwamba haya maji tunayaacha yanavuka mpaka halafu wananchi wetu wanapata shida ya maji,”

“Naiomba Wizara ya maji iharakishe mradi huu wa ziwa Challa ambao vyanzo vyake vya maji ni vingi. Mradi huu ulitengewa na ulikubaliwa kutolewa Sh36.9 bilioni, ninaomba fedha hizi zianze kutoka maana mpaka sasa haijatoka hata senti moja tangu bajeti ya serikali ya mwaka jana itenge fedha hizi ,”alisema Profesa Mkenda

Akizungumza kwa niaba ya Meneja Mkuu wa Kampuni ya watumia maji wilaya ya Rombo (Kiliwater), mhandisi Martin Kinabo alisema kuwa upo mradi wa maji wa Njoro II ambao ni utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji Ziwa Challa.

Alisema ni mradi ambao umeanza kutekelezwa na Serikali katika halmashauri ya Rombo ili kukabiliana na upungufu wa maji wakati wa kiangazi.

“Mradi huu ambao utakuwa na vyanzo vinne vya maji utazalisha mita za ujazo 1,728 kwa siku ambazo zinaweza kuhudumia wananchi wapatao 24,686 na utapunguza upungufu wa maji kwa asimia 13 wakati wa mvua na asilimia 6.4 wakati wa kiangazi,’’aliuelezea mradi huo.

Aliongeza kusema kuwa mpaka sasa zaidi ya Sh220 milioni zimetumika.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *