img

Mwalimu auawa usiku na mtu asiyejulikana

December 4, 2020

Angelita Sudi (58), mwalimu wa Shule ya Msingi Olele wilayani Rombo ameuawa nyumbani kwake na watu wasiojulikana, alipotoka nje usiku kwenda msalani.

Mwalimu huyo ambaye pia alikuwa katibu wa Parokia ya Olele, aliuwawa usiku wa Novemba 30, nyumbani Kijiji cha Kilema.

Akisimulia ilivyokuwa, dada wa marehemu aliyekuwa akiishi naye, Febronia Sudi alisema usiku wa siku ya tukio marehemu alitoka nje kwenda msalani na akiwa huko akauliza kwa nini taa zimezimwa lakini kabla hajaenda kuangalia (dada mtu), alimsikia ndugu akilalamika kuchomwa kisu.

“Ilikuwa saa tatu usiku. Alikuwa anaenda nje lakini alipofungua mlango akakuta taa zimezimwa wakati zilikuwa zimewashwa. Ghafla nikasikia yowe, nilipotoka nje akaniambia kuna mtu amemchoma kisu kifuani na kukimbia. Alianguka chini,” alieleza dada huyo.

Alishindwa kumnyanyua ndugu yake pale chini hivyo, anasema alitoka kwenda kuomba msaada lakini walipofika wakakuta ameshafariki.

Akizungumzia tukio hilo, Paroko wa Parokia ya Olele, Sixtus Kesi alisema limeacha simanzi kwa kanisa na jamii kwa ujumla hivyo kuwataka wananchi wa Rombo kukemea uovu unaofanywa.

“Ni tukio lililoleta simanzi, kila anayefika pale analia. Matukio haya yanapangwa kwenye vituo vya gongo na bangi. Marehemu alikuwa katibu wa parokia, hakika ni msiba mzito saana. Tunamwomba Mungu huyo mwovu ajulikane na vyombo vya sheria vimchukulie hatua stahiki,” alisema Kesi.

Mtendaji wa Kata ya Olele, Isack Kivuyo alisema alipata taarifa kutoka kwa jirani hivyo akaenda eneo la tukio kuuchukua mwili kwa kushirikiana na askari polisi kuupeleka ukahifadhiwe Hospitali ya Huruma.

Kamanda wa polisi mkoani Kilimanjaro, Emmanuel Lukula alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema jopo la maofisa na wapelelezi wameanza uchunguzi kuhusiana na kifo hicho hivyo kuwataka wananchi kuwa watulivu na wenye taarifa zitakazosaidia kumpata muuaji kushirikiana nalo.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *