img

Mtandao wa ngono unavyochochea maambukizi mapya ya VVU

December 4, 2020

 Ni katika Hospitali ya Itamba, Iringa nakutana na Grace Kinyamagoha, Ofisa Muuguzi Msaidizi, ambaye ananieleza namna mtandao wa ngono unavyofanya kazi.

“Anapokuja mgonjwa, akapimwa na kugundulika na virusi vya Ukimwi (VVU), anaulizwa ana wapenzi wangapi, kisha sisi humuomba majina, makazi na mawasiliano ya wapenzi hao, kisha tunawafuatilia,” anasema Kinyamagoha.

Kinyamagoha alishawahi kukutana na kijana wa miaka 41, mwenye wapenzi 16.

Taarifa ya utafiti wa viashiria na matokeo ya Ukimwi kwa mwaka 2016-17 iliyotolewa Aprili 2019, inaonyesha asilimia 5 ya watu wenye umri wa miaka 15 hadi 64 wanaishi na VVU. Idadi kubwa ya watu hao, karibu asilimia 40, hawajui iwapo wana maambukizi au la.

Anasema baada ya mteja kutaja majina na mawasiliano ya wenza, wanawafuatilia walipo kisha wanawapa elimu kabla ya hawajawapima kwa ridhaa yao.

“Kwa mfano, kati ya wale wenza 16 wa kijana A, huenda tukawabaini wasichana wanane wana maambukizi, tunawashauri kisha kila mmoja naye anadodoswa ili awataje wenza wake,” anasema Kinyamagoha.

“Huenda kati ya wale wanane, watatu kati yao kila mmoja ana wapenzi watano tena, na tukiwakifuatiliwa tunabaini wenye VVU, hao pia tunawadodosa na wanawataja wapenzi wao na hapo tunakuwa tumefikia mtandao huo wa ngono.”

Kinyamagoha anasema, ni watu wachache wanaokuja kupata matibabu wanaotaja kuwa na uhusiano na watu wawili au watatu, bali huwa kuanzia wanane hadi 16 au hata 20.

“Anaweza kutaja leo wachache lakini akija kliniki kwa mara nyingine, anataja wenza wengine,” anasema Kinyamagoha.

Anasema nia ya kufuatilia mtandao huo ni kuwafikia wale wote wenye maambukizi na kuhakikisha wanatumia dawa ili kupunguza kiwango cha maambukizi na wale wasio na maambukizi, waondoke katika hatari ya maambukizi.

Kinyamagoha anasema inawezekana kabisa, mgonjwa mwenye wenza saba, wanne kati yao wana maambukizi na watatu hawana maambukizi.

Akizungumzia kuhusu mtandao wa ngono na huduma zinazotolewa, Mshauri Mkuu wa Masuala ya Uzazi wa Mpango na Afya ya Uzazi wa USAID Boresha Afya, Kanda ya Kusini, Dk Ana Themba anasema katika mtandao huo, baada ya kubaini mtu mwenye VVU wanaanza kumpa dawa na kumpima magonjwa yanayoenda na VVU.

“Kwa mfano kwa mwanamke, tunampima saratani ya shingo ya kizazi kwa sababu ni ugonjwa unaoambatana na maambukizi haya hasa kinga inapokuwa chini, tukishabaini ana dalili tunamuanzishia dawa,” anasema Dk Themba.

Pia, anasema huduma nyingine ni kuhakikisha anatumia njia za uzazi wa mpango ili asipate mimba zisizotarajiwa hadi pale afya yake itakapoimarika.

“Kuna wakati inabidi tusimamie pia suala la ukatili wa kijinsia, kuna wagonjwa baada ya kugundulika na VVU wanaogopa kuwaambia wenza wao, kwa sababu anaogopa atapigwa na hata kushindwa kutumia kinga au dawa, lakini tunawahoji wagonjwa na tunafuatilia,” anasema

Bernadetha Msongole, mshauri wa masuala ya VVU USAID Boresha Afya anasema kuna wakati mtu aliyebainika na VVU ana mume lakini bado ana wenza wawili, hapo ni watu watatu wapo katika mtandao.

“Kazi yetu ni kuwafuatilia wana mtandao, kuanzia mume na hadi wale ‘michepuko’ tunachosisitiza ni usiri ili isijulikane nani ametoa namba zao za mawasiliano,” anasema Msongole.

Anasema zipo njia nne za kuwafikia, kwanza, kumshawishi mgonjwa amlete mwenza, pili, mgonjwa kuruhusu mtoa huduma amfuate mwenza na kumpima.

“Njia nyingine ni mwathirika kuja na mwenza na kuwapima wote kwa pamoja, lakini kumpa muda mgonjwa, wa siku 14 ajitafakari na kumshawishi mwenza kwenda kupima,” anasema Msongole.

Anasema, wazo la kuusaka mtandao wa ngono lilitokana na kasi ya maambukizi, awali mtu mwenye VVU akishapimwa na kugundulika, upimaji unaishia kwenye familia.

“Lakini kutokana na tafiti zilizofanywa ikabainika kuwa kuna watu wana wapenzi wengi, (multiple partners) , hata wanne au watano. Hao wenye wapenzi wengi ndiyo walio katika hatari zaidi ya kupata maambukizi,” anasema

Anasema ikaonekana ni muhimu kufuatailia mtandao wa ngono ili kumaliza maambukizi, ni lazima kila mwenye maambukizi, apewe matibabu ili kupunguza nafasi ya kuambukiza wengine .

“Uwezo wa kuambukiza ni mdogo watu wengi zaidi watapimwa na kupewa ushauri wa kujilinda au kutumia dawa,” anasema Msongole.

Wakati huohuo, Desemba mosi mwaka huu, siku ya maadhimisho ya Ukimwi Duniani, Urusi ilitangaza kugundua chanzo ya majaribio ya kutibu VVU.

Novemba mwaka huu, Alexey Mazus, Mtaalamu Mkuu wa masuala ya Ukimwi Urusi, alisema yapo matumaini makubwa kuwa chanjo ya VVU itapatikana siku za karibuni.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *