img

Fahamu kuhusu saratani ya shingo ya kizazi

December 6, 2020

Ugonjwa huu husababishwa na virusi vinavyoitwa Human papilloma, ambapo mtu anaweza kupatwa na virusi hawa wakati wa kujamiana na mtu mwenye maambukizi. Human Papillomavirus aina ya 16 na 18 husababisha kansa ya aina hii kwa asilimia 75 duniani kote huku aina ya 31 na 35 zikisababisha maambukizi kwa asilimia 10.

Watu walio katika hatari ya maambukizi ya ugonjwa huu ni kwa ujumla wanawake wote lakini zaidi wale wasiokwenda kufanyiwa uchunguzi wa kila mwaka kuhusiana na ugonjwa huu unaojulikana kitaalamu kama pap smear, wanawake walioathirika na virusi vya human papillomavirus HPV au genital warts, wanaovuta sigara, wenye ukimwi na wasiokula vyakula bora hasa wasiozingatia mboga na matunda katika lishe zao.

Kutokana na uchunguzi huo, timu ya wataalamu wa ugonjwa huo imeeleza sababu zinazochangia kupata saratani ya shingo ya kizazi na kubainisha dalili ambazo huonekana kwa mtu ambaye anasumbuliwa na ugonjwa huo.

Kimsingi mabadiliko ya awali ya saratani hii hayatoi dalili yoyote ya moja kwa moja hadi mwanamke afanyiwe uchunguzi au vipimo vingine vya ugonjwa huo. Dalili zinazoonesha kuwepo kwa saratani ya shingo ya kizazi ni pamoja na kutokwa na damu ambayo si ya hedhi, kutokwa na uchafu, majimaji au usaha sehemu za siri.

Hata hivyo dalili nyingine ni pamoja na kuhisi maumivu makali wakati wa kujamiiana na kusababisha kutokwa na damu baada ya tendo hilo ambapo pia ni pamoja na maumivu ya tumbo chini ya kitovu sambamba na maumivu ya kiuno.

Kufanyiwa uchunguzi wa pap smear ili kubaini ugonjwa huu kuna nafasi kubwa katika kuzuia watu kupatwa na saratani ya shingo ya kizazi. Uchunguzi wa awali wa saratani ya shingo ya kizazi unatakiwa kufanyiwa wanawake walio katika mahusiano ya ndoa na pia wanatakiwa kupima mara kwa mara hadi wanapofikia umri wa miaka 69.

Mwanzoni uchunguzi huu unatakiwa ufanyike mara kwa mara kwa muda wa miaka mitatu mfululizo. Ikitokea katika miaka mitatu mfululizo uchunguzi huo haujatoa dalili zozote za kuwepo saratani basi mwanamke anaweza kuendelea kufanyiwa uchunguzi mara moja kila baada ya miaka miwili na mitatu hadi pale atakapofikisha umri wa miaka 69.
,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *