img

ACT Wazalendo yakubali kushiriki kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, yajipanga kupendekeza jina la makamu wa kwanza wa rais

December 6, 2020

Chama cha ACT-Wazalendo kimetangaza kuridhia Chama kushiriki kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar na imeielekeza Kamati ya Uongozi kupendekeza jina la mwanachama atakayekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.

Msimamo huo umetangazwa na Katibu Mkuu wa Chama hicho Ado Shaibu wakati akizungumza na vyombo vya habari, leo Disemba 6, 2020 ambapo amesema kuwa baada ya jana kikao cha Kamati Kuu kukaa waliamua hayo kwa faida ya taifa pamoja na chama.

Amesema kuwa kikao hicho pamoja na mambo mengine, Kamati Kuu ilipokea taarifa ya maoni ya wanachama juu ya hali ya siasa nchini hususani Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwezi Oktoba, 2020 Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

“Jana tarehe 05 Disemba, 2020 Kamati Kuu ya Chama cha ACT Wazalendo ilikutana katika kikao chake maalum, ikiwa na lengo la kujadili na kufikia maamuzi juu ya masuala kadhaa yanayohusu mustakabali wa Taifa na Chama chetu”, amesema Ado.

Ameongeza kuwa, “Kamati Kuu imeridhia Chama kushiriki kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar na imeielekeza Kamati ya Uongozi kupendekeza jina la mwanachama atakayekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar”.

Novemba 19, 2020, Ikulu ya Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Serikali ya Mapinduzi Dkt Hussein Mwinyi, alitangaza baraza la Mawaziri katika serikali yake huku akiacha kutangaza majina ya Mawaziri katika Wizara mbili ambazo zinatakiwa kujazwa na chama cha ACT-Wazalendo.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *