img

LANGO yawashika mkono wakulima wa mwani Mchinga

December 4, 2020

Na Ahmad Mmow, Lindi.

Imeelezwa kwamba iwapo kutakuwa na jitihada za kusimamia na kuwainua wakulima wa zao la mwani wa kata za Mbanja na Mchinga, manispaa ya Lindi, zao hilo linaweza kuwa ni miongoni mwa mazao yanayoweza kuinua vipato vya wakulima wa zao hilo.

Hayo yameelezwa jana na mkurugenzi wa Mtandao wa Mashirika yasiyo ya kiserikali mkoani Lindi( Lindi Association of Non Governmental Organizations/ LANGO), Michael Mwanga wakati wa mkutano wa mrejesho kwa wadau wa utekelezaji wa mradi  wa Kuimarisha Usawa wa Kijinsia na Kuwawezesha Kiuchumi Wanawake na Vijana. Mkutano ambao umefanyika katika mtaa wa Mchinga moja,manispaa ya Lindi.

Mwanga katika hafla hiyo ambayo pia ilitumika kukabidhi mradi huo kwa wakulima wa mwani wa vikundi sita vilivyopo katika mitaa ya Ruvu, Mchinga moja na Mchinga mbili alisema  endapo kutakuwa na jitihada za wadau mbalimbali wa zao la mwani, zao hilo linaweza kuwa chanzo kikubwa cha uchumi na mapato kwa wakulima wa zao hilo na taifa.

Alisema iwapo wadau watatilia mkazo na kuhamasisha wakulima kuzalisha zao hilo linaweza kuchangia uchumi na vipato vya wakulima. Hivyo kuongeza idadi ya mazao ya biashara.

Alisema nguvu za pamoja za wadau zinahitajika. Kwani pamoja nakuwepo dalili nzuri za kuzalishwa kwa wingi lakini bado kuna changamoto ambazo zinatakiwa kuondolewa. Ikiwano wakulima wazao hilo kutokuwa na chombo cha kuwaunganisha na hata kuwasemea.

Alibainisha kwamba wakulima wa zao hilo katika tarafa hiyo ya Mchinga hawana chama cha msingi cha ushirika ( AMCOS) ambacho kingewaunganisha na kuwasemea nakutumiwa na wakulima wa zao hilo kupata fursa zinazotokana na ushirika kama wakulima wa mazao mengine. Ikiwamo wa korosho na ufuta.

” Kukosekana kwa chama cha ushirika cha kutetea wakulima wa mwani, bei ndogo ya zao la mwani kulingana na kazi wanayofanya, uvuvi haramu wa kutumia uriba(sumu) ambao unaharibu ukuaji wa mwani, na utegemezi wa vikundi kwa wanunuzi na kutojitoa kwa kazi yao ni miongoni mwa changamoto,” Mwanga alibainisha.

Alitoa wito kwa wadau kuwa na muunganiko sahihi utakaorahisisha mawasiliano na utekelezaji wa mipango mbalimbali inayohusu uzalishaji, usimamizi na utatuzi wa changamoto mbalimbali. Kwani hivi sasa hakuna muunganiko katika ngazi mbalimbali baina ya wadau. Hali ambayo inachangia kuwepo ugumu wa kufanikisha matarajio ya wakulima wa zao hilo.

Mbali na hayo mkurugenzi huyo alisema katika kutekeleza mradi huo ambao unafadhiliwa na ushirika la kimataifa la Oxfam na kutekelezwa katika kata za Mbanja na Mchinga kwa kipindi cha miezi 12 ( Januari hadi Desemba 2020), LANGO  imesaidia vifaa vya uzalishaji kwa vikundi 10 vya wanawake na vijana wanaofanya kazi ya kilimo cha mwani. Ambapo limetoa kamba 150 na taitai 400  kwa vikundi sita. Vifaa ambavyo vinathamani ya shilingi 4,500,000.

Kwa upande wake kaimu ofisa mtendaji wa kata ya Mchinga ambae ni ofisa maliasili wa tarafa ya Mchinga, Sharifa Tomela alitoa wito kwa wakulima wa zao hilo wazingatie utunzaji wa mazingira wakati wa uzalishaji.

Alisema licha ya zao hilo kuwa na manufaa kwa wakulima na serikali kutambua juhudi zao katika kujikwamua kutoka kwenye umasikini, lakini lisiwe chanzo cha kuharibu mazingira. Bali wafanye kilimo cha zao hilo kuwa rafiki wa mazingira.

Nae ofisa maendeleo ya jamii wa halmashauri ya manispaa ya Lindi, Idd Maketa alitoa wito kwa wakulima wa zao hilo ambao wapo kwenye vikundi wasajili vikundi vyao. Kwani Ofisi yake ipo tayari kuhakikisha vinasajiliwa ili iwe rahisi kuundiwa vyama vya msingi vya ushirika.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *