img

Uingereza yakamilisha maandalizi utoaji chanjo ya COVID-19

December 6, 2020

 

Chanjo ya kinga dhidi ya virusi vya corona ambayo imetengenezwa na kampuni ya kimarekani ya Pfizer na ile ya kijerumani ya BioNTech hivi sasa inasambazwa katika hospitali tofauti nchini Uingereza.

Hatua hiyo inatekelezwa siku mbili kabla ya kuanza  kile kinachotajwa kuwa programu kubwa kabisa ya utoaji chanjo nchini humo.

Kiasi cha dozi 800,000 za chanjo zinatarajiwa kuwa kila mahali, kabla ya kuanza utekelezaji wa utoaji wa chanjo hizo hapo Jumanne.

Malkia Elizabeth wa II wa Uingereza atapatiwa chanjo ya virusi vya corona katika muda wa wiki chache zijazo wakati mpango huo mpana utakapoanza.

Malkia huyo mwenye umri wa miaka 94, na mumewe Phillip, mwenye miaka 99, wamo kwenye orodha ya kupatiwa chanjo mapema kutokana na umri wao lakini hawatopatiwa kipaumbele dhidi ya watu wengine.

Hayo ni kulingana na magazeti kadhaa ya Uingereza ambayo yameripoti habari hizo leo Jumapili.

Chanjo kwa malkia Elizabeth itahimiza wengine kushiriki

Viongozi hao wakuu wa falme ya Uingereza wataweka hadharani taarifa za kupokea chanjo hiyo kama “hatua yenye nguvu dhidi ya vuguvgu la kupinga utolewaji wa chanjo”, limeripoti gazeti la Sunday Times.

Gazeti la The Mail limesema Malkia na mumewe wanatumai hatua hiyo “itawahimiza watu wengi zaidi kupatiwa chanjo”.

Katika kipindi cha janga la virusi vya corona Malkia Elizabeth ametumia muda mwingi kwa kujitenga kwenye kasri la Windsor kutokana na umri wake, na mwaka huu hatojumuika katika matukio ya familia ya msimu wa Krimasi ambayo kitamaduni hufanyika kwenye kasri la Sandringham  mashariki ya Uingereza.

Jumatano iliyopita Uingereza ilikuwa nchi ya kwanza duniani kuidhinisha chanjo ya Pfizer-BioNTech na maafisa wa afya tayari wameorodhesha sifa na vigezo vya umri na hatari ya kupata maambukizi kwa watu watakaopatiwa kwanza chanjo hiyo.

Uingereza imeagiza dozi milioni 40 za chanjo ya Pfizer-BioNTech  na inatarajiwa kupokea shehena ya kwanza ya dozi 800,000 wakati wa kuanza kutolewa chanji siku ya Jumanne.

Nchini Ujerumani na Urusi hali ya maambukizi bado inatia wasiwasi 

Wakati hayo yakijiri idadi ya maambukizi ya virusi vya corona nchini Ujerumani leo imeongezeka kwa visa 17,767  na kufanya idadi jumla ya maambukizi nchini humo kufikia visa 1,171,323.

Takwimu hizi ni kwa mujibu wa taasisi ya magonjwa ya kuambukiza ya Ujerumani ya Robert Koch. Ripoti ya taasisi hiyo kadhalika inaonesha watu 255 wamekufa katika muda wa saa 24zilizopita na kufanya idadi ya waliopoteza maisha nchini Ujerumani kutokana na janga hilo kufikia watu 18,772.

Nchini Urusi kumerekodiwa idadi mpya kubwa ya maambukizi 29,039. Idadi hiyo inafanya jumla ya maambukizi kufikia  2,460,770  tangu kuzuka kwa janga hilo na kwamba kuna rekodi mpya ya vifo 457 ndani ya saa 24, na kufanya idadi jumla sasa kufikia 43,141.

Pakistan yazidiwa na idadi kubwa ya wagonjwa wa COVID-19 

Kwengineko idadi ya maambukizi ya virusi vya corona nchini Pakistan imefikia kiwango kibaya na hospitali za nchi hiyo zinakabiliana na kiwango kikubwa cha wagonjwa wa COVID-19 katika wimbi la pili la maradhi hayo.

Katibu mkuu wa jumuiya ya madaktari nchini Pakistan Sajjd Qasier amesema maafisa wa afya wanapitia kipindi kigumu inayozidishwa makali na maambukizi mapya ya kila siku.

Qasier amesema hospitali zimejaa wagonjwa mahututi wa Covid-19 na mgonjwa mpya anaweza kupata kitanda iwapo ni mwenye bahati au mgonjwa mwingine ameruhusiwa kutoka hospitali.

Kiasi wagonjwa saba walifariki dunia jana usiku kwenye hosptiali ya umma mjini Peshawar waakti hospitali ilipoishiwa gesi ya oksijeni kuwasaidia kupumua.

Idadi ya visa vipya inapindukia 3000 kwa siku katikia nchi hiyo yenye maambukizi 416,499 na vifo  8,361 vilivyosabababishwa na Covid-19.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *