img

UN yaitaka Belarus kuachilia huru waandamanaji

December 5, 2020

Umoja wa Mataifa (UN) umetoa wito wa kuachiliwa huru kwa watu waliowekwa kizuizini kinyume cha sheria nchini Belarus.

Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet, alizungumza katika kikao maalum kilichofanyika kwenye Baraza la Haki za Kibnadamu juu ya hali ya Belarus.

“Imeripotiwa kuwa zaidi ya watu 27,000 wamewekwa kizuizini tangu tarehe 9 Agosti. Mamia ya watu wanaendelea kuzuiliwa kila wiki wakati wa maandamano yaliyoanza mwezi uliopita. Karibia watu 1000 mnamo 8 Novemba na 700 mnamo Novemba 15 wamezuiwa.”

Bachelet pia alisema kuwa kulikuwa na madai ya majeruhi wakati polisi walipokuwa wakiwatawanya waandamanaji.

Akisisitiza kuwa madai yaliyotolewa ya wafungwa “kuteswa, kutendewa unyama na kudhalilishwa” yaliwatia wasiwasi, Bachelet alibainisha kupokea malalamiko zaidi ya 2,000 yalitolewa kuhusiana na suala hili hadi mwisho wa Oktoba.

Bachelet alisema kuwa waandishi wa habari 373 wamewekwa kizuizini tangu Agosti, waandishi wa habari 6 kwa sasa wako kizuizini na watatu kati yao wanakabiliwa na vifungo vya gerezani.

Akihimiza serikali ya Belarus kuwa lazima imalize haraka ukiukaji wa haki za kibinadamu unaoendelea, Bachelet pia alitoa wito wa kuachiliwa huru kwa watu wote waliokamatwa kiholela na kuwekwa kizuizini kinyume cha sheria.

Rais wa serikali ya sasa Alexander Lukashenko, alishinda uchaguzi wa urais uliofanyika nchini Belarus Agosti 9, ambapo baadaye maandamano yakaanzishwa kwa madai ya kuwa “uchaguzi ulikumbwa na visa vya wizi.”

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *