img

Uchaguzi Uganda 2021:Bobi Wine ni nani na nguvu yake nini?

December 4, 2020

Dakika 2 zilizopita

Bobi

Nilimuona Bobi Wine ambaye jina lake asili ni Robert Kyagulanyi Ssentamu kwa mara ya kwanza mnamo mwaka 2008.

Nilikuwa nafanya kazi nchini Uganda na ndiyo kwanza wimbo wake maarufu wa ‘Kiwani’ ulikuwa unatamba. Marafiki zangu waandishi wa habari walikuwa wamekwenda kumwona katika ofisi zake zilizokuwa katika eneo la Kamwokya Kaskazini Mashariki mwa mji mkuu wa Uganda, Kampala, nami nilijiunga katika msafara huo kwa lengo la walau kumtia machoni.

Wakati huo, hakukuwa na aliyekuwa na mawazo kwamba mbunge huyu wa sasa Jimbo la Kyadondo Mashariki, angekuja kuwa mwanasiasa mashuhuri achilia mbali mshindani namba moja wa Rais Yoweri Museveni na chama chake cha NRM katika Uchaguzi Mkuu wa Januari mwakani.

Wakati huo, miaka 12 iliyopita, Bobi alikuwa akijulikana kwa kuimba nyimbo zinazoeleza maisha ya watu masikini – yeye mwenyewe akiwa amezaliwa na kukulia katika mazingira ya kimasikini huko huko Kamwokya, na hilo ndilo jambo lililompa umaarufu mkubwa miongoni mwa wananchi wa taifa hilo ambao wengi wao ni masikini.

Nilipigwa na butwaa nilipoanza kusikia habari za Bobi Wine zikianza kupamba moto. Nikashangaa zaidi niliposikia amefanikiwa kuwa mbunge mwaka 2017; akiwa mgombea binafsi huku akiwabwaga wagombea wa vyama vikuu vya NRM na FDC vilivyokuwa na wagombea maarufu kwenye jimbo hilo.

Nini hasa kimemfanya mwanamuziki huyu mashuhuri aliyekuwa akisifika kwa kuimba nyimbo za kimapinduzi nakujiita ”Rais wa ghetto’ kubadilika na kuwa mshindani wa kipekee dhidi ya utawala wa takribani miongo minne wa NRM?

VBobi

Kijana, Mkristo na kutoka kabila la Baganda

Kwa mujibu wa mwandishi mashuhuri wa Uganda, Andrew Mwenda, Bobi Wine ana sifa tatu zinazomfanya kuwa mgombea wa aina yake dhidi ya Museveni.

Taifa la Uganda lina sifa kubwa tatu zenye mashiko kisiasa; lina wananchi wengi vijana, dini inayoongoza kwa watu wengi ni Wakristo wa madhehebu ya Wakatoliki na kabila lenye watu wengi zaidi ni la Baganda ambalo watu wake wanapatikana katikati ya taifa hilo.

Bobi Wine ni kijana mwenye umri wa miaka 38, anatoka katika kabila la Baganda na dini yake ni Mkristo wa madhehebu ya kikatoliki.

Katika maboksi hayo matatu muhimu, kijana huyu anatia alama ya tiki kote.

Katika miaka yote tangu serikali ya Rais Museveni ilipoamua kuruhusu mfumo wa vyama vingi, mshindani wake mkuu alikuwa ni Kizza Besigye wa chama cha FDC ambaye ingawa kiumri ni mdogo kwake; wana historia inayoshabihiana kisiasa.

Huwezi kusikiliza tena

Maelezo ya video,

Kura za vijana zinaweza kumpa ushindi Bobi Wine?

Suala la umri si dogo katika muktadha wa uchaguzi wa Uganda mwakani. Katika taifa lenye watu milioni 43 – kutokana na makadirio ya sense ya mwaka 2014 iliyoonyesha taifa hilo lina watu milioni 34.9, zaidi ya nusu ya watu wake wana umri chini ya miaka 40.

Kimsingi, kwa mujibu wa takwimu za Tume ya Uchaguzi ya Uganda, asilimia 80 ya wapiga kura wa taifa hilo katika uchaguzi huo wana umri wa kati ya miaka 18 hadi 40; umri ambao Bobi Wine anaangukia.

Ni asilimia 1.7 tu ya wapiga kura wa Uganda wana umri wa zaidi ya miaka 70. Takwimu hizo zinaonyesha pia kwamba watu wenye umri wa kuanzia miaka 50 na kuendelea – ambao angalau wameona mafanikio ya utawala wa Museveni katika maisha yao, wanafikia asilimia 13 ya wapiga kura wote.

Linapokuja suala kabila, lina maana kubwa pia kwa sababu ukiondoa idadi yao kubwa, Wine ni mtu aliye karibu na utawala wa kifalme wa kabila lake.

Kuna wakati alikuwa akijulikana kwa jina la Omubanda wa Kabaka (Mpambanaji wa Kabaka – yaani Mfalme wa watu wa kabila la Baganda).

Katika miaka yake 20 ya kwanza madarakani, Rais Museveni alikuwa akiungwa mkono kwa kiasi kikubwa na watu wa kabila hilo kwa sababu alipindua serikali iliyokuwa ikiongozwa na watu kutoka Kaskazini mwa Uganda ambao hawakuutendea kwa heshima utawala huo.

Baada ya miaka 35 ya madarakani, Ufalme na watu wa kabila hilo wanaweza kuwa sasa wanafikiri kuwa na mtu wao katika Ikulu ya Entebbe. Hii ni kete kubwa kwa Bobi.

Matumizi ya mitandao ya kijamii

Takwimu rasmi za Mamlaka ya Mawasiliano ya Uganda zinaonyesha kwamba taifa hilo sasa lina watu takribani milioni 20 wanaotumia mtandao wa intaneti.

Kwa sababu wengi wa watumiaji wa mitandao ni vijana na watu wa umri huo ndiyo wengi zaidi nchini humo, inadaiwa kwamba Bobi na chama chake cha NUP kinatawala dunia ya mitandao ya kijamii kwa asilimia takribani 80.

Kila anachofanya Bobi Wine katika siasa zake anahakikisha kuna namna kinawafikia wananchi wa Uganda kwa haraka.

Hii ndiyo namna aliweza kuwateka watu kwa kufanya kampeni za nyumba kwa nyumba mwaka 2017 ambapo alihakikisha picha mnato na video zinasambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii kwa faida yake.

Ingawa mwanasiasa kukubalika katika mitandao ya kijamii si kigezo pekee cha kumwezesha kushinda uchaguzi, lakini tofauti hii ya asilimia 20 kwa 80 ni kubwa kiasi kwamba inatakiwa iingie katika hesabu kali za uchaguzi.

Ujasiri

nn

Kwa sababu ya historia ya miaka ya nyuma ambako Waganda wamewahi kutawaliwa kijeshi na madikteta, wananchi wameanza kuamini kwa viongozi wanaoonekana ngangari na wanaoweza kuvumilia shubiri za kisiasa.

Kwa kujua kwamba Museveni anapenda kutumia mabavu katika siasa zake, Bobi amekuwa wakati mwingine akifanya matukio ya akichokozi dhidi ya vyombo vya dola, ili nguvu zisizo za kawaida zitumike dhidi yake na kumjengea huruma kwa wananchi.

Mojawapo ya vitendo ni kukutana na wafuasi wake katika mikusanyiko mikubwa ya watu ingawa serikali imeipiga marufuku kwa sababu ya ugonjwa wa Corona.

Source link

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *